Dar es Salaam. Kama mara yako ya mwisho kufika Dar es Salaam ni miaka 10 iliyopita, pengine unahitaji mwenyeji wa kukupokea na kukuelekeza maeneo mbalimbali ya jiji hili.
Hilo linatokana na ukweli kwamba karibu kila kitu kimebadilika, kuanzia barabara, majengo marefu kwa mafupi, na hata kuwapo kwa miji mipya, kumeibadili Dar es Salaam kwa kiwango kikubwa.
Baadhi ya maeneo yaliyoonekana ya kawaida zamani sasa ni kivutio, kiasi cha watu kuyatumia kupiga picha wakiambatanisha na maelezo kuwa hii ni Tanzania, si nchi za nje.
Ujumbe huo ni tafsiri inayobeba uhalisia wa mfanano wa baadhi ya maeneo ya jiji hilo na miji mingine ya mataifa ya nje, ambayo aghalabu ilitumika kama mfano kwa uzuri.
Barabara ya Bagamoyo, kuanzia eneo la Sayansi hadi Morocco katika Wilaya ya Kinondoni, ni kielelezo cha maeneo yaliyopitia mabadiliko ya mandhari kiasi cha kushangaza.

Mvuto wa eneo hilo umetokana na nyumba za ghorofa zilizojengwa kwa mpangilio, nakshi za aina yake, na barabara iliyonyooka. Hakika, Dar es Salaam ya leo sio ya jana.
Kama unastaajabu mwonekano wa mchana, utakachokiona usiku kitakushangaza zaidi. Ni mvuto unaoambatana na mwangaza wa taa zenye mitindo mbalimbali katika kuta na baraza za maghorofa.
Badala ya Posta iliyozoeleka kama makao makuu ya ofisi mbalimbali, kwa sasa eneo hili ndiko yaliko makao makuu ya kampuni mbalimbali.
Migahawa yenye hadhi ya kipato cha kati na juu ndizo ofisi nyingine zinazopatikana katika eneo hilo, ikiwa ni tafsiri halisi ya mabadiliko ya jiji.
Mabadiliko ya Dar es Salaam hayahusishi majengo peke yake. Mawasiliano ya barabara za zege na lami katika mitaa mbalimbali ni jambo jingine litakalokupoteza kama hujakanyaga jiji hili kwa miaka kadhaa.
Kama hiyo haitoshi, madaraja na barabara za juu sio Afrika Kusini na Kenya pekee, hadi Dar es Salaam zinapatikana kwa sasa. Lipo lile la Kijazi Interchange lililopo Ubungo, Daraja la juu la Mfugale, Daraja la Juu Kurasini, na Uhasibu.

Unapoingia Dar es Salaam kwa njia ya Morogoro, unakaribishwa na makutano ya barabara ya Kijazi (Kijazi Interchange), lile eneo lililokuwa kitovu cha msongamano wa magari, sasa ni kuteleza tu.
Achilia mbali kuleta mandhari murua, ujenzi wa barabara hizo uliofanyika kwa vipindi tofauti umesaidia kupunguza msongamano wa magari, hivyo kurahisisha maisha ya wananchi.
Ujenzi wa barabara za lami katika mitaa mbalimbali ulioambatanishwa na uwekaji wa taa za barabarani ni moja ya vitu vilivyolifanya jiji hili libadilike.
Madaraja ya juu
Daraja la Mfugale ndilo lililokuwa la kwanza kujengwa na kisha kuzinduliwa Septemba 28, 2018.
Ujenzi wa daraja hilo ulilenga kuondoa foleni kwa watumiaji wa barabara wanaotoka katikati ya jiji kwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na wale wanaotoka Ubungo kwenda bandarini na Mbagala.
Siku ambayo daraja hilo lilizinduliwa ndipo ujenzi wa daraja la juu la Chang’ombe ulitangazwa, lengo likiwa ni kuendelea kuboresha na kuondoa foleni. Awali, baada ya kutatuliwa Tazara, shida ilihamia Chang’ombe.

Hata hivyo, changamoto imeendelea kubaki katika eneo la kutoka Buguruni kuvuka kwenda Temeke na Kurasini, kwani bado foleni imeendelea kuwa kubwa katika baadhi ya siku na saa.
Mbali na ujenzi huo, pia mkakati wa kumaliza foleni katika jiji ulihamia kwenye mradi wa makutano ya barabara ya Ubungo maarufu Kijazi Interchange na baadaye Kurasini.
Jitihada hizo zilikwenda mbali zaidi na sasa watu wanaotoka Posta kwenda Masaki hawalazimiki
kupita Daraja la Selander, badala yake kuna daraja jipya la Tanzanite.
Mbali na kupunguza msongamano, pia limekuwa kivutio kipya cha utalii kutokana na jinsi lilivyojengwa likichuana kwa ubora na uzuri na lile la Julius Nyerere linalounganisha Kurasini na Kigamboni, ambalo pia limekatisha baharini.
Haya yote yaliyofanyika yamebadilisha mandhari ya jiji la Dar es Salaam na kulifanya kuwa jipya.
Barabara za mitaa
Mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam Awamu ya Pili (DMDP) nao umechangia kwa kiasi kikubwa kulifanya jiji hilo kuwa na mwonekano wa kuvutia katika baadhi ya maeneo.
Chini ya mradi huo, barabara za lami zimejengwa katika maeneo tofauti ambayo awali isingekuwa rahisi kupitika. Kwa sasa, yamewekwa taa na kuongeza mvuto na urahisi wa usafiri kwa wananchi.
Eneo kama Mtoni Kijichi na Mbagala Kuu, ambalo linatajwa kuteuliwa kuwa la mfano, ni sehemu ambayo uwekaji wa barabara za lami umebadilisha asilimia 90 ya mwonekano wake na kwa kiasi kikubwa hata aina ya maisha.
Miundombinu hiyo imeongeza sifa ya eneo hilo na mtazamo wa watu juu ya wenzao wanaoishi humo umebadilika. Sasa wanaonekana kuwa wenye maisha bora tofauti na awali.
Uboreshaji huo ulikwenda sambamba na ujenzi wa daraja linalounganisha Vikunai na Kigamboni, ambalo pia linatumika kama njia ya haraka kwa wale wanaotoka Mbagala kwenda maeneo ya karibu, ikiwamo Toangoma.

Baadhi ya maeneo mengine yaliyoboreshwa chini ya mradi wa DMDP ni Temeke, Buza, Kinondoni, Tabata, na baadhi ya masoko katika Wilaya ya Temeke na Kinondoni.
Pamoja na mafanikio hayo, bado yapo maeneo mengine yana hali mbaya, hasa Jimbo la Ukonga, kwani barabara zake nyingi ni mbovu. Hali hii huwa changamoto kubwa kwa wananchi, hasa wakati wa mvua.
Mfano halisi ni barabara inayoanzia Banana kuelekea Msongola, ambayo ina hali mbaya licha ya kuwapo kwa Hospitali ya Wilaya ya Ilala (Kivule) katika eneo hilo, licha ya kuwa tegemeo kubwa kwa wananchi wengi.
Mkazi wa Kivule, Fremu Kumi, Angel Wambura, anasema barabara ya eneo hilo ni changamoto kubwa kwa wananchi, hasa mvua zinaponyesha, kwani hali inakuwa ngumu zaidi.
“Kutokana na ubovu wa barabara, daladala zinakatisha safari. Kuna daladala ambazo ruti yake ni Fremu Kumi–Machinga Complex au Mnazi Mmoja, lakini hazifiki mwisho kutokana na ubovu wa barabara. Sasa kipindi cha mvua hali ndiyo huwa ngumu zaidi, na nauli zinakuwa maradufu. Serikali nayo iwakumbuke wananchi wanaoishi huku kwa kuwaboreshea barabara.
“Eneo hili lina hospitali ya wilaya, baada ya Hospitali ya Amana kuwa ya rufaa ya mkoa. Hivyo, kutokana na ubovu wa barabara, inakuwa vigumu kwa wananchi kwenda kupata huduma kwa wepesi,” anasema.
Anataja maeneo korofi zaidi ni Matembelea ya Kwanza na Kizuiani kuelekea Kitunda Shule. Pia eneo kuanzia Sirari kuelekea Msongola.
Magomeni Kota
Sina shaka kama uliwahi kuishi Dar es Salaam, unakumbuka taswira ya Magomeni inayounganisha Mwembechai na Usalama, eneo lililokuwa na nyumba za watumishi wa umma wa enzi hizo—Magomeni Kota.
Ninaposema watumishi wa umma wa enzi hizo, na nyumba hizo ziliakisi enzi haswa, maana ni mithili ya mabanda yanayotumika kama kambi za siku kadhaa na wakati wowote ungedhani zinaanguka.
Mambo hayako hivyo tena kwa sasa; eneo hilo limetapakaa nyumba zenye ghorofa sita na ndani yake kuna kila huduma kwa ajili ya kukidhi haja ya kaya 644.
Wakati wa uzinduzi wake, Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ulisema mradi huo wa nyumba za ghorofa una uwezo wa kuchukua kaya 644.
Kadhalika, kuna eneo la uwekezaji la Machinga Center ambalo lina vizimba 286, vyoo vya kulipia na uwekezaji wa sakafu juu na chini. Zilizinduliwa Machi 23, 2022, na Rais Samia Suluhu Hassan.

