
Buchosa. Baadhi ya mabalozi wa CCM wilayani Sengerema, Mkoa wa Mwanza, wanamlalamikia Katibu wa Umoja wa Vijana (UVCCM) Tawi la Majengo, Taratibu Julius, kwa madai ya kuwachangisha Sh810,000 kwa ajili ya kupiga picha za kuwawezesha kupewa baiskeli za ‘Samia’.
Hata hivyo, Julius amekanusha madai hayo alipoulizwa kwa simu na Mwananchi leo Jumanne, Januari 21, 2025 akisema yanavumishwa na maadui zake kisiasa.
“Hizo taarifa si sahihi. Zinatumika na maadui zangu wa kisiasa kunichafua. Mimi nilikuwa napiga picha za viongozi kwa ajili ya kuweka ukutani. Hao mabalozi wameshinikizwa na watu ambao hawanitakii mema,” amesema Julius.
Ameongeza kuwa katika baadhi ya maeneo alilazimika kurejesha fedha alizochukua kwa kuwa picha zilichelewa.
Kutokana na tuhuma hizo, Kamati ya Siasa ya CCM Kata ya Ilenza wilayani Sengerema ilikaa kikao cha dharura kujadili tuhuma zinazomkabili Julius na kumsimamisha uongozi, kisha kumuita kwenye Kamati ya Maadili ili ajibu tuhuma zake.
Akizungumza na Mwananchi leo, Mwenyekiti wa CCM Kata ya Ilenza, Lazaro Lupalika, amedai walifikia uamuzi huo baada ya kumwita mtuhumiwa kwenye kikao cha kamati ya siasa ya kata na kukiri kwa maandishi kuwa alitenda kosa hilo.
Katibu wa CCM Wilaya ya Sengerema, Waridi Josephat, alipozungumza kwa njia ya simu na Mwananchi amesema taarifa za tukio hilo anazo na alitoa maelekezo kwa makatibu wa CCM kata zote kutotoa ushirikiano kuhusu jambo hilo na kutaka lisirudiwe.
Wakizungumza na Mwananchi leo wilayani hapa, baadhi ya mabalozi hao kutoka Kata za Bulyaheke, Luhalanyonga na Ilenza wamesema upigaji wa picha hizo ulifanyika kati ya Desemba 16 hadi 22, 2024.
Bahati Mkama, balozi wa tawi la Majengo, amesema baada ya kupiga picha katika Kata za Ilenza na Luhalanyonga, kijana huyo alihamia matawi ya Lusolelo na Nyangalamila akiendelea kushawishi mabalozi wachange fedha na kupiga picha.
“Alipiga picha za mabalozi wapatao 47 na kukusanya kiasi cha Sh236,000, ndipo baadhi ya viongozi wa chama wa kata hiyo waliposhtuka na kumkamata kwa lengo la kupata taarifa sahihi juu ya uhalali wake wa kufanya kazi hiyo kwa viongozi wa juu wa chama hicho.
“Tunaomba uongozi wa CCM kuanzia ngazi ya kata kumchukulia hatua. Hii ni aibu kwa chama chetu. Viongozi kama hawa hawakubaliki,” amesema Mkama.
Katibu wa CCM Kata ya Bulyaheke, Cosmas Matu, ameliambia Mwananchi kwa njia ya simu kuwa baada ya kumuhoji, Julius alikiri kuwa hakutumwa na kiongozi yoyote, ndipo alipoamuriwa kurudisha fedha hizo.