Mabinti wa Malcolm X wamechukua hatua za kisheria za kulishtaki jeshi la Polisi la Marekani, Polisi ya Upelelezi (FBI) na Shirika la Ujasusi la nchi hiyo (CIA) kwa kumuua baba yao kwa “kukusudia”.
Malcolm Little, ambaye baadaye alikuja kujulikana kama Haj Malik Shabazz na Malcolm X, alikuwa kiongozi mashuhuri wa haki za kiraia wa Wamarekani weusi wenye asili ya Afrika, hadi alipouawa mwaka 1965. Alikuwa pia mwanaharakati mtetezi mkubwa wa haki za Weusi na mwanachama wa zamani wa harakati ya Nation of Islam.
Mabinti wa kiongozi huyo wa Wamarekani weusi, siku ya Ijumaa walifungua kesi katika mahakama ya shirikisho ya Manhattan wakivituhumu vyombo vya usalama vya Marekani kwa kushindwa kwa makusudi kumlinda baba yao na kuzuia juhudi za kuwatambua wauaji wake.
Katika kesi hiyo, walalamikaji wanadai kwamba vyombo vya kutekeleza sheria vya Marekani vilijua kuhusu vitisho vilivyokuwepo dhidi ya baba yao, lakini “vilishindwa kuingilia kati kwa niaba yake.”

Kesi hiyo inasema, mashirika hayo “yaliwaondoa maafisa wao makusudi ndani ya ukumbi” kabla ya Malcolm X kupigwa risasi na kumwacha wazi zaidi aweze kudhuriwa kwa kuwakamata walinzi wake siku chache kabla ya tukio.
Mabinti wa Malcolm wanasema pia kwamba mashirika hayo yalijihusisha na “ufichaji wa kihadaa na ubabaishaji” baada ya mauaji ya Malcolm X kwa kuficha taarifa kutoka kwa familia yake na kuzuia juhudi za kuwatambua wauaji wa kiongozi huyo mashuhuri wa Wamarekani Waislamu wenye asili ya Kiafrika.
Malcolm X alikuwa mwanaharakati wa Kiislamu wa kutetea haki za binadamu ambaye aliwaelezea viongozi wengi waliokuwa na mamlaka ya juu ndani Marekani kama maadui zake, akiwemo mkurugenzi wa wakati huo FBI J. Edgar Hoover.
FBI ilikuwa inamfuatilia kwa karibu Malcolm X na ilikuwa imekusanya taarifa muhimu za kurasa 2,300 kumhusu mwanaharakati huyo.
Mwaka mmoja kabla ya kuuawa Malcolm X, Hoover alituma ujumbe wa telegramu ofisi ya FBI katika Jiji la New York akiwaamuru maajenti wa ofisi hiyo kwa kuwaambia, “fanyeni kitu kuhusu Malcolm X.”
Malcolm X aliuliwa kwa kupigwa risasi Februari 1964 wakati alipoanza kuhutubia ndani ya ukumbi mmoja mjini New York.
FBI na vyombo vingine vya usalama na utekelezaji sheria vilimchukulia Malcolm X kama tishio kwa itikadi ya Ukwezwaji wa Wazungu (White Supremacy) nchini Marekani…/