Barabara za mwendokasi
Ujenzi wa barabara za mabasi yaendayo haraka ni jambo lingine lililobadili sura ya Jiji la Dar es Salaam. Huduma hiyo imekuwa kivutio si kwa watu wa ndani pekee, bali hata mataifa mengine ya Afrika yamefika nchini kuona namna huduma hiyo inavyoendeshwa.
Baada ya kukamilika katika eneo hilo na kutoa huduma kwa miaka kadhaa, mradi huo umeanza kutanuka, na hivi karibuni wakazi wa Mbagala na maeneo ya jirani wataanza kunufaika.
Kwa mujibu wa Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, awamu ya pili ya ujenzi wa barabara za mabasi yaendayo haraka kutoka Gerezani hadi Mbagala Rangi Tatu umekamilika.
Mradi huo unahusisha ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita 20.3, vituo 27, barabara za juu tatu na njia za maji za chini zenye urefu wa kilomita 40.
Mradi huo hauishii hapo. Ulega anasema hayo wakati akikagua ujenzi wa awamu ya tatu ya barabara ya kiwango cha zege ya mabasi yaendayo haraka kutoka Posta ya zamani hadi Gongo la Mboto yenye urefu wa kilomita 23.3, utakaogharimu Sh231 bilioni, unaotarajiwa kukamilika Aprili mwakani.
Pia, ujenzi unaendelea kutoka katikati ya mji kwenda Tegeta na Mwenge hadi makutano ya Morogoro (Kijazi Interchange-Ubungo).
Barabara za njia nane, nne
Moja ya vitu vilivyobadili mandhari ya Dar es Salaam ni ujenzi wa barabara za njia nane wenye urefu wa kilomita 19.2 kuanzia Kimara hadi Kibaha.
Kati ya njia hizo, tatu zinatumiwa na magari yanayoelekea mikoani na tatu yanayoingia Jiji la Dar es Salaam, na mbili za katikati ni mahsusi kwa ajili ya mabasi yaendayo haraka.
Miundombinu hiyo iliyogharimu zaidi ya Sh161 bilioni imefanya maisha ya wakazi wa Kibaha wanaofanya shughuli zao Jiji la Dar es Salaam kuwa rahisi, kwani foleni iliyokuwa mwiba hivi sasa haipo.
Hiyo haina tofauti na upanuzi wa barabara kuanzia Morocco hadi Mwenge, ambao kujengwa kwake kulitokana na amri ya aliyekuwa Rais wa Tanzania, hayati John Magufuli, baada ya kufuta shamrashamra za sherehe ya Uhuru Desemba 2015 na kuamuru Sh4 bilioni zilizokuwa zimetengwa zitumike kugharimia ujenzi huo.
Kwa hiyo, kama unajijua hujafika Dar es Salaam kwa miaka 10, badili fikra zako. Manzese, Kijitonyama, Magomeni, Mbezi, Kigamboni na maeneo mengine mengi uliyokuwa na picha zake kichwani, zifute; fika upate picha na taswira mpya za jiji hili.
Bernard Kiluwa, mkazi wa Mkoa wa Katavi, anasema mara ya mwisho kufika Dar es Salaam ni wakati kituo cha daladala kipo Ubungo, nyuma ya Tanesco, tofauti na sasa kuwa Mawasiliano.
“Nilipotea. Nilipoambiwa hapa ndiyo Ubungo, daraja, kituo hakipo, barabara zilivyojengwa, nilishindwa kujizuia kuuliza hapa ni wapi kila wakati,” anasema.
Anasema hata ujenzi wa barabara ya njia nane ya Kimara hadi Kibaha umefanya maeneo mengi kuwa na muonekano wa tofauti kuliko ilivyokuwa imezoeleka.
“Eneo kama Mbezi kwa Msuguri, Stop Over, Kimara Bucha, watu walikuwa wakipanga biashara zao hadi barabarani, na ilikuwa ni alama kwetu. Tukiwaona tunajua hapa ni sehemu fulani, sasa hivi kondakta asipotaja vituo unapotea,” anasema Bernard.
Barabara ya Bagamoyo
Lakini siyo kusafiri tu na kurudi ndani ya Jiji hili la Dar es Salaam ndiko kumefanya baadhi ya watu kushangaa kubadilika kwa maeneo hayo, bali hata wale waliopo ndani ya jiji wakati mwingine hushangaa kilichofanyika.
“Hili eneo la Makumbusho hadi Morocco nilikuwa nina muda sijapita hiyo barabara. Nilianza kwa kuona picha mtandaoni, nikajua ni nje ya nchi. Nilipojaribu kufuatilia maoni, nikagundua ni Tanzania, tena Dar es Salaam, ndipo niligundua nina siku nyingi sijatembea,” anasema Grace Richard.
Anasema mara nyingi amekuwa mtu wa kutoka nyumbani kwake Mbagala kwenda Posta kazini, huku akieleza kuwa kupanuka kwa mji kumefanya huduma nyingi zilizokuwa zikifuatwa sehemu fulani kupatikana karibu kila eneo, jambo linalofanya watu wasiende maeneo mengine.
“Kumebadilika. Miaka sita nyuma na sasa kulivyo, ukimuonyesha mtu hawezi kuamini,” anasema Richard.

“Kuna wakati ulikuwa unaweza kusubiri hadi saa zima ili upite hapa mataa ya Uhasibu. Japokuwa ujenzi wa hili daraja la juu haujakamilika, ila tumeshaanza kuona tofauti. Magari yanayotoka Mbagala kwenda Posta hayakai foleni,” anasema Qauthar Alhamdu, mkazi wa Kijichi.
“Ni hatua kubwa, kwani hili limepunguza hata muda tunaoutumia barabarani kwenda kazini. Tunaamini ujenzi ukikamilika, foleni itapungua zaidi,” anasema.