
Manchester, England. Sababu mbili zinafanya mechi ya leo saa 1:30 usiku baina ya Manchester City na Liverpool kwenye Uwanja wa Etihad kuwa ngumu kwa safu ya ulinzi kwa kila timu.
Kwanza ni muendelezo wa kufumania nyavu ambao timu hizo kila moja imekuwa nao katika mechi za Ligi Kuu England (EPL) msimu huu lakini ya pili ni rekodi ya mechi za nyuma baina ya Manchester City na Liverpool kuzalisha mabao.
Manchester City imeziona nyavu za timu pinzani katika mechi 12 mfululizo zilizopita kwenye EPL huku Liverpool ikifanya hivyo katika michezo 22 mfululizo ya ligi hiyo.
Katika mechi tano zilizopita za ligi baina ya timu hizo, zimefungana idadi ya mabao 12 ikiwa ni wastani wa mabao 2.4 kwa mchezo na ni mechi moja tu kati ya hizo ambayo timu moja haikupata bao.
Ushindi leo utaifanya Liverpool izidi kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi ambapo itafikisha pointi 64 wakati kwa Manchester City unaweza kuisogeza hadi nafasi ya pili kwani itafikisha pointi 47 lakini hilo litatimia iwapo Nottingham Forest itapoteza dhidi ya Newcastle United.
Wenyeji Manchester City watawakosa John Stones, Oscar Bobb, Manuel Akanji na Rodri ambao ni majeruhi sababu ambayo itaifanya Liverpool kuwakosa Conor Bradley, Cody Gakpo, Joe Gomez na Tyler Morton.
Kinara wa ufungaji kwenye EPL hadi sasa, Mohamed Salah hapana shaka ndiye mchezaji wa kuchungwa zaidi na safu ya ulinzi ya Manchester City wakati Liverpool yenyewe ikihitajika kumpa ulinzi wa kipekee Erling Haaland anayeshika nafasi ya pili kwa kufumania nyavu katika ligi hiyo akiwa na mabao 19.
Anthony Taylor ndiye atakuwa refa wa kati leo akisaidiwa na Gary Beswick na Lee Betts huku refa wa akiba akiwa ni Andy Madley.
Mchezo mwingine leo utachezwa kwenye Uwanja wa St.James’ Park kuanzia saa 11:00 jioni ambao utazikutanisha Newcastle United na Nottingham Forest.