M23 wanavyoacha vilio kwa wasafirishaji wa Tanzania

Mgogoro unaoendelea Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umezidi kuleta hasara katika maeneo mbalimbali. Wasafirishaji nchini Tanzania wanadai kuwa asilimia 80 ya malori yaliyokwama katika taifa hilo la Afrika Mashariki mizigo yake imeibwa lakini pia vipuri vimenyofolewa.

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tatoa), Elias Lukumay, katika mahojiano na Mwananchi, anaeleza kuwa bado malori hayo yapo huko kwa kuwa hali haijatulia hadi sasa, lakini cha kusikitisha yameibiwa mizigo yake pamoja na kung’olewa vifaa mbalimbali.

“Tunashukuru madereva wetu walitoka salama, lakini magari yaliyobaki asilimia 80 mizigo yake na vifaa viliibwa,” alisema Mwenyekiti huyo.

Hata hivyo, alisema malori ambayo hadi sasa yapo salama ni yale yaliyopo yadi, lakini yale yaliyokuwa barabarani mengi ndiyo hayo yameibiwa vitu mbalimbali.

Kuhusu athari ambazo wamezipata tangu kutokea kwa machafuko hayo, alisema ni kushindwa kufanya biashara katika eneo hilo la Goma na Bakavu ambako vita imeshamiri.

“Kutokana na hilo, hata Serikali inashindwa kupata mapato yake. Kwa mfano kama gari moja lilikuwa inaingiza Sh7 milioni likisafiri, ni wazi itakosa hela hiyo,” alisema.

Lukumay amependekeza kuwa Serikali ya Tanzania na ile ya DRC, ziangalie njia za kidiplomasia kuyarejesha magari hayo nchini hata kwa kuyasindikiza na ulinzi maalumu mpaka mpakani mwa Rwanda.

Amesema kwa kufanya hivyo kutawawezesha kufanya biashara na nchi nyingine zenye uhitaji, ukizingatia bandari ya Tanzania inategemewa na nchi zaidi ya saba katika kusafirisha bidhaa zake zinazotoka nje ya nchi.

Madereva waenda kuyachukua kisiri

Mwenyekiti Chama cha Wamiliki wa Malori Wadogo na wakati Tanzania (Tamstoa), Chuki Shabani, amesema kwa kuwa kuna baadhi mikopo walioichukua benki bado inaendelea kusoma, wana mpango wa kuziandikia benki husika barua ili wawasimamishie riba.

“Tangu malori hayo yamekwama nchini humo, ni wazi wamiliki hawafanyi kazi, lakini kule benki walipochukua mkopo ama kwa kununua gari magari au kufanyia biashara, inaendelea kusoma salio.

“Hii ni vita, hawakupenda kusimama kufanya kazi, hivyo tumeona tuwasaidie wanachama wetu ili wasiumie zaidi na tayari tumewatangazia wafike ofisini kwa ajili ya hilo, kwa kuwa kila mmoja anajua namna anavyoifanya biashara hiyo na isitoshe wamekopa katika benki na taasisi mbalimbali,” alisema Shabani.

Kuhusu magari, alisema bado wanasubiri tamko la Serikali kama kumeshakuwa salama ili kwenda kuyachukua, japokuwa alisema wana taarifa baadhi ya wamiliki kuwatuma madereva kwenda kuyachukua kwa siri, jambo ambalo ni hatari kwa usalama wao.

“Tunaomba wamiliki wanaowatuma madereva wao kwenda kuyachukua magari hayo kinyemela waache mara moja, kwa kuwa wanahatarisha maisha yao, Serikali ilitumia gharama kuwaokoa na kuwarejesha nyumbani.

“Hapa naomba nisisitize tena kuwa mali zinatafutwa, lakini siyo uhai wa watu, hivyo tusubiri maelekezo ya Serikali katika hili na siyo kuwatoa kafara Watanzania wenzetu,” alisema Chuki.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Malori Tanzania (Chawamata), Nuhu Mgodoka, alisema suala la madereva kuambiwa waende kuchukua magari kisiri nchini humo bado hawajapata malalamiko yake hadi sasa na kueleza kama lipo hivyo siyo sawa.

Mmoja wa madereva ambaye hakutaka kutajwa jina lake, alisema yeye ni miongoni mwa waliokwenda kuchukua magari kinyemela na hiyo ni kwa sababu anaona atashindwa kuendesha maisha yake.

“Hatujui lini Serikali itasema magari hayo yakachukuliwe, na sisi ndio maisha yetu yalipo na wala matajiri wasisingiziwe katika hili na hata kama kuna wanaolazimisha madereva wao, basi ni wachache, lakini sisi madereva hali zetu kiuchumi ndio zinatusukuma kujitoa mhanga.

Dereva hiyo alieleza zaidi kuwa maisha yao hawategemei mshahara kwa kuwa hauwatoshi, isipokuwa kuwa barabarani ndiko kunawafanya waishi.

Mgogoro wenyewe

Mgogoro Mashariki mwa DR Congo ulianza tangu miaka ya 1990, lakini umekuwa ukiongezeka kwa kasi katika wiki za hivi karibuni. M23, kundi linalojumuisha waasi wa kabila la Watutsi, linasema linapigania haki za wachache, huku serikali ya DR Congo ikidai kuwa waasi hao wanaoungwa mkono na Rwanda wanajaribu kuchukua udhibiti wa utajiri mkubwa wa madini uliopo mashariki mwa nchi hiyo.

Mpaka sasa maelfu ya watu wameripotiwa kukimbia makazi yao, huku waasi wakitangaza kudhibiti miji kadhaa katika eneo hilo, huku mapigano kati ya vikosi vya Serikali na M23 yakiendelea maeneo mengine.

Tayari juhudi mbalimbali zinaendelea ili kusitisha vita hiyo, ikiwemo mkutano wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika Februari 8, 2025 jijini Dar es Salaam.

Pamoja na mambo mengine, iliamuliwa kikosi cha M23 na serikali ya DRC kukaa mezani kufanya mazungumzo, lakini hilo linaonekana kugonga mwamba kwani Ijumaa Februari 14, kikosi hicho kimeuteka Mji wa Bukavu na kuthibitishwa na kiongozi wake, Corneille Nangaa kupitia Shirika la Habari la Reuters.