Dodoma. Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira, Cyprian Luhemeja amesema mazingira ni suala mtambuka, hivyo amewashauri mabalozi wa mazingira kutumia fursa zilizopo kupanua wigo wa kushiriki kuyatunza na kuchangamkia fursa zilizopo.

Taarifa ya ofisi hiyo kwa umma imesema Luhemeja ameyasema hayo jana Jumanne, Mei 20, 2025 jijini Dodoma alipokutana na kufanya mazungumzo na mabalozi wa mazingira.
Amewapongeza kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuunga mkono Serikali katika jitihada za kuhifadhi na kutunza mazingira hususan shughuli ya upandaji wa miti.

Amesema ili kuhakikisha suala la mazingira linagusa nchi nzima, Ofisi ya Makamu wa Rais iliwateua maofisa viungo wa mazingira katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara ambao hufanya kazi kwa ukaribu na maofisa mazingira wa mikoa pamoja na Makatibu Tawala.
“Nichukue nafasi hii kuwashauri mjipange ili kila mkoa uwe na balozi wa mazingira ambaye atafanya kazi kwa ukaribu na ofisa kiungo pamoja na ofisa mazingira wa mkoa husika, kwa kufanya hivyo mtaibua fursa nyingi za mazingira na kujipatia kipato,” amesema.

“Halmashauri nyingi sasa zinataka kujiunga na biashara ya kaboni, hivyo mkijipanga kimkoa na kwa kushirikiana na maofisa viungo na maofisa mazingira wa mikoa mnaweza kuingia kwenye fursa hizo,” amesema.
Kwa upande wa mabalozi hao akiwemo, Richard Kalongola amesema kutokana na uzoefu wake wa masuala ya maji na fukwe (diving) amenuia kujikita zaidi katika uchumi wa buluu wakati Dk Margaret Mutaleba alisema amepanga kujihusisha zaidi na usafi wa majiji.

Hivyo, mabalozi hao kwa umoja wao wamemshukuru Luhemeja kwa kutambua umuhimu na mchango wao katika kuhifadhi na kulinda mazingira.