
Dar es Salaam. Katika kipindi cha ujauzito,mtoto akiwa tumboni hupitia mabadiliko mengi ya ajabu,na moja ya mabadiliko hayo ni pamoja na ‘Lanugo.
Kwa mujibu wa utafiti wa International Journal of Pediatric Research wa mwaka 2018, Lanugo ni nywele nyepesi zinazokuwa kwenye mwili wa mtoto mchanga, ambapo kazi yake kubwa ni kudhibiti joto la mwili wa mtoto huo.
Utafiti huo, umeeleza kuwa lanugo hukua kati ya wiki ya 16 na 20 ya ujauzito na hukua kwenye maeneo ya uso,mgongo,mikono,miguu na tumbo kwa kipindi chote awapo tumboni.
Ukiachana na kutunza joto la mwili, utafiti huo umeeleza kuwa, lanugo huimarisha mazingira ya mtoto tumboni na kutoa nafasi ya mtoto kushughulikia mabadiliko ya mazingira anapozaliwa.
Tafiti zinaeleza kuwa, lanugo huanza kuanguka baada ya mtoto kuzaliwa, na yote hayo ni mchakato wa ukuaji wa mtoto.
Hata hivyo,kiasi cha lanugo hutofautiana; wapo wenye lanugo nyingi na wengine chache.
Kwa mujibu wa utafiti uliochapishwa kwenye jarida la Pediatrics mwaka 2010, nywele hizo husaidia mfumo wa kinga wa mtoto kwa kujilinda dhidi ya maambukizi ya magonjwa na maambukizi katika mazingira ya mimba.
Aidha, baadhi ya tafiti, zimefafanua kuwa, ikiwa lanugo hazitoota kipindi cha ujauzito, ni ishara mbaya na jambo lisilo la kawaida kwa mtoto aliye tumboni.
Baadhi ya sababu za kutoota kwa lanugo ni pamoja na mabadiliko ya homoni za mama,mtoto kuwa njiti na athari za kimazingira.
Kwa mujibu wa tafiti, mabadiliko ya homoni za ‘estrojeni’ na ‘progesterone’ kwa mama, mama kuwa na upungufu wa virutubisho au matatizo ya afya, husababisha mtoto kukosa nywele hizo zinazohifadhi joto la mtoto kipindi cha ujauzito.