
Umbali kutoka Bukavu mpaka Goma, kwa barabara ni kilometa 193.9. Ni miji mwili, mmoja upo ncha ya Kusini ya Ziwa Kivu na mwingine ncha ya Kaskazini. Bukavu ni Kusini na Goma Kaskazini. Miji hiyo inapakana na Rwanda.
Goma ni mji mkuu wa Jimbo la Kivu Kaskazini, wakati Bukavu ipo Jimbo la Kivu Kusini. Miji hiyo miwili ni mada kuu ya machafuko ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Tayari Goma ipo kwenye himaya ya Muungano wa Mto Congo. Na sasa wanakwenda Bukavu.
M23, kifupi cha March 23, kwa kirefu March 23 Movement (Vuguvugu la Machi 23), pia hujitambulisha kama Congolese Revolutionary Army (Jeshi la Mapinduzi la Congo), lakini ulimwengu unawatambua kuwa ni kikundi cha waasi. Hata hivyo, wananchi wa Goma wanawapa uhalali.
Kikundi cha M23 ni mwanachama na mhusika mkuu wa Muungano wa Mto Congo, ambao ndiyo unaendeleza mapambano dhidi ya Serikali ya DRC.
Lengo mama ni kufanya mapinduzi na kuiondoa madarakani Serikali inayoongozwa na Rais Felix Tshisekedi.
Februari 6, 2025, menejimenti Muungano wa Mto Congo, ilifanya mkutano mkubwa wa hadhara, uliofanyika kwenye Uwanja wa Unity. Kubwa kuhusu mkutano huo si barabara zote za kuelekea uwanjani zilivyofungwa, bali maelfu ya wananchi wa Goma walivyojitokeza.
Wakazi wa Goma, wakiwa na bashasha, walihudhuria mkutano huo wa Muungano wa Mto Congo.
Picha ilijengwa dhahiri kuwa wapiganaji hao ambao hutafsiriwa kama magaidi, wana uhalali mkubwa miongoni mwa jamii za Goma na Mashariki ya DRC kwa jumla.
Katika mkutano huo, Muungano wa Mto Congo ulitangaza viongozi watakaiongoza Goma, chini ya mamlaka yao.
Ni kipindi ambacho Serikali ya DRC, ilimsimika Meja Jenerali Somo Kakule Evariste kuwa Gavana mpya wa Kivu Kaskazini, baada ya aliyekuwepo, Meja Jenerali Peter Cirimwami, kuuawa na M23, Januari 31, 2025.
Siku nne kabla ya mkutano kwenye uwanja wa Unity, Kiongozi wa Muungano wa Mto Congo, Corneille Nangaa, akiongozana na Rais wa M23, Bertrand Bisimwa, walizuru mitaa ya Goma na kufanya usafi. Wananchi waliwashangilia muda wote kupitia tukio hilo.
Ni wiki moja imepita tangu washirika wa Muungano wa Mto Congo, waudhibiti na kuushikilia mji wa Goma.
Maelfu ya wananchi waliokuwa wakiwashangilia viongozi hao, wanajenga sura ya mshangao kwa jumuiya za kimataifa, maana ndugu zao wengi wamepoteza maisha, hali inazidi kuwa mbaya.
Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, Vivian Van De Perre, amesema hadi Alhamisi (Februari 6), idadi ya vifo ni watu zaidi ya 3,000, na baadhi ya maeneo, ukipita mtaani maiti zimetapakaa, zimeoza na zinatoa harufu.
Hali ikiwa hivyo, Muungano wa Mto Congo, unasonga mbele, tayari wameshautwaa mji wa Nyabibwe, umbali wa kilometa 70 kutoka Bukavu.
Wasiwasi ni kwamba wakati wowote wataikamata Bukavu. Maana yake, majimbo yote ya Mashariki ya Congo, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, yatakuwa chini ya waasi.
Kiini cha machafuko
Zipo sababu za kihistoria na kuna mpya. M23 wanasimama upande wa kihistoria, wakati kiongozi wa Muungano wa Mto Congo, yeye ana ajenda ya kumng’oa madarakani Tshekedi. Muungano huo wa masilahi ndiyo sababu ya machafuko yaliyopo.
M23 ni kikundi kilichoasisiwa na kupewa jina la M23, lengo likiwa kupigania maazimio ya amani, yaliyopatikana Machi 23, 2009, chini ya wasuluhishi, Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa na Rais mstaafu wa Nigeria, Olesugun Obasanjo.
Kihistoria, M23 ni matokeo ya kikundi cha CNDP, ambacho itikadi yake ilikuwa kupigania haki za Watusi waliopo DRC. Ni sehemu ya masilahi ya jamii ya Banyamulenge, waliopigana vita pamoja na Laurent Kabila kumwondoa Mobutu Sese Seko, katika Vita ya Kwanza ya Congo.
Chini ya aliyekuwa kiongozi wake, Laurent Nkunda, CNDP, mnyororo wake upo pia kwenye Vita vya Pili vya Congo, kipindi ambacho jamii ya Watusi, Mashariki ya DRC, walipoamka kumkabili Laurent Kabila, baada ya kuwageuka.
Watutsi hao wa DRC, walimsaidia hata Mobutu, lakini aliwageuka.
Serikali ya DRC chini ya Joseph Kabila na CNDP kwa upande wa pili, walisaini makubaliano ya amani, Machi 23, 2009. Makubaliano hayo yaliipitisha CNDP kuwa chama rasmi cha siasa DRC, halafu wapiganaji wake wakatakiwa kujiunga na jeshi la nchi hiyo.
Kingine kilichosainiwa ni kurejeshwa kwa uhusiano wa kidiplomasia baina ya Rwanda na DRC. Maana, nyuma ya CNDP, ilionekana kuna mkono wa Rwanda. Ikasainiwa pia kwamba Rwanda na DRC zibadilishane mabalozi.
Wapiganaji wa CNDP waligoma kujiunga na jeshi la DRC, matokeo yake wakaanzisha kikundi chao cha kupigania utekelezwaji wa makubaliano ya Machi 23, 2009, wakajiita M23, yaani Machi 23.
Mwaka 2012, M23 walifanikiwa kuudhibiti mji wa Goma. Hata hivyo, vikosi vya kulinda amani, vikiongozwa na majeshi ya Tanzania na Afrika Kusini, viliwafurusha M23 Goma.
Pamoja na hivyo, M23 wameendelea kujipanga na kusumbua Mashariki ya DRC, hasa Kivu Kaskazini.
Corneille Nangaa
Kuanzia mwaka 2015 mpaka 2021, Corneille Nangaa, alikuwa Mkurugenzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi DRC (Ceni). Nangaa, alikuwa kiongozi wa Ceni wakati wa Uchaguzi Mkuu DRC 2018, ambao Tshisekedi alishinda kiti katikati ya mauzauza ya kisiasa.
Tshisekedi, hakuwa kwenye mazingira ya kushika japo nafasi ya pili. Mchuano mkali ulikuwa baina ya Emmanuel Shadary, aliyekuwa na tiketi ya chama kilichokuwa madarakani, PPRD na muungano wa FCC, dhidi ya Martin Fayulu, aliyegombea kupitia ushirika wa Lamuka.
Mshangao wa dunia, Tshisekedi ndiye aliyetangazwa mshindi, nafasi ya pili akawa Fayulu na Shadary wa tatu. Kisha, ikaundwa Serikali ya mkataba baina ya Tshisekedi na kilichokuwa chama tawala, PPRD cha Kabila. Ilionekana dhahiri kwamba ushindi wa Tshisekedi ulikuwa mpango.
Ndoa ya Tshisekedi na Kabila ilivunjika. Halafu, kwa kile kilichotafsiriwa ni kupishana na Tshisekedi kupitia makubaliano yao wakati wa uchaguzi mwaka 2018. Februari 2023, Nangaa aliasisi chama kipya cha siasa, kinachoitwa ADCP (Hatua kwa ajili ya Utu wa Congo na Watu Wake).
Nangaa, alijipanga kushiriki Uchaguzi Mkuu DRC 2023 katika ngazi zote. Hata hivyo, Nangaa alikumbana na mashitaka ya umma, akituhumiwa kucheza mchezo mchafu wa kura kwenye Uchaguzi Mkuu 2018. Nangaa alikimbia nchi akidai usalama wake haukuwa wa uhakika nchini DRC.
Desemba 15, 2023, Nairobi, Kenya, Nangaa alisaini mkataba na M23. Makubaliano ya Nangaa na M23 ndiyo yaliyozaa Muungano wa Mto Congo, ambao unaongozwa na Nangaa. M23 wanaita Muungano wa Mto Congo jukwaa la amani, wakati Serikali ya DRC inawaita magaidi.
Tshisekedi anamtuhumu Joseph Kabila kuwa nyuma ya Muungano wa Mto Congo. Agosti 8, 2024, Mahakama ya Kijeshi DRC, ilimhukumu kifo Nangaa, akiwa hayupo mahakamani, kwa makosa ya uhalifu wa kivita, uasi dhidi ya mamlaka na uhaini.
Mbali na Goma na Nyabibwe, Muungano wa Mto Congo, kupitia mwanachama wake, M23, wanaushikilia pia mji wa Sake, uliopo Kivu Kaskazini, ambao upo umbali wa kilometa 25 kutoka Goma.
Nangaa anasema shabaha yao si Goma wala Bukavu, bali ni kufika Kinshasa na kumwondoa madarakani Tshisekedi.
Dhahiri, M23 wamepata ushirika wa wanasiasa wanaotaka mapinduzi, hivyo ni vita ya kimasilahi. Nangaa na madaraka, M23 na haki za Watutsi wa DRC, huku macho na masikio yakisubiri matokeo ya kikao cha wakuu wan chi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) hapo kesho.