M23 yadaiwa kuwaua walinda amani 13 wa UN

Goma. Waasi wa kundi la M23 wanadaiwa kuwaua wanajeshi na walinda amani 13 wa Umoja wa Mataifa (UN) katika majibizano ya risasi yaliyotokea Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Shirika la Habari la Associated Press limeripoti jana, Januari 26, 2025 kuwa M23 walitekeleza mauaji hayo Jumamosi katika kile kinachotajwa kuwa uvamizi mpya wa miji iliyokuwa chini ya Serikali ya Rais Felix Tshisekedi.

Walinda amani hao waliuawa katika majibizano ya risasi yaliyotokea katika Mji wa Goma, wenye wakazi zaidi ya milioni mbili, katika juhudi za kuwazuia M23 kuingia na kuuzingira mji huo.

Kutokana na mauaji ya maofisa hao, Baraza la Amani la Umoja wa Mataifa liliitisha kikao cha dharura jana saa 4:00 asubuhi kujadili hali ya sintofahamu iliyoibuka nchini humo.

Serikali ya DRC nayo imeomba kikao na baraza hilo. Kikao hicho kimepangwa kufanyika leo, Jumatatu Januari 27, 2025, asubuhi.

Jumamosi, vikosi vya DRC na wazalendo vilitangaza kuwadhibiti wapiganaji wa M23 kuingia katikati ya Mji wa Goma kwa kushirikiana na maofisa na walinda amani wa Umoja wa Mataifa.

Vikosi hivyo vinaungwa mkono na majeshi kutoka Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SAMIDRC).

“Kundi la M23, linalofadhiliwa na Rwanda, ni wazi linalenga kuuhujumu uongozi mpya wa Marekani ulioingia madarakani kwa kuusogelea Mji wa Goma na kuhatarisha maisha ya raia zaidi ya milioni mbili wa Goma,” amesema Kate Hixon, Mratibu wa Shughuli za Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Amnesty International nchini Marekani.

DRC, Umoja wa Mataifa na Marekani zimekuwa zikiishutumu Rwanda kwa kuwafadhili waasi hao, huku wengi wao wakitajwa kuwa ni Watutsi waliokimbilia DRC zaidi ya muongo mmoja uliopita.

Hata hivyo, Serikali ya Rwanda imekanusha madai ya kufadhili kundi hilo, ingawa ilithibitisha kuwepo kwa silaha zake Mashariki mwa DRC kwa kile ilichodai kuwa ni kuimarisha ulinzi wa mipaka yake.

Kwa mujibu wa wataalamu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya wanajeshi 4,000 wa Rwanda wako nchini DRC.

Kipande cha video kinachosambaa mitandaoni kinaonyesha gari jeupe la kijeshi la UN likiteketea katika moja ya barabara inayotoka Mji wa Sake kuelekea Goma.

Miongoni mwa walinda amani waliouawa ni walinda amani wawili wa Afrika Kusini waliouawa Ijumaa, huku mmoja kutoka Uruguay, aliyekuwa amevaa kofia ngumu yenye nembo ya UN, naye akiuawa Jumamosi.

Ofisa wa UN, aliyezungumza na Associated Press kwa sharti la kutotajwa jina, alisema walinda amani watatu kutoka Malawi ni miongoni mwa waliouawa katika majibizano hayo ya risasi.

Pia, walinda amani saba wa Afrika Kusini waliokuwa chini ya mwamvuli wa Jeshi la Kulinda Amani la Umoja wa Maendeleo wa nchi za Kusini mwa Afrika (SAMIDRC) waliuawa katika kipindi cha siku mbili zilizopita, jambo ambalo Idara ya Ulinzi ya Afrika Kusini ilithibitisha kupitia taarifa yake kwa umma.

Kwa mujibu wa Jeshi la Uruguay, askari wake aliyeuawa ni Rodolfo Álvarez, ambaye alikuwa miongoni mwa Kikosi cha Nne cha Uruguay nchini DRC. Jeshi hilo limesema kikosi chake kimekuwa kikifanya kazi kwa kufuata miongozo ya Umoja wa Mataifa na kusaidia kunusuru maisha ya raia.

“Tumekuwa tukifanya kila tuwezalo kuimarisha ulinzi wa wanajeshi wetu wanaofanya kazi kwenye mazingira magumu nchini DRC. Hata hivyo, baadhi ya walinda amani wetu wamejeruhiwa kwenye majibizano hayo,” imesema taarifa ya jeshi hilo.

Askari watatu wa Uruguay kati ya waliojeruhiwa wamebakia Goma, huku wanne wakipelekwa Uganda kwa matibabu.

Tangu mwaka 2021, vikosi mbalimbali vimekuwa vikishirikiana na Serikali ya DRC kupambana na waasi wa M23. Vikosi hivyo ni pamoja na SAMIDRC na walinda amani wa Umoja wa Mataifa, ambao wanapambana kuwarudisha nyuma waasi hao kuingia Mjini Goma.

Kikosi kingine cha kulinda amani kutoka Umoja wa Mataifa, Monusco, kilichoingia DRC zaidi ya miongo miwili iliyopita, kimefanikiwa kupeleka wanajeshi zaidi ya 14,000.

Waziri wa Ulinzi wa Afrika Kusini, Angie Motshekga, alitembelea kikosi cha walinda amani kutoka nchini mwake kilichopo DRC siku moja kabla ya mauaji hayo kutokea.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika.