Waasi wa M23 wamerejesha mashambulizi yao Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), baada ya kukaa kimya siku mbili zilizopita.
Al Jazeera, imeripoti leo Jumatano Februari 12, 2025, kuwa waasi hao jana (Jumanne) wamevamia na kukiteka Kijiji cha Ihusi kilichopo takriban kilometa 40 kutoka ulipo uwanja wa ndege wa Kavumu ulioko kilometa 70 kutoka mji wa Bukavu ambao ni makao makuu ya Jimbo la Kivu Kusini.
Kundi la M23 ambao linajinasibu kulinda masilahi ya watu jamii ya Watutsi, walianza uvamizi wao Jimbo la Kivu Kusini baada ya kuteka sehemu kubwa ya Jimbo la Kivu Kaskazini ukiwemo Mji wa Goma.
Mapigano ya kuuteka Mji wa Goma ambao ni makao makuu ya Jimbo la Kivu Kaskazini Mashariki mwa DRC yalisababisha vifo vya watu zaidi ya 3,000 huku maelfu wakijeruhiwa.
Bukavu ni Mji ambao hofu inazidi kutanda miongoni mwa raia na wakazi wa eneo hilo baada ya waasi hao kutengua ahadi ya kuendelea na mapigano wiki iliyoisha, walipouteka Mji wa Nyabibwe jambo lililosababisha baadhi ya shughuli kusimama ikiwemo shule kufungwa.
Mwandishi wa Al Jazeera, Malcolm Webb, akiripoti kutokea jijini Nairobi nchini Kenya, amesema wakazi wa Bukavu wanasubiria kuona iwapo wapiganaji wa M23 watafanikiwa kupambana na vikosi vya Jeshi la Ulinzi la DRC (FARDC) na kuuteka mji huo.

Tayari inadaiwa watu wameanza kuyakimbia makazi yao, wengine wanakimbilia kwenye kambi za wakimbizi zilizoko kaskazini mwa Mji wa Goma baada ya waasi hao kuanza kuonekana katika baadhi ya maeneo ya Jimbo la Kivu Kusini.
M23 ilitoa taarifa kwa umma Jumatatu ikikanusha kuwafukuza wananchi waliokimbilia kwenye kambi za wakimbizi, huku likisema watu walikuwa wakiondoka kwa hiari yao katika kambi ya Bulengo na kurejea katika kile ilichodai ni makazi yao baada ya Amani kurejeshwa na waasi hao.
“Baadhi yao wanaonekana wakifungasha mizigo kuondoka kutafuta maeneo yenye utulivu. Wengine wanasema watakaa huko mpaka kieleweke ama watakapolazimishwa kuyaachia makazi yao kutokana na vita hiyo,” amesema mwandishi huyo.
Jumamosi viongozi, 24 kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) walikutana jijini Dar es Salaam, Tanzania na kuazimia kwa kuwataka wakuu wa majeshi kwa kila nchi wanachama kujifungia na kuja na mkakati wa kumaliza mzozo huo.
Viongozi hao walikutana kwa dharura jijini Dar es Salaam, baada ya kuhofia kile kinachotajwa ni hatari ya mapigano hayo kugeuka kuwa vita ya Kikanda.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, machafuko hayo yamesababisha watu zaidi ya milioni 6.7 kuyakimbia makazi yao ndani ya taifa hilo, wengi wao wakikimbia Jimbo la Kivu Kaskazini kwenda Kivu Kusini kukwepa mapigano.
Mapigano ya hivi karibuni mjini Goma, kati ya M23 dhidi ya FARDC, yamesababisha watu zaidi ya 500,000 kuyakimbia makazi yao mwaka huu jambo lililosababisha uwiano usiyo sawa wa rasilimali ikiwemo chakula jambo lililosababisha janga la kibinadamu mashariki mwa nchi hiyo.
Bruno Lemarquis, ambaye ni ofisa wa juu wa UN nchini DRC, amesema mapigano hayo yameathiri utoaji wa huduma za kibinadamu kwa waathiriwa wa vita hiyo huku akitaja uamuzi wa Rais Donald Trump, kusitisha misaada kupitia Shirika la Kimataifa la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) kuwa nayo imeathiri.
Trump aliagiza kusitishwa kwa utoaji wa misaada na ufadhiri wa Shirika la Marekani la Misaada ya Kimataifa (USAID) kwa siku 90 ili kupisha tathmini ya kina ya utendaji wa Shirika hilo, uamuzi huo aliutangaza saa chache baada ya kuapishwa na kuanza majukumu yake kama Rais wa taifa hilo.
“Kusitishwa kwa shughuli za ufadhiri kunamaanisha kusimamishwa kwa programu za dharura ikiwemo makazi na malazi yaliyokuwa yakitolewa kwa wakimbizi ambao ni waathiriwa wa vita inayoendelea nchini DRC,” amesema Lemarquis.
Rwanda yakomalia msimamo
Pamoja na Serikali ya Rais Felix Tshisekedi kuendelea kuishutumu Rwanda kuwafadhili waasi hao wa M23, ambapo mapigano dhidi ya FARDC yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 3,000, taifa hilo limeendelea kukanusha kuwa halihusiki na shughuli zinazoendeshwa na waasi nchini DRC.
DRC imekuwa ikiishutumu Rwanda kuwafadhiri waasi hao kwa masilahi ya kujipatia rasilimali ikiwemo Madini, Rwanda kupitia Balozi wake UN, James Ng’anzi imekazia kwenye kanusho la Rais Paul Kagame kuwa haihusiki.
“Tunapingana vikali na kitendo cha Serikali ya DRC kujaribu kutuchafua kuwa tunahusika kufadhiri machafuko yanayoendelea Mashariki mwa DRC. Hatuhusiki na hilo,” alisema Ngango, alipohutubia Mkutano wa Dharura wa Baraza la Haki za Binadamu la UN.
“Jambo hili liko wazi, Ila kwa sababu ya tishio la waasi kuwepo DRC mtu pekee wa kurushiwa lawama ni Rwanda. Baada ya Mji wa Goma kuangukia mikononi mwa waasi, mashambulizi mfululizo pia yameanza kuilenga Rwanda,” amesema Balozi huyo huku akiituhumu DRC kwa kumwaga silaha kuzunguka uwanja wa Goma.
Shambulizi la Codeco
Wakati M23, wakiendelea kujitanua kuelekea Jimbo la Kivu Kusini, Waasi wa Kundi la Codeco nao wameibuka na kushambulia vijiji vya Djaiba Jimbo la Ituri Mashariki wa DRC na kuua watu zaidi ya 55.

Jean Vianney, ambaye ni kiongozi wa vijiji hivyo, alisema mashambulizi ya kundi hilo dhidi ya raia yalianza Jumatatu saa 2 asubuhi ambapo watu wengi waliuawa kwa kupigwa risasi, kukatwa mapanga na kuchomwa moto wakiwa ndani ya nyumba zao.
Miongoni mwa wanaohofiwa kuuawa katika shambulizi hilo la Codeco ni pamoja na watoto huku waasi hao wakishikilia sehemu kubwa ya migodi iliyopo Ituri hususan ya Dhahabu.
UN imekuwa ikiishutumu Codeco kwa kutekeleza mashambulizi katika jamii hususan kwenye jamii za kabila la Wahema, na kutekeleza uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu. Eneo kubwa la Mji wa Djigui Jimbo la Ituri unakaliwa na watu wa Kabila la Wahema.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.