Maagizo matano ya Serikali kwa kampuni inazomiliki hisa chache

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Profesa Kitila Mkumbo ametoa maagizo matano kwa wakurugenzi ambao Serikali inamiliki hisa chache, ili kuongeza ufanisi na mchango wake.

Maagizo hayo ni bodi kuja na mikakati thabiti ambayo itaboresha utendaji wa kampuni na kuongeza faida, kuongeza ushirikiano na sekta binafsi, kuoanisha mikakati yao ya kibiashara na vipaumbele vya kiuchumi vya Taifa, kuangalia namna ya kukumbatia mageuzi ya kidijitali, pamoja na utawala bora utakaopelelekea uwajibikaji, uwazi na uongozi unaozingatia maadili.

Ametoa maelekezo hayo wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa wakurugenzi wa bodi za kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa hisa chache yaliyofunguliwa leo Machi 26, 2025 Kibaha mkoani Pwani.

Profesa Mkumbo amesema Ofisi ya Msajili wa Hazina inasimamia jumla ya taasisi 308 ambapo kati ya hizo 56 ni zile ambazo Serikali ina umiliki wa hisa chache.

Kupitia taasisi hizo uwekezaji wa Sh86.3 trilioni umefanywa huku na kati ya kiasi hicho Sh2.9 trilioni zikiwekezwa kwenye kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa hisa chache na Sh83.4 trilioni kikienda kwa taasisi ambazo Serikali ina umiliki wa asilimia 100.

“Tunataka tuone matunda ya uwekezaji huu na ndio maana nawataka mfanye kila liwezekanalo kuongeza ufanisi wa taasisi zenu,” amesema Profesa Mkumbo.

Ametoa kauli hii wakati takwimu zikionyesha kuwa gawio linalotolewa kwa Serikali kutoka katika taasisi hizo limeongezeka kwa kutoka Sh58 bilioni mwaka 2019/20 hadi kufikia Sh195 bilioni mwaka 2023/24.

“Hii ni ishara ya uthibitisho wa nia ya dhati ya kampuni hizo kuunga mkono jitihada za Serikali katika kutengeneza mazingira rafiki ya biashara,” amesema Profesa Mkumbo.

Alitumia nafasi hiyo kuzitaka taasisi hizi kuendelea kuchangia zaidi ili kutimiza lengo la Serikali la kuongeza mapato yasiyo ya kikodi kutoka kwa taasisi inazomiliki kwa asilimia 100 na zile inazomiliki kwa hisa chache.

 Serikali imejidhatiti kuongeza mapato hayo kutoka asilimia tatu za sasa hadi kufikia asilimia 10 ndani ya kipindi cha miaka mitano.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dk Tausi Kida amesema dhamira ya Serikali ya kuendelea kutengeneza mazingira rafiki ya biashara ili kuongeza mchango wa taasisi zake na zile ambazo ina umiliki wa hisa chache.

“Tunatarajia kuzindua mpango wa pili wa maboresha ya mazingira ya biashara ‘blueprint’ wiki ijayo ikiwa ni ishara ya dhamira ya Serikali ya kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini,” alisema Dk Kida.

Amesema lengo la kuzinduliwa kwa mpango huo ni kuainisha changamoto za wakati huu na kuzitatua ili kuchochea uwekezaji nchini.

Naye Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu amesema mkutano huu unalenga kutoa nafasi ya majadiliano kuhusu mchango wa teknolojia linapokuja suala la maamuzi yatokanayo na takwimu na ufanisi wa taasisi.

Amesema Ofisi ya Msajili wa Hazina inaona haja ya wakurugenzi wa bodi za kampuni ambazo Serikali ina hisa chache kukumbatia mageuzi ya teknolojia.

“Tanzania sio kisiwa, hivyo wakurugenzi wetu wanapaswa kujiandaa kuongoza taasisi zao kwa kutumia maono yanayoendana na mabadiliko ya teknolojia ulimwenguni,’ amesema Mchechu.

Mchechu amesema matarajio yake ni kuona majadiliano yatakayofanyika katika mafunzo hayo yatengeneze mazingira bora kwa maofisa watendaji wakuu na wakurugenzi ili waweze kutumia teknolojia kwa ufanisi na hivyo kuongeza tija ya taasisi wanazoziongoza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Lightness Mauki anayesimamia Utendaji, Ufuatiliaji na Tathmini-Mashirika ya Kibiashara amesema kwa kipindi cha miaka minne iliyopita gawio kutoka kwa kampuni ambazo Serikali ina hisa chache limekuwa likikua kwa wastani wa asilimia 50 kila mwaka.

“Naamini mchango wa kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa hisa chache unaweza kuongezeka mara dufu kwa mwaka huu wa fedha kwani takwimu za hivi karibuni zimekuwa za kuridhisha,” amesema Mauki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *