Lugha ya kihaya ilivyosababisha mwenendo wa kesi kufutwa

Bukoba. Mahakama imefuta mwenendo wa hatua za awali za uhamishaji wa shauri la mauaji (committal Proceedings) kutoka Mahakama ya chini kwenda Mahakama Kuu, kwa kuwa mshtakiwa haelewi lugha ya Kiswahili wala Kiingereza.

Badala yake, mshtakiwa huyo, Mugisha John anazungumza lugha ya Kihaya pekee hivyo Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba imefuta mwenendