Wakazi wa miji ya nchi mbalimbali duniai wameendelea kufanya maadnamano ya kuwaunga mkono watu wanaohulumiwa wa Palestina na kulaani jinai zinazofanywa na utawala wa Israel unaotekeleza mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza.
Mtandao wa Sahab umeripoti kuwa, ukurasa wa telegram ya mtandao wa habari wa Quds umeonyesha picha za maandamano yaliyofanywa na wananchi wa Norway katika mji mkuu wa nchi hiyo, Oslo, kulaani jinai za utawala ghasibu wa Israel na kuwaunga mkono wananchi wa Palestina na Lebanon.

Jarida la kila wiki la chama cha The French Workers’ Party nchini Ufaransa limeandika kuwa maelfu ya wakazi wa mji mkuu wa nchi hiyo, Paris wamefanya maandamano kupinga uhalifu unaoendelea kufanywa na Israel dhidi ya watu wa Gaza na Lebanon huku wakipiga nara “Israel, mtenda jinai,” “Idumu Palestina”, “Palestina itaibuka mshindi” na “Israel itashindwa.” Waandamanaji hao huko Paris wametaka kusitishwa vita na mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Gaza na Lebanon haraka iwezekanavyo.
Maandamano mengine ya kuwatetea watu wa Palestina na kulaani mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza na Lebanon yamefanyika katika mji wa Zurich nchini Uswisi, Utrecht, katikati mwa Uholanzi, Bosnia na Herzegovina, Stockholm, mji mkuu wa Uswidi na katika miji mingine mikuu ya nchi za Ulaya.