
Dar es Salaam. Je, wewe ni mmoja kati ya watu wanaopenda kutumia uongo ili kupata kitu au kujinasua katika changamoto fulani unayopitia?
Unafahamu kuwa na tabia ya kupenda kusema uongo pamoja na kutokubalika katika dini na jamii kwa ujumla, inaweza kukuweka katika hatari ya kupata msongo wa mawazo?
Kwa mujibu wa maandiko, tafiti na wataalamu mbalimbali wa saikolojia kupenda kusema uongo kutakujengea tabia ya kuwa na hofu, kutoaminika katika jamii, migogoro na watu mbalimbali hivyo kukuweka katika hatari ya kupata changamoto za afya ya akili.
Maandiko pia yanasisitiza juu ya umuhimu wa kupenda kusema ukweli na namna unavyosaidia katika kuimarisha afya ya akili.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Chama cha Wanasaikolojia wa Marekani, kwa kushirikiana na mkufunzi wa masuala ya saikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Notre Dame, Lijuan Wang na kuchapishwa katika tovuti ya Psychological Today, ukweli unasaidia kuimarisha afya ya akili.
Utafiti huo ulihusisha watu takribani 72 na kuwagawanya katika makundi mawili ambapo kundi moja liliagizwa kusema ukweli pekee, na kundi la pili likipewa uhuru wa kusema lolote kwa takribani wiki 10.
Ilionekana baada ya wiki 10 kuwa wale waliosema ukweli walifaidika zaidi kiafya, walionyesha uhusiano mzuri na wapendwa wao. Walipata unafuu wa msongo wa mawazo, maumivu ya kichwa yalipungua na hawakuwa na hisia za majuto au kujilaumu.
Kiutafiti, kusema uongo kunamuweka mtu katika hatari kupata msongo wa mawazo, hofu, uzito mkubwa kupindukia, kutokuwa na uhusiano mzuri na watu pamoja na kupunguza ufanisi wa kazi.
Sababu ya kusema uongo
Baraka Shabani mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam amesema baadhi ya watu, hulazimika kusema uongo ili wapate kitu fulani au kujiokoa katika hatari.
Amesema katika mazingira fulani, mtu ili aweze kupata kitu anachokihitaji, analazimika kusema uongo.
Ameeleza kuwa hiyo inatokana na hulka kwa baadhi ya watu katika jamii, kuamini kile wanachoambiwa uongo kama kweli huku wakishindwa kuwa na imani na kile wanachoambiwa kama ukweli.
Ametolea mfano wa mwanamume anayemtaka mwanamke anayependa fedha ilhali hana kitu.
“Ili kumpata inabidi nidanganye na kuigiza kama nina uwezo mzuri wa kifedha, maana nikimueleza ukweli mwanzoni siwezi kumpata, ”ameeleza.
Kwa upande wake, Anna Zebedayo amesema tabia ya mtu kupenda kusema uongo katika kila jambo lake, linaanzia katika misingi ya malezi yake.
Amesema pengine katika malezi yake tangu akiwa mtoto amekuwa akisema uongo bila ya kuonywa na kuelezwa kwa nini kusema uongo siyo jambo zuri.
“Pia wakati mwingine amekuwa akiona watu wanaomzunguka wakisema uongo bila kuonywa wala kupatwa na chochote, kutokana na mtoto hujifunza zaidi kwa kile anachokiona, anaweza kuuchukua uongo na kuufanya kama sehemu ya maisha yake, ”ameeleza.
Ukweli unavyosaidia kuimarisha afya ya akili
Mwanasaikolojia Modesta Kamonga, amesema kupenda kusema ukweli si tu ni jambo la kimaadili, bali pia lina manufaa makubwa kwa afya ya akili.
Ametaja baadhi ya manufaa hayo ni pamoja na kumuepusha mtu kupata msongo wa mawazo pamoja na kutokuwa na hofu.
“Hofu ya kugunduliwa kuwa umesema uongo husababisha mtu kuwa na wasiwasi na huzuni, jambo ambalo halina afya kwa ustawi wa afya ya akili. Mtu anaposema ukweli huwa huru na kuwa na amani jambo linalochangia afya njema ya akili, ”amesema.
Amesema kuwa mtu anayependa kusema ukweli hujenga uhusiano mzuri, iwe wa kifamilia, kirafiki au kikazi, kwani uhusiano huo hujengwa juu ya misingi ya uaminifu.
“Mtu anayesema ukweli huaminika zaidi na hivyo hujenga uhusiano wenye nguvu na wenye afya, ”amesema na kuongeza kuwa msema kweli hujiamini na hufanya uamuzi sahihi.