Ma-DC watwishwa mzigo utatuzi wa migogoro familia, ardhi

Ruangwa. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wakuu wa wilaya kuhakikisha wanasimamia utatuzi wa migogoro ya wosia, ardhi na ile ya kifamilia kwenye maeneo yao.

Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo kwenye uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya msaada wa kisheria ya Mama Samia leo Februari 19 2025 katika uwanja wa Madini wilayani Ruangwa Mkoa wa Lindi.

Amewataka wakuu wa wilaya kwenda kusimamia ipasavyo majukumu yao kwa viongozi watakao kwenda kutoa msaada wa kisheria wa Mama Samia Aid Campain.

Majaliwa amesema wakuu hao wana jukumu la kusimamia maeneo yao kuhakikisha kampeni hiyo inaondoa changamoto za migogoro mbalimbali ya kisheria.

“Niwaombe wakuu wa wilaya kwenda kutoa ushirikiano mzuri kwa viongozi watakaokuja kutoa msaada wa kisheria hasa kwenye migogoro ya wosia, ardhi  pamoja na migogoro ya kifamilia,” amesema.

Amesema lengo la kuanzisha kampeni hiyo ni kuondoa migogoro yote kwenye jamii huku akiwataka wananchi kuhakikisha wanaandika wosia ili kupunguza changamoto hizo kwenye familia.

“Watu wengi wamekuwa hawaandiki wosia hivyo naomba wananchi kujitahidi kuandika wosia ili kuweza kuondoa changamoto kwenye familia,” amesema.

Kwa upande wao Chama cha Wanasheria  Tanganyika (TLS) wameiomba Serikali kutoa tamko kwa baadhi ya vyombo vya dola kuacha kuingilia majukumu ya TLS hali ambayo inakatisha tamaa ya utendaji kazi.

Akimwakilisha Rais wa TLS , Ipilinga Panya  amesema kuwa chama chao kipo kisheria ila baadhi ya vyombo vya dola vimekuwa na tabia ya kuingilia majukumu yao na kufanya wasifanye kazi kwa ufanisi.

“Tunaomba Serikali kutoa tamko kwa baadhi ya vyombo vya dola kukamata mawakili wakihisiwa wanaingilia majukumu yao,” amesema Panya.

Hata hivyo, baadhi ya wanachi wamesema kampeni hiyo itasaidia kuwaongezea uwelewa wa mambo ya kisheria na kujua namna ya kufanya wanapopata changamoto za kisheria.

“Kampeni hii itaenda kutuongezea uwelewa wa mambo ya kisheria na namna gani tunaweza  kupata msaada wa kisheria na kutuongezea uwelewa,” amesema Fatuma Ally.

Kwa upande wake, Rashidi Juma amesema wananchi wengi hawana uwelewa wa mambo ya kisheria, hivyo kampeni hiyo itasaidia  kuwaongezea uelewa hasa kwenye migogoro ya ardhi na miradi.

“Wananchi wengi hatuna uwelewa wa masuala ya kisheria ila ujio wa kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia itasaidia kutatua migogoro mingi  na kwa muda mfupi,” amesema Juma.