Kuendelea mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Lebanon kumeitumbukiza nchi hiyo katika mgogoro wa kimazingira na kiafya.
Kanali ya Sahab imelinukuu shirika la utangazaji la Iran (IRIB) na kuripoti kuwa, kuendelea mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya aghalabu ya vitongoji na vijiji vya kusini mwa Lebanon ambavyo vinategemea kilimo ni tishio la moja kwa moja kwa usalama wa chakula na maji katika eneo hilo; ambapo athari zake zinaweza kudumu kwa miaka kadhaa.
Mashambulizi ya ndege za kivita za jeshi la utawala wa Kizayuni dhidi ya miundombinu na rasilimali za maji nchini Lebanon yamesababisha moja kwa moja na kwa njia isiyo ya moja kwa moja mgogoro wa afya ya umma huko Lebanon.
Habari nyingine kutoka Lebanon inaeleza kuwa, ndege isiyo na rubani ya Israel ilishambulia eneo karibu na kituo cha upekuzi cha jeshi katika mji wa Saida kusini mwa Lebanon na kuuwa shahidi watu watatu.
Watu 6, wakiwemo wanajeshi 4 wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa kusini mwa Lebanon (UNIFIL) pia wamejeruhiwa katika shambulio hilo.

Ndege za kivita za jeshi la utawala wa Kizayuni pia zimeshambulia kliniki moja katika eneo la al Sarafand kusini mwa Lebanon na kusababisha uharibifu katika kituo hicho cha afya.