Ushindi ambao Yanga na Simba zimeupata juzi Jumamosi na jana Jumapili umezihakikishia timu hizo kutinga hatua ya makundi ya mashindano ya klabu Afrika.
Yanga iliyoifunga CBE ya Ethiopia kwa mabao 6-0 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar Jumamosi, imetinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa ushindi wa mabao 7-0 baada ya kushinda mechi ya kwanza ugenini ya raundi ya pili ya mashindano hayo dhidi ya wapinzani wao hao kutoka Ethiopia.
Simba ambayo jana Jumapili imeifunga Al Ahli Tripoli ya Libya kwa mabao 3-1, imetinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa matokeo ya jumla ya ushindi wa mabao 3-1 baada ya timu hizo kutoka sare ya bila kufungana katika mechi ya kwanza iliyochezwa Libya.
Droo ya upangaji wa hatua ya makundi kwa mashindano hayo yote mawili itachezeshwa Oktoba 7 huko Cairo, Misri.
Kuna mambo sita ambayo yanaweza kuwa ya kushangaza baada ya timu ambazo zitashiriki hatua ya makundi ya mashindano ya klabu Afrika sambamba na Simba na Yanga kujulikana.
Jambo la kwanza ni kuwa katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, kuna timu 10 ambazo zimeshawahi kukutana na Yanga kwenye mashindano ya klabu Afrika hapo nyuma huku kwenye Kombe la Shirikisho Afrika kukiwa na timu tano ambazo zimewahi kukutana na Simba katika mashindano tofauti ya klabu Afrika.

Timu 10 ambazo zimewahi kukutana na Yanga kwa nyakati tofauti hapo nyuma ambazo zimeingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu ni Al Ahly, Esperance, Mamelodi Sundowns, TP Mazembe, CR Belouizdad, Raja Casablanca, Pyramids FC, Al Hilal, Sagrada Esperanca na MC Alger.
Timu tano zilizotinga hatua ya makundi katika Kombe la Shirikisho Afrika ambazo ziliwahi kukutana na Simba hapo nyuma kwenye mashindano tofauti ya klabu Afrika ni Al Masry, Zamalek, RS Berkane, Asec Mimosas na Enyimba.
Jambo la pili ni kuwa kila kanda ya soka Afrika, imepata mwakilishi katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kukosekana kwa timu kutoka kanda ya kati ya soka Afrika (Uniffac) katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ni jambo la tatu la kushangaza.
Hii ni mara ya kwanza baada ya misimu 14 kwa kanda hiyo kutokuwa na timu kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho tangu 2010 ambapo haikuingiza pia.
Jambo la nne ni timu mbili za Tanzania kwa mara ya kwanza kuwekwa katika vyungu ambavyo hazikuwahi kuwepo katika upangaji wa droo ya makundi ya mashindano ya klabu Afrika.
Kwa mara ya kwanza, Yanga itakuwa katika chungu cha pili kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ambacho kitakuwa na timu za CR Belouizdad, Raja Casablanca na Pyramids wakati Simba kwa mara ya kwanza itakuwa katika chungu cha kwanza kwenye Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa na timu za Zamalek, RS Berkane na USM Alger.
Simba kushiriki hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu kunaifanya iandike rekodi ya kuwa timu pekee Tanzania na Afrika Mashariki kucheza hatua ya makundi ya Mashindano ya klabu Afrika mara sita mfululizo ambazo ni nyingi zaidi kuliko timu nyingine yoyote Afrika.
Jambo la sita la kushangaza ni uwepo wa timu tisa ambazo zinashiriki kwa mara ya kwanza katika hatua ya makundi ya mashindano ya klabu Afrika.
Katika ligi ya mabingwa Afrika, timu tatu zinashiriki kwa mara ya kwanza hatua ya makundi ambazo ni Sagrada Esperanca, Maniema na Stade d’Abidjan.
Kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, timu sita ambazo zinashiriki kwa mara ya kwanza hatua ya makundi ni ASC Jaraaf, Bravos Maquis, Lunda Sol, Orapa, Black Bulls na Stellenbosch.Caf