Mabeki Stars chunga sana mtu huyu

Serhou Guirassy, amekuwa mchezaji muhimu akiibeba Guinea kwenye michuano ya kufuzu Afcon 2025, akiwa amefunga mabao sita katika mechi tatu mfululizo zilizopita huku akiwa kinara wa jumla.

Mshambuliaji anatarajiwa leo kuiongoza Guinea akiaminika kuwa anaweza kuipa kazi ngumu safu ya ulinzi ya Stars chini ya Ibrahim Bacca na Dickson Job kumzuia asifunge, kumbuka hakucheza mechi ya kwanza dhidi ya Stars.

Kuhusu mkakati wa kumzuia straika huyo, kipa wa Stars Aishi Manula, alisema wamemsoma vizuri Guirassy na kama safu ya ulinzi wana kazi ya kuikabili timu nzima.

Guirassy mpaka sasa amecheza mechi nane, huku akifunga mabao sita na kutoa pasi iliyozaa bao moja (assist) kwenye Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) akiwa na Borussia Dortmund ambapo amekuwa akitajwa kuwa mmoja kati ya wachezaji mahiri zaidi kwenye ligi hiyo kwa sasa.

Kinara wa ufungaji kwenye ligi hiyo ni Harry Kane pamoja na Omar Marmoush wakiwa na mabao 11 kila mmoja, huku nafasi ya tatu akishika staa huyo wa Guinea.

Kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Guirassy amecheza mechi nne huku akipachika mabao matatu na kutoa pasi mbili zilizozaa mabao kuonyesha kuwa mabeki wa Stars wanatakiwa kufanya kazi kubwa na kumzuia staa huyo aliyefunga mechi tatu mfululizo kwenye kufuzu Afcon 2025.

Sehrou Guirassy ni mshambuliaji mwenye uwezo mkubwa wa kufunga mabao ya aina nyingi kutokana na umahiri wake wa kiufundi na uwezo mzuri wa kufikiri akiwa uwanjani. Mabao yake mara nyingi huonyesha ufanisi wa hali ya juu kwa staili tofauti:

Mashuti Makali

Anapenda kutumia nguvu kwenye mashuti yake, hasa akiwa ndani ya eneo la penalti. Mara nyingi hupiga mashuti ya moja kwa moja yanayokuwa magumu kwa kipa kuyazuia, hivyo mabeki na viungo wa Stars hawatakiwi kumpa nafasi hiyo.

Mabao ya vichwa

Kutokana na kimo chake na nguvu alizonazo, Guirassy ni hatari sana kwenye mipira ya juu. Ana uwezo wa kuunganisha krosi, kona, na mipira ya adhabu kwa kupiga mipira ya vichwa, jambo pekee ambalo Stars hawatakiwi kufanya ni kuruhusu mipira ya kutengwa au kona ambazo siyo za lazima.

Kumalizia Haraka (One Touch Finishes)

Guirassy ni mwepesi sana kufunga mabao kwa mguso mmoja tu, hasa baada ya kupokea pasi za mwisho kutoka kwa wachezaji wenzake.

Uwezo binafsi

Guirassy ana uwezo wa kujitengenezea nafasi zake binafsi kwa kutumia chenga na nguvu kuwapita mabeki, kisha kufunga mabao ya kuvutia.

Kiwango chake cha ufanisi kinaonyesha kwamba si mshambuliaji wa kutegemea aina moja ya mabao, bali anajua kujibadilisha kulingana na mazingira ya mchezo.

Guirassy alijiunga na Borussia Dortmund msimu huu wa mwaka 2024/2025, akitokea Klabu ya Stuttgart inayoshiriki Ligi Kuu Ujerumani. Ameshacheza kwenye klabu kadhaa kubwa kama Rennes na Amiens zinazoshiriki Ligi Kuu ya Ufaransa.

Guirassy pia amechezea timu za Taifa ya Ufaransa chini ya miaka 20, 19 na 16 ambapo alifunga jumla ya mabao 11 katika mechi 24.