Mabanati wa Ghaza waendesha ‘Muqawama wa Kiqur’ani’ ili kuzipa nyoyo sakina na utulivu

Kundi moja la mabanati katika Ukanda wa Ghaza limeamua kuweka darsa za kuhifadhi Qur’ani ili kuzipa nyoyo zao sakina na utulivu kwa maneno matukufu ya Mwenyezi Mungu, licha ya eneo hilo kuendelea kuandamwa na mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Mtandao wa Sahab umeripoti kuwa, wazo hilo limebuniwa na dada wawili wa Kipalestina waitwao Ranim na Aayat, ambao umekaribishwa na wasichana na wanawake wa Ghaza.

Dada hao wa Kipalestina wanasema, licha ya hali ngumu inayowakabili, wasichana wengi Wapalestina wa marika tofauti wanataka kuhifadhi Qur’ani. Wasichana hao hupita kwenye barabara zilizochimbika na kubomelewa na juu ya vifusi hadi kufika nyumbani kwa kina Ranim na Aayat kwenye nyumba ambayo nusu yake imebomolewa, ambayo sasa imekuwa madrasa ya kuhifadhia Qur’ani. Pamoja na hayo, wakazi wengi wa eneo hilo wanahofia nyumba hiyo kuja kuripuliwa na kubomolewa kikamilifu na jeshi la Kizayuni.

Renim, ambaye ni mwalimu wa Qur’ani anasema, baadhi ya wanawake wanaojishughulisha na elimu za Qur’ani wameondokewa na wazee na ndugu zao na ameongezea kwa kusema: “licha ya hali ngumu na nzito ya kisaikolojia, tunaendelea kuhifadhi Qur’ani; na hii ni zawadi kubwa kwa kuwepo wasichana walio tayari kuhifadhi Qur’an kwa hamu na shauku kubwa”.

Bibi Sundus ambaye ni mmoja wa wanaojishughulisha na elimu za Qur’ani huko Ghaza anasema: “pamoja na uharibifu na masaibu yanayotupata, tunaendelea kuikabili dhiki yoyote inayotufika. Qur’ani, iwe katika vita au kabla ya vita, ni nuru kwa mwanadamu na inatupa utulivu, nasi tunahisi amani na usalama, badala ya hofu.

Kuhusiana na nukta hii, katika sehemu ya Aya ya 20 ya Suratul-Muzzammil Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

…”فَاقْرَءُوا مَا تَیَسَّرَ مِنَ الْقُرْآنِ ۚ عَلِمَ أَنْ سَیَکُونُ مِنْکُمْ مَرْضَىٰ ۙ وَآخَرُونَ یَضْرِبُونَ فِی الْأَرْضِ یَبْتَغُونَ مِنْ فَضْلِ اللَّهِ ۙ وَآخَرُونَ یُقَاتِلُونَ فِی سَبِیلِ اللَّهِ…”

…Basi someni kilicho chepesi katika Qur’ani. (Yeye Allah) Anajua ya kuwa baadhi yenu watakuwa wagonjwa, na wengine wanasafiri katika ardhi wakitafuta fadhila ya Mwenyezi Mungu, na wengine wanapigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu…

Halikadhalika, Muqawama na subira iliyoonyeshwa na watu wa Ghaza katika kuhimili unyama na ukatili wa mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni na kuomba auni na msaada wa Allah kwa kushikamana na mafunzo ya Qur’ani Tukufu vimewapa uelewa watu wengi duniani wa kitabu hicho kitakatifu.

Mkabala wake, jeshi la utawala wa Kizayuni halijaacha kuchukua kila hatua ya kuipiga vita na kuivunjia heshima Qur’ani na matukufu mengine ya Kiislamu.

Askari washenzi wa Israel wamebomoa Misikiti chungu nzima ya Ghaza na kuivunjia heshima mara nyingi Qur’ani Tukufu, kitendo ambacho kimelaaniwa na Waislamu na watetezi wa haki na heshima duniani…/