Maandamano makubwa yafanyika kila pembe ya dunia kulaani mauaji ya kinyama katika Skuli ya Al-Tabeen, Ghaza

Watu katika nchi na mataifa mbalimbali duniani wameandamana kulalamikia na kulaani mauaji ya kimbari na ya kinyama ya Wapalestina yaliyofanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel katika Skuli ya Al-Tabeen katika Ukanda wa Ghaza.

Siku ya Jumapili mtandao wa Telegram wa Kanali ya Quds News ulionyesha picha za maandamano makubwa ya wananchi wa Canada ya kulaani jinai za utawala wa Kizayuni katika Skuli ya Al-Tabaeen katika mji wa Ghaza, ambapo waandamanaji hao walipiga nara za kulaani jinai za utawala wa Kizayuni za kuwaua wanawake na watoto wasio na ulinzi.

Ukurasa wa mtumiaji mmoja wa Palestine Online nao pia ulionyesha katika mtandao wa kijamii wa X taswira za maandamano ya watetezi na waungaji mkono wa Palestina katika mji mkuu wa Malaysia, Kuala Lumpur, ambapo washiriki wa maandamano hayo wameonyesha mshikamano wao na watu wa Palestina na kutaka kukomeshwa mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa katika Ukanda wa Ghaza.

 

Waungaji mkono kadhaa wa Palestina katika miji ya Gothenburg na Stockholm nchini Sweden, katika miji kadhaa ya Uholanzi na jiji la Manchester, nchini Uingereza, nao pia waliandamana kuonyesha mshikamano na watu wa Palestina.

Huko Amman, mji mkuu wa Jordan, watu walikusanyika karibu na ubalozi wa utawala wa Kizayuni na kulaani mashambulizi ya utawala wa Kizayuni katika Skuli ya Al-Tabeen huko Ukanda wa Ghaza.

Unyama na uharibifu uliofanywa na jeshi la Kizayuni katika Skuli ya Al-Tabeen

Waandamanaji walitoa nara za “Waliokuwa wakisali wamekufa shahidi, ni aibu kwa wale wanaochukua hatua ya kuanzisha uhusiano (na Wazayuni)”.

Nchini Morocco pia wananchi waliandamana kupinga mauaji ya kinyama ya Wazayuni katika kambi za wakimbizi wa Kipalestina huko Ghaza.

Huku wakiwa wamebeba bendera za Palestina, waandamanaji hao walitoa nara za “Roho zetu na nafsi zetu ni mhanga kwa ajili ya Msikiti wa Al-Aqsa” na “Baki hai Palestina”.

Siku ya Jumamosi, jeshi la utawala ghasibu wa Israel liliwashambulia kwa makombora waumini wa Kipalestina waliokuwa wakisali Sala ya Alfajiri katika Skuli ya Al-Tabeen katika kitongoji cha Al-Darj katika mji wa Ghaza, ambapo Wapalestina wasiopungua 100 waliuawa shahidi na wengine wengi walijeruhiwa.

Wengi wa waliouawa shahidi katika jinai hiyo walikuwa watoto, wafanyakazi wa serikali, wahadhiri wa vyuo vikuu na shakhsia wa kidini ambao hawakuhusika kwa namna yoyote na harakati za kisiasa au za kijeshi…/