Maana ya ongezeko la simu janja katika huduma za kifedha

Maana ya ongezeko la simu janja katika huduma za kifedha

Hivi sasa, zaidi ya Watanzania milioni 24 wanatumia simu janja (smartphone), sawa na asilimia 35.29 ya watumiaji wa vifaa hivyo, kwa mujibu wa taarifa za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA). Hatua hii ni muhimu katika mchakato wa mageuzi ya utoaji wa huduma za mawasiliano na huduma za kifedha kupitia simu.

Simu janja si tena anasa. Kwa sasa, vifaa hivi vimekuwa zana muhimu za kujipatia kipato, kuweka akiba, kutuma na kupokea fedha, na hata kukopa. Kadri mabadiliko haya yanavyozidi kushika kasi, mfumo wa huduma za kifedha nao unabadilika.

Ikizingatiwa kuwa watu wengi bado wako nje ya mfumo rasmi wa kibenki, simu janja zimekuwa lango jipya la upatikanaji wa huduma za kifedha.

Kwa sekta ya fedha, ongezeko hili linaweza kumaanisha mambo kadhaa:

Kwanza, simu janja ni upenyo unaoweza kutumika kuwafikia kundi kubwa zaidi la watumiaji wa huduma za kifedha. Programu za kifedha (fintech), huduma za benki kwa ajili ya kufanya malipo, kupokea fedha, huduma za kifedha kupitia mitandao ya simu na nyinginezo, zinaweza kuongeza ubunifu wa huduma kuwafikia vijana wa vijijini, wafanyabiashara wa sokoni, wafugaji, na makundi mengine muhimu katika kufanikisha ujumuishi wa huduma za kifedha.

Pili, mfumo wa uwekaji kumbukumbu hauna budi kuimarika. Badala ya mtindo wa kawaida wa kutumia nyaraka na mahojiano ya ana kwa ana, mfano katika kupata mkopo, ubunifu uongezeke katika kuhifadhi na kutumia taarifa kutoka kwenye simu—kama vile historia ya matumizi, miamala, na tabia za matumizi ya pesa—kupima uwezo wa mkopaji. Taarifa hizi zitumike kama nyenzo za kufanya tathmini ya kustahiki huduma za mikopo

Tatu, simu janja zinaongeza urahisi wa kufikisha elimu ya kifedha kwa watu wengi zaidi. Video fupi kwa Kiswahili, jumbe mbalimbali kupitia majukwaa ya kijamii, na programu za kujifunza zinaweza kuchukua nafasi ya warsha, semina, matamasha, na vipeperushi vya karatasi katika kufikisha jumbe na taarifa za huduma za kifedha.

Hii hurahisisha elimu kuwafikia watumiaji wengi kwa muda mfupi. Mtu aweze kujifunza jinsi ya kupanga bajeti, kuepuka utapeli wa mtandaoni, au kuanza kuweka akiba, yote kupitia simu yake tu.

Nne, simu mahiri zinachochea ukuaji wa malipo ya kidijitali. Mfumo wa Lipa Namba, malipo kwa kutumia QR code, na uhamishaji wa fedha kupitia programu umekuwa rahisi zaidi.

Mfanyabiashara wa Kariakoo, Samunge au Ngamiani Tanga hahitaji tena mashine kubwa ya POS; simu tu inamtosha kupokea malipo kutoka kwa wateja na kutuma fedha kwa wasambazaji wake papo hapo.

Vilevile, simu janja zinawapa vijana fursa ya kuanzisha biashara za kidijitali. Maduka ya mtandaoni, wauzaji kupitia TikTok, wauzaji wa Instagram, na watoa huduma mbalimbali wanaendesha shughuli zao kupitia simu pekee.

Biashara na malipo yataendelea kukua na kufanyika mtandaoni, na simu janja zitaendelea kuongeza ufanisi wa hilo

Hata hivyo, changamoto bado zipo. Gharama ya simu janja bado ni kubwa kwa baadhi ya Watanzania. Mtandao wa intaneti haujafika maeneo yote, na wengi hawana ujuzi wa kutumia programu za kifedha kwa usahihi.

Zaidi ya hayo, kuongezeka kwa visa vya utapeli mtandaoni na matumizi mabaya ya taarifa binafsi kunaweza kudhoofisha imani kwa mifumo ya kifedha ya kidijitali.

Ili Tanzania inufaike kikamilifu, taasisi za kifedha zinapaswa kutengeneza huduma zinazolenga simu janja kama kipaumbele, si kama nyongeza. Programu ziwe nyepesi, ziweze kufanya kazi hata bila intaneti, na zitumie Kiswahili.

Serikali na kampuni za mawasiliano waongeze uwekezaji katika miundombinu ya mtandao vijijini, wahimize usalama wa kidijitali, na kuhakikisha simu janja zinapatikana kwa gharama nafuu.

Kwa njia nyingi, uchumi wa Tanzania wa baadaye utaegemea kile ambacho watu wanaweza kufanya kupitia kifaa walichonacho mkononi. Iwe ni mvuvi wa Bagamoyo anayepokea malipo kwa simu au muuza barabarani mjini Morogoro anayepanga bajeti kupitia programu ya simu, simu janja si tena kifaa cha mawasiliano pekee, ni njia ya kuingia rasmi kwenye mfumo wa kifedha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *