Lundenga kuzikwa Jumatatu Morogoro, wadau wamlilia

Dar es Salaam. Waliowahi kushiriki mashindano ya Miss Tanzania, wamezungumzia kifo cha muasisi wa mashindano hayo, marehemu Hashim Lundenga.

Lundenga amefariki dunia leo Jumamosi Apili 19, 2025 katika Hospitali ya Kitengule iliyopo Tegeta jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu na atazikwa Jumatatu katika makaburi ya Kidatu, wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro.

Taarifa ya kifo chake hicho pia zimethibitishwa na Katibu wa Kamati ya Miss Tanzania, Bosco Majaliwa.

“Ndio Hashimu Lundenga amefariki kama masaa mawili yaliyopita katika Hospitali ya Itengule iliyopo Tegeta hapa.

“Hashimu ameumwa muda mrefu sana, nafikiri taarifa ya kuumwa kwakwe watu wengi wanayo, alipata ‘stroke’ muda mrefu sana, alilazwa kwenye Hospitali Muhimbili alitolewa, alilazwa Mlongazila akatolewa akawa anaendelea kupata kliniki lakini hali ikazidi kuwa mbaya zaidi,” amesema.

Ameongeza kuwa, “Kwa hiyo jana alizidiwa wakamleta hapa kwenye Hospitali ya Itengule lakini bahati mbaya amefariki dunia, msiba upo nyumbani kwake Bunju.”

Walichosema warembo

Baadhi ya waliowahi kuwa washiriki wa shindano la Miss Tanzania wamezungumzia msiba huo huku wakielezea namna gani walivyoweza kufanya kazi na Lundenga wakati wa uhai wake.

Mmoja wa warembo hao ni Miriam Odemba, ambaye amesema Lundenga licha ya kuwa mwandaaji wa mashindano hayo kwake alikuwa mjomba na baba.

Odemba ambaye alikuwa Miss Temeke mwaka 1997 amesema  kuwa Lundenga alikuwa mtu aliyekuwa na maono, mshauri mzuri na msimamizi mzuri kwa warembo nchini.

“Mimi nilifahamiana na Lundenga nikiwa na miaka sita ambapo ka mara ya kwanza nilikwenda jijini  Dar es Salaam na mama yangu  tukitokea Arusha,  nilikaa kwake kwa miezi sita.

“Wakati nikiwa kwake aliniambia kwa mwonekano wangu naweza kuja kuwa Miss Tanzania siku moja, kwani tangu nikiwa mdogo nilikuwa mrefu,”amesema Odemba na kuongeza;

“Baada ya hapo tulipoteana kwani nilirudi tena Arusha na alikuja kuniona kwenye mashindano ya Miss Temeke, ambapo waandaaji walinipata nikiwa kwenye kibanda cha simu.

“Alishangaa kuniona katika mashindano hayo, na hata baada ya kujua nimeshiriki hakuwa upande wangu badala yake aliacha haki itendeke na mwisho wa siku nikaibuka kuwa Miss Temeke na kupata tiketi ya moja kwa moja ya kushiriki Miss Tanzania,”amesema Odemba.

Aidha mrembo huyo ambaye kwa sasa anaishi nchini Uholanzi amesema baada ya kushinda taji hilo ilimfungulia milango mingi ikiwemo ushiriki mashindano ya M-Net Face of Africa 1998 na sasa ni mmoja wa wanamitindo wakubwa wanaoiwakilisha vema Tanzania nje ya nchi.

Kutokana na mchango wake kwenye tasnia ya urembo, Lundenga, Odemba ameshauri aandikiwe kitabu chenye historia ya kupambania mashindano hayo kwa kuwa ni kati ya watu walioacha alama kwenye nchi hii.

Kwa upande wake Basila Mwanukuzi (Miss Tanzania 1998), amesema hadi leo kuwa mwandaaji wa Miss Tanzania anajivunia Lundenga.

Basila kupitia kampuni yake ya The Look alikabidhiwa na serikali kuandaa mashindano hayo kuanzia mwaka 2018.

“Mimi kwangu Lundenga ni ‘Uncle’ na ninaheshimu mchango wake kwangu hadi serikali kuniamini niwe muandaaji wa mashindano haya,”amesema.

Basili ambaye pia amewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, amesema hata wakati anakabidhiwa kuandaa mashindano hayo, neno analokumbuka kutoka kwa Lundenga ni kuwa anamuamini ataweza .

“Nakumbuka aliniambia haya mashindano mimi ningeweza hata kuwakabidhi watoto wangu hati miliki yake, lakini naona wewe unafaa na utaweza kuyasimamia na kunikabidhi rasmi kwa baraka zote”amesema Basila.

Naye Jokate Mwegelo amesema “Tutamkumbuka kama mdau aliyekuwa mstari wa mbele katoka kuibua vipaji vya wasichana hususani kwenye tasnia ya urembo na wengi kupitia jukwaa hilo wamejulikana na kujipata

Jokate amesema,”Nakumbuka alikuja nyumbani kuwaomba wazazi wangu nishiriki shindano la Miss Tanzania, mama yangu alikuwa hataki na Lundenga na wenzake walipokuja, walifukuzwa, lakini kwa ushawishi wake mwisho wa siku aliwakubalia,”amesema Jokate.

Jokate alikuwa mshindi wa pili katika shindano la Miss Tanzania 2006 ambapo mshindi alikuwa Wema Sepetu.

Alisema kuwa mashindano ya urembo yalimpa umaarufu mkubwa na kufanikiwa kupata teuzi mbalimbali ikiwemo Mwenyekiti wa Chipukizi wa Chama Cha Mapinduzi, Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe na baadaye Mkuu wa Wilaya ya Temeke.

Kwa sasa Jokate ni Katibu Mkuu wa wa Umoja wa Vijana CCM (UVCCM).

Neno la Mwenyekiti wa Kamati Miss Tanzania

Aliyekuwa, Mwenyekiti wa Kamati ya Miss Tanzania, Prashant Patel, amesema kuwa Lundenga hakuwa na fikra za kibiashara zaidi kuandaa mashindano haya bali aliyapenda moyoni mwake.

‘Ndio maana pamoja na kamati kuwa na watu wengi, lakini ulipotaja Miss Tanzania watu walimjua zaidi Lundenga kwa kuwa ndio alikuwa kabeba sura yake, aliyapenda sana mashindano hayo,”amesema.

Patel amesema alijuana na Lundenga akiwa katika masuala ya michezo na hata alipompelekea wazo la kushirikiana naye katika kuendesha hakusita kumuunga mkono.

Mkurugenzi huyo wa zamani wa hoteli ya White Sands, amesema jambo la kumuenzi Lundenga ni kuhakikisha mashindano hayo yanaendelezwa ili kufikia ndoto zake na kueleza milango ipo wazi kwa watakaohitaji ushauri wa kimawazo kwao.

Walichosema waandaaji wa kanda na vitondoji

Baadhi ya waliowahi kuandaa mashindano hayo ngazi ya Wilaya na vitongoji, wamesema Lundenga alikiwa mtu mvumilivu na msikivu kwa kila mtu.

Aliyekuwa muandaaji wa Kanda ya Ilala, Jackson Kalikumtima amesema waandaaji walikuwa wakipewa shutuma nyingi ikiwemo kufanya upendeleo kwa washindi, lakini hilo halikumkatisha tamaa Lundenga katika kazi yake.

 “Lundenga alikuwa rafiki wa kila mtu, mvumilivu wa kila jambo alilozushiwa na ndio maana aliweza kufanya kazi muda mrefu na wasichana pamoja na kuzushiwa mambo mbalimbali ambayo hayakumkatisha tamaa,”amesema.

Aidha Kalikumtima amesema nchi imepoteza mtu muhimu ambaye aliweza kubadili maisha ya wasichana wengi baadhi kuaminiwa na mamlaka na kuteuliwa na wengine kupata ajira na wengine hata kupata waume wenye hadhi kubwa serikalini.

Aidha amesema kupitia mashindano hayo wapo wasichana waliomiliki magari ya thamani na wengine kupewa nyumba kupitia zawadi mbalimbali za washindi zilizokuwa zikitolewa na wadhamini.

Amesema maono yake ilikuwa siku moja Tanzania itoe mshindi wa Miss World, huku akibainisha hata kufanikiwa kutoa Miss Afrika (Nancy Sumari) mwaka 2005.

Amesema kuwa ushindi wa Nancy ulikuwa ni hatua nzuri ambayo historia yake hadi leo haijafikiwa.

Aliwataja kati ya warembo wa Kanda ya Ilala ambao pia washindi taji la Miss Tanzania kuwa ni Hoyce Temu (balozi wa Tanzania Umoja wa Mataifa), Mbiki Msumi(Mhadhiri Chuo Kikuu Huria), Jacqueline Mengi na Angela Damas.

Naye Mahmoud Zubeiry aliyekuwa akiandaa Miss Mzizima, amesema Lundenga alikuwa rafiki wa waandishi wa habari na kwa kupitia mashindano hayo aliwafungulia fursa kwa kuwapa nafasi ya kuwa waandaaji.

 “Mimi nakumbuka kupitia mashindano ya Miss Tanzania niliweza kununua kiwanja changu cha kwanza nikiwa kwenye tasnia ya uandishi, hivyo mafanikio haya huwezi kuyataja bila kumtaja Lundenga,’amesema Zubeiry.

Somoe Ng’itu muandaaji wa mashindano ya Miss Chang’ombe, amesema Miss Tanzania ilikuwa ni mtoko wa watu wengi kipindi hicho na ilikuwa ikfuatiliwa na watu wake kwa waume hata kushinda mpira wa simba na Yanga, yote hii ikiwa ni juhudi za Lundenga.

Amesema kupitia mashindano hayo watu walifanya biashara ikiwemo wenye kumbi, vyakula, nguo na wabunifu mbalimbali wa mavazi nchini.

Kwa mara ya kwanza mashindano ya Miss Tanzania yalifanyika mwaka 1967 ambapo Theresia Shayo aliibuka mshindi.

Hata hivyo Mwalimu Nyerere akayapiga marufuku akidai yalikuwa yanaendeleza ukoloni mamboleo na yanatweza utu wa mwanamke.

Miaka 27 baadaye (1994), Rais wa wakati huo, hayati Ali Hassan Mwinyi aliyaruhusu na Lundenga kupewa kibali cha kuyaendesha kupitia kampuni yake ya White Sands na baadaye mwaka 1995 kupitia kampuni ya Lino International Agency ambapo  Aina Maeda aliibuka mshindi.

Na baada ya hapo aliendelea kuyasimama hadi pale mwaka 2017 serikali ilipomkabidhi Basila Mwanukuzi kuyaendesha.

Waliowahi kuwa Miss Tanzania chini ya Lundenga

Waliowahi kuwa Mamiss chini ya uongozi wa Hashim Lundenga ni  Emily Adolf (1995), Shose Sinare (1996), Saida Kessy (1997), Basilla Mwanukuzi (1998) na Hoyce Temu (1999).

Wengine ni Jacqueline Ntuyabaliwe(2000), Millen Magese (2001), Angela Damas (2002), Sylvia Bahame(2003), Faraja Kotta(2004), Nancy Sumari(2005), Wema Sepetu (2006) na Richa Adhia (2007).

Pia wapo  Nasreen Karim(2008), Miriam Gerald(2009), Genevieve Emmanuel(2010), Salha Israel(2011), Brigette Alfred (2012), Happiness Watimanywa(2013), Lilian Kamazima(2014), Diana Edward (2016)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *