Mabomu matatu ya vita vya dunia yagundulika Kolon

Katika mji wa Kolon hapa Ujerumani, limeanza leo zoezi la kuwahamisha watu kutoka eneo kubwa la mji huo, kufuatia kugundulika kwa mabomu matatu ya Marekani ya tangu Vita vya Pili vya Dunia.

Sehemu kubwa ya katikati mwa jiji la Kolon imefungwa kwa hivi sasa ili kutowa nafasi ya kuteguliwa mabomu matatu ambayo hayakuripuka yaliporushwa dhidi ya mji huo wakati wa vita vya pili vya dunia.

 Köln 2025 Zoezi la kuhamisha watu baada ya mabomu kugundulika
Köln 2025 Zoezi la kuhamisha watu baada ya mabomu kugundulikaPicha: Björn Kietzmann/DW

Zoezi hilo ndio kubwa zaidi kufanyika likihusisha kiticho cha bomu tangu mwaka 1945 na zaidi ya watu 20,000 wanalazimika kuhamishwa kwenye eneo la Deutz ambako ni viunga vya mji wa Kolon,ukingoni Mashariki mwa mto Rhine. Mkaazi mmoja alikuwa na maelezo haya kuhusu kuhamishwa.

“Natumai  kwamba ikiwa mabomu ni matatu na tumesambazwa maeneo mbali mbali namna hii,basi tutaweza kurudi majumbani kwetu kukiwa bado kuna mwanga.Kwasababu zoezi hili linaweza kwenda mpaka usiku.”

Taarifa ya mamlaka

Mamlaka za mji huo wa Kolon zimesema kupitia taarifa iliyoandikwa kwenye tovuti yake kwamba shughuli hiyo ya kuhamisha watu ni kubwa zaidi kuwahi kutokea  tangu vilipomalizika vita vya pili vya dunia lakini wanataraji kwamba watafanikiwa kuyateguwa mabomu hayo matatu leo hii hii.

Pamoja na hilo msemaji wa mji huo wenye shughuli nyingi ameliambia shirika la habari la kijerumani dpa kwamba bado haijafahamika ni wakati gani mchakato wa kuteguwa mabomu hayo utaanza.

Vizuizi vya barabara vimewekwa katika maeneo mbali mbali tangu alfajiri ya leo huku maafisa wa usalama wakikaguwa majengo yote yaliyoko kwenye eneo hatari la takriban mita 1000, kujiridhisha ikiwa ni matupu. Maafisa hao pia wamesema pia wamesema huenda ikachukuwa masaa chungunzima kuhakikisha kwamba kila mtu amehamishwa.

Katika jimbo hili la North Rhine-Westphalia ambako inapatikana miji ya Kolon na Bonn kila mwaka hugundulika mabomu kati ya 1500 hadi 2000 ambayo hayajaripuka yaliyovurumishwa kwenye jimbo hili wakati wa vita vya pili vya dunia.

Na kiasi 200 ya mabomu hayo huwa ni yale makubwa kama haya yaliyogundulika huko mjini Kolon kwa mujibu wa Kai Kulschewski ambaye ni mkuu wa shughuli ya uteguaji mabomu katika mji huo.

Maafisa wa ukaguzi mji wakiwa kazini Köln
Maafisa wa ukaguzi mji wakiwa kazini KölnPicha: Henning Kaiser/dpa/picture alliance

Kolon ni miongoni mwa miji iliyoshambuliwa 

Kama ilivyokuwa kwa miji mingine mingi mikubwa ya Ujerumani, Cologne pia ulikabiliwa na mashambulizi makubwa wakati wa vita vya pili vya dunia vilivyomalizika barani Ulaya kwa hatua ya kusalimu amri utawala wa Manazi Mei 8 mwaka 1945.Soma pia: Macron asema Ufaransa haitaki kuchochea “Vita vya Tatu vya Dunia” kutokana na uvamizi wa Urusi

Itakumbukwa kwamba katikati ya mji wa Kolon ni eneo ambalo linakaliwa na idadi kubwa ya watu ikilinganishwa miji mingine ya Ulaya kwa mujibu wa Ralf Mayer mkuu wa shughuli za ukaguzi wa mji huo aliyezungumza na kituo cha habari cha umma ARD.

Kadhalika ni muhimu kufahamu kwamba hivi sasa shughuli ya uhamishaji wakaazi wa eneo hilo imezilenga pia hospitali, majumba wanakoishi wazee waliostaafu na wazee wanaohitaji uangalizi, na makumbusho chungunzima.

Kituo cha treni kwenye eneo la Deutz ambacho pia kinatumiwa na matreni ya safari ndefu kimefungwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *