Lundenga azikwa makaburi ya familia Kidatu Morogoro

Dar es Saaam. Mwili wa aliyekuwa mratibu wa mashindano ya Miss Tanzania, Hashim Lundenga, umezikwa leo Aprili 22,2025 katika makaburi ya familia, Kidatu, mkoani Morogoro. 

Mazishi ya Lundenga yamefanyika saa 6.00 mchana na kuhudhuriwa na wakazi wa maeneo ya Kidatu, Mkamba, Nyandeo na maeneo mengine ya jirani.

Mbali ya wakazi wa maeneo hayo, wadau wa masuala ya mashindano ya urembo kutoka Dar es Salaam na mikoa ya Pwani na Morogoro pia wameshiriki katika mazishi hayo.

“Tumezika salama na sasa tunarejea Dar es Salaam kuendelea na matanga,” amesema Yason Mashaka ambaye alikuwa mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Miss Tanzania enzi ya Lundenga.

Lundenga alifariki dunia Aprili 19, 2025 katika hospitali ya Kitengule iliyopo Tegeta jijini Dar es Salaam, alipokuwa akipatiwa matibabu ya homa ya mapafu.

Kwa mujibu wa mkewe aitwaye Twigy Hashim ameiambia Mwananchi kabla ya kufikwa na umauti mumewe alikata kauli kwa miezi minane.

“Ukweli ni muda mrefu alikuwa amekata kauli. Yapata miezi minane ila kabla ya miezi hiyo, alikuwa anasisitiza kwamba ikitokea umauti umemkuta akazikwe nyumbani. Lakini pia alikuwa anasisitiza kwamba tuwaangalie watoto wetu ili wawe na maadili mema.

Hata hivyo mama huyo ambaye ameishi maisha ya ndoa na Hashim kwa miaka 45 amesema mumewe ameugua kwa miaka minne.

“Aliugua mwaka mmoja akalazwa bila kuinuka. Miaka mingine mitatu alikuwa anaumwa huku anatembea kidogokidogo ukijumlisha inakuwa miaka minne ya kuugua kwake,”amesema

Mbali na mjane huyo. Mtoto wa marehemu aitwaye Harris Lundenga amesema baba yake alianza tena kuzidiwa Jumatano Aprili 16,2025.

“Jumatano alizidiwa tulimpeleka katika Hospitali ya Kitengule akalazwa na kuruhusiwa Ijumaa. Lakini bahati mbaya tulivyoamka naye asubuhi akazidiwa tukamrudisha tena hospitalini. Baada ya kufika hospitali ndio mauti ikamfika,”amesema Harris.

Akitoa salamu za pole Mkurugenzi wa Kampuni ya Look inayoendesha mashindano ya kumsaka Miss Tanzania, Basila Mwanukuzi amesema tasnia ya urembo nchini imepoteza nguzo muhimu kwani Hashim Lundenga alikuwa mtu aliyechonga njia ya mafanikio kwa mabinti wa Kitanzania.

“Kwa kweli tumepata msiba mkubwa, tumepoteza nguzo ya tasnia ya urembo, Anko Hashim ndio mlezi na muasisi wetu, mimi mwenyewe nilipitia jukwaa la Miss Tanzania kutambulika kwa jamii. Leo imefika hatua hata mabinti kutoka vyuo wanashiriki kwenye mashindano haya,” amesema Basila.

Naye Mshindi wa pili katika mashindano ya Miss Tanzania mwaka 1994, Lucy Tabasamu, amesema marehemu Hashim Lundenga ameacha alama kubwa ambayo haifutiki katika tasnia ya urembo nchini na kwamba alikuwa Anko kweli.

“Tutamkumbuka Lundenga kwa haya aliyoyaanzisha, ameacha alama kubwa ambayo haitaweza kufutika. Lundenga alikuwa ni Anko kweli, kwani alibeba mashindano haya kutoka kwenye taswira ya uhuni na kuyaheshimisha,” amesema Lucy.

Aidha kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Dk Kedmond Mapana amesema marehemu Hashim Lundenga, kupitia shindano la urembo la Miss Tanzania alitengeneza jukwaa la mafanikio kwa wanawake wengi nchini ambapo baadhi yao wameteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali.

“Kwa hiyo unaangalia namna gani jukwaa hili lilikuwa kubwa, lakini wote ni mashahidi kwamba warembo wote waliopitia katika jukwaa hili la Miss Tanzania wakati ule wa Hashim Lundenga wamekuwa ni watu waliopewa nafasi kubwa sana na Serikali, tumeona kuna wakuu wa wilaya wengi wameteuliwa, tumeona hata mabalozi wmeteuliwa, tumeona wamepata nafasi nyingine na wengine wameingia kwenye Sanaa, kwa hiyo sisi Basata tumepoteza mtu mahumu sana,” amesema Dk Mapana.

Ikumbukwe mwili wa Lundenga ulisafirishwa jana Aprili 21, 2025 kutoka jijini Dar es Salaam kwenda Kidatu ambako ndiko mazishi yake yamefanyika.

Lundenga alikuwa mratibu wa mashindano ya Miss Tanzania tangu mwaka 1994 hadi 2018 na kisha baadaye kumuachia Basilla Mwanukuzi ambaye anaratibu mashindano hayo hadi sasa. Pia amewahi kuhudumu katika kamati ya Klabu ya Yanga

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *