
BEKI wa Azam FC, Lusajo Mwaikenda amevunja rekodi ya msimu uliopita ya mabeki waliofunga mabao mengi zaidi katika Ligi Kuu, baada ya nyota huyo kufunga moja na kufikisha matano katika ushindi wa kikosi hicho wa 4-2, dhidi ya Kagera Sugar.
Lusajo alifunga bao hilo dakika ya 42, akiunganisha kwa kichwa kona iliyopigwa na Abdul Suleiman ‘Sopu’ na kuisawazishia Azam baada ya Hijjah Shamte kuitanguliza Kagera dakika 26, kisha Idd Seleman ‘Nado’ kupachika la pili dakika ya 58.
Kagera ilijibu mapigo na kusawazisha dakika ya 60 kupitia kwa Kassim Fekha, huku Nassoro Kapama akijifunga dakika ya 82 katika harakati za kuokoa mpira wa Lusajo na kuipa Azam bao la tatu, kabla ya Mcolombia Jhonier Blanco kufunga bao moja kali la nne katika dakika ya 87 ya mchezo.
Kitendo cha Lusajo kufunga bao moja kimemfanya kufikisha mabao matano ya Ligi Kuu msimu huu na kuivunja rekodi ya msimu uliopita, ambapo beki aliyekuwa na mabao mengi zaidi alikuwa ni Derrick Mukombozi wa Namungo FC aliyefunga manne.
Mbali na Mukombozi, mwingine aliyefunga mabao mengi zaidi msimu uliopita ni Nicholas Gyan anayemudu kucheza namba mbili na wakati mwingine akicheza kama winga wa kulia akiichezea Singida Fountain Gate aliyemaliza msimu pia na mabao manne.
Msimu huu mbali na Lusajo, mabeki wengine wenye mabao mengi ni Ibrahim Hamad ‘Bacca’ wa Yanga mwenye manne, Shomari Kapombe (Simba), Erasto Nyoni (Namungo FC), Pascal Msindo (Azam FC) na Hernest Malonga wa Singida Black Stars ambao kila mmoja amefunga mabao matatu.
Wengine wanaofuatia ni wenye mabao mawili ambao ni Wilson Nangu wa kikosi cha JKT Tanzania, Che Malone Fondoh (Simba), Yoro Diaby (Azam FC), Heritier Lulihoshi (Dodoma Jiji) na Mkongomani Andy Bikoko anayeichezea timu ya Tabora United.
Akizungumzia kiwango chake msimu huu, Lusajo alisema licha ya ubora anaouonyesha wa kufunga ila ni hatari zaidi wakati akiwa anashambulia, kwa sababu ni muda ambao wapinzani huweza kutumia gepu lililopo na kuweza kuwaadhibu wasipojipanga.
“Suala la kufunga huwa linatokea kwa sababu nacheza na akili za wapinzani wetu na kuangalia ni muda gani naweza kutumia nafasi ya kushambulia bila ya timu kudhurika, ni jambo nzuri pia kwangu kwa sababu matunda yanaonekana,” alisema Lusajo.