
Dar es Salaam. Serikali imezindua rasmi mfuko wa ufadhili wa Rais Samia Suluhu Hassan (Samia Scholarship Fund) utakaokuwa endelevu, kwa ajili ya kutoa mafunzo ya ubingwa na ubobezi kwa wataalamu wa afya, huku ikikusudia kuimarisha mfumo wa tehama.
Mfuko huo utahusisha wataalamu wa sekta ya afya wakiwemo madaktari, wataalamu wa dawa za usingizi, maabara, radiolojia na wauguzi.
Hayo yamesemwa leo Jumanne, Aprili 8, 2025 na Waziri wa Afya Jenista Mhagama wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Afya, akisisitiza kundi la wauguzi litapewa kipaumbele, kwakuwa linatoa huduma kwa wagonjwa kwa asilimia 80 baada ya kazi ya upasuaji inayofanywa na madaktari na wataalamu wa dawa za usingizi.
Amesema tangu kuanza kwa ufadhili huo miaka minne iliyopita, Samia Scholarship imetoa kiasi cha Sh30 bilioni kwa kusomesha wataalamu hao.
“Tunakuja na mabadiliko makubwa katika sekta ya afya. Tuna uwepo wa vifaatiba vya kisasa ambavyo vinaweza kutoa huduma za kibingwa na kibobezi, lakini tuna wataalamu wachache eneo hilo wenye uwezo wa kuvitumia.
“Tumefanya tathimini ni magonjwa gani yanahitaji wataalamu zaidi, tumeona katika upandikizaji wa figo, uloto, ini na upasuaji wa mgongo, ubongo, kichwa upasuaji wa moyo kwa njia ya matundu, uimarishaji huduma kwa wagonjwa mahututi, huduma hizi zina namna yake si kila mtu anaweza kuhudumia,” amesema.
Waziri Mhagama amesema sababu ya kukua kwa teknolojia, kwenye vifaa vya uchunguzi wanahitajika wataalamu kwa kuwa wagonjwa wenye dalili wanaongezeka na tiba inatakiwa itolewe kwa wakati pia huduma za dharura zinahitaji ubobezi.
“Tutasomesha wataalamu kwa kuzingatia mahitaji, tutayapa kipaumbele. Wito kwa wataalamu kujitokeza kuomba fursa za kujiendeleza kupitia mfuko huu, wanawake hatujitokezi hili halinifurahishi,” amesema na kuongeza;
“Mafunzo haya yatolewe kwa seti kama ni ubobezi kwenye moyo timu nzima itakayofanya kazi kwenye eneo hilo la tiba ya moyo kuanzia daktari wa usingizi, nesi atakayemhudumia mgonjwa baada na wakati wa upasuaji, maabara za damu au radiolojia wote watasomeshwa.
“Asilimia 80 ya huduma ya tiba inafanywa na muuguzi, ukienda kwenye upasuaji muuguzi yupo daktari akishamaliza ni kazi ya muuguzi kuhakikisha mgonjwa anakua sawa mpaka anaruhusiwa,” amesisitiza.
Amesema tayari MOI wanakusudia kuweka tiba za ubobezi kwa madaktari katika ubobezi wa mifupa ya mikono, miguu, nyonga, kichwa, mgongo na kwamba kila mfupa uwe na wataalamu wake hiyo itawafanya wawe bobezi zaidi katika tiba mbalimbali.
Amesema katika kutimiza hayo, Serikali inazingatia Dira ya Maendeleo ya Taifa, lakini pia Wizara inakusudia kubadilisha Sera ya Afya ya mwaka 2007 kwakuwa hailingani na mabadiliko ya sasa.
Pamoja na hayo, Waziri amesema wanakusudia kuimarisha mfumo wa tehama, ambapo taarifa za mgonjwa zitatunzwa katika mfumo kuanzia hatua ya msingi ya matibabu yake, itakayowawezesha watalaamu ngazi za rufaa kuona taarifa zake za matibabu na dawa alizozitumia awali.
Pia Waziri Jenista amesema unaanzishwa mfumo rasmi wa maoni ya wateja ambao watatoa maoni yao kuhusu upokeaji huduma na iwapo wanaridhika, ambao utazinduliwa hivi karibuni.
Naibu Waziri wa Tamisemi anayeshughulikia afya, Dk Festo Dugange amesema huduma za afya zimeendelea kuboreka kwa kiwango kikubwa nchini, hasa katika eneo la vifaa tiba ngazi za msingi na rufaa.
“Ilikuwa nadra kupata kituo cha afya chenye mashine ya XRay lakini vituo sasa vina mashine hizi, pia asilimia 100 vituo vya afya vina majengo ya upasuaji kwa mama wajawazito, imekuwa historia tumeshasahau kutoa wagonjwa halmashauri kwenda hospitali nyingine ni hatua kubwa tumepiga,” amesema Dk Dugange.
Mganga mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe amesema kumekuwa na kuongezeka kwa upatikanaji wa huduma za afya ngazi ya msingi ambako kuna takribani asilimia 80 mpaka 85 ya Watanzania.
Kumekuwa na uwekezaji katika vifaa na vifaa tiba katika eneo la ubingwa na ubingwa bobezi, kwa sasa Tanzania imeweza kupiga hatua kutoa huduma hizo.
“Tunapata wagonjwa wengi kutoka nje kuja kutibiwa hapa, Tanzania ni nchi iliyoweza kufanya vizuri katika kutokomeza magonjwa yanaweza kuzuilika kwa chanjo kama polio na ulemavu wa ghafla na vifo vya watoto chini ya miaka mitano, tumepunguza kupitia uwezekaji uliofanyika eneo la chanjo,” amesema.
Pia amesema Serikali imeweza kushirikiana na sekta binafsi katika kutoa huduma, na kuongeza ajira miongoni mwa Watanzania.
Dk Magembe amesema idadi ya wananchi wanafika vituoni kupata huduma za afya imeongezeka hali inayoashiria wengi wameacha kujitibu na kuridhika na viwango vya utoaji huduma hospitalini.
“Watoa huduma ngazi ya jamii wamekuwa askari wazuri katika hili. Tunaendelea kuboresha huduma kwa tiba za kisasa.”
Mkurugenzi mkaazi wa WHO Tanzania, Dk Charles Sagoe-Moses amesifu jitihada zinazoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan hasa katika kupunguza vifo vya mama na mtoto kwa asilimia 80 katika kipindi cha uongozi wake.