Lyimo achaguliwa mwenyekiti TLP,  21 wafutwa uanachama, wamkataa

Dar es Salaam. Wajumbe 84 wa mkutano mkuu wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), wamemchagua, Richard Lyimo kuwa Mwenyekiti wa chama hicho kwa miaka mitano ijayo.

Lyimo aliyekuwa Katibu Mkuu wa TLP anashika nafasi hiyo ambayo kwa muda mrefu, Hamad Mkadamu alikuwa anakaimu baada ya Augustino Mrema kufariki duniani Agosti 21, 2022.

Mkutano huo uliofanyika leo Jumapili, Februari 2, 2025 jijini Dar es Salaam ulihudhuriwa pia na Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza.

Kwenye kuchagua viongozi nafasi ya mwenyekiti haikuwa na upinzani kwani Lyimo alikuwa mgombea pekee aliyechukua fomu, hivyo hata kuchaguliwa kwake hakupigiwa kura bali ilitumika demokrasi ya kunyoosha mikono.

Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TLP Taifa

Pia katika mkutano huo, Johari Hamis amechaguliwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tanzania Bara, bila upinzani baada ya kukosa mshindani.

Katiba ya chama hicho toleo la mwaka 2009 inaruhusu iwapo mgombea wa nafasi hiyo atakosa washindani, atachaguliwa kwa kunyoosha mikono wanaomkubali na kumkataa na upande watakaokuwa wengi atakuwa ameshinda.

Mkutano huo kwa kauli moja uliridhia kuwafuta uwanachama wanachama 21 wa chama hicho, wakiwemo viongozi waliofanya majaribio ya kuandaa mikutano miwili ya kuchaguana ili kuziba nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa mwenyekiti, marehemu Mrema kinyume na katiba ya chama hicho.

Viongozi hao ni pamoja na Dominata Rwechangura aliyekuwa makamu mwenyekiti wa chama hicho, Ivan Maganza aliyekuwa mwenyekiti wa vijana wa chama hicho taifa.

Wengine waliofukuzwa Mariam Kassim, Riziki Nganga, Stanley Ndumagoba, Mary Mwaipopo, Mohamed Mwinyi, Laurian Kazimiri, Nataria Shirima, Kinanzaro Mwanga, Godfrey Stivin na Rashid Amiri.

Wengine ni Twaha Hassan, Tunu Kizigo, Damari Richard, Hamad Alawi, Mohamed Hemed, Mariam Hamis , Mussa Fundi, Mwajuma Mussa na Osward Nyoni.

Hata hivyo, Mwananchi imezungumza na Maganza baada ya kuvuliwa uanachama, ambapo amesema mkutano huo hautambui na uamuzi uliofanyika ni batili.

“Mkutano huo ni batili, mbona wengine hatuna taarifa yeyote, kisheria ulitakiwa kutangazwa siku 28 kabla ya kufanyika, wengine hatuna taarifa na maamuzi hayo siyatambui nitafuatilia kudai haki yangu,” amesema Maganza

Naye Damari Richard, amesema mkutano huo wamevunja sheria kwani wao kama viongozi hawajapata taarifa.

Richard Lyimo akishangilia ushindi wake pamoja na wanachama wa TLP

“Mgombea yeyote lazima apitishwe na halmashauri kuu, sasa Lyimo na wenzake wamepitishwa na halmashauri gani kama sisi wajumbe halali hatujui kinachoendelea,”amesema

Alipoulizwa Naibu Msajili Nyahoza, amesema mkutano huo ni halali na aliyeuitisha  anatambuliwa na katiba na taratibu za chama chao na walishatoa taarifa, hivyo yote yaliyofanyika ni halali na yana baraka kutoka kwa wajumbe.

“Kama kuna malalamiko ya watu kutimuliwa uanachama nikiletewa kwa kufuata utaratibu nitayashughulikia lakini kwa sasa wamezingatia vigezo vyote,” amesema

Uchaguzi huo bado unaendelea kwa nafasi ya makamu mwenyekiti Zanzibar ambapo kuna wagombea wawili, akiwamo aliyekuwa anakaimu nafasi ya mwenyekiti taifa, Mkadam na Mgao Kombo Mgao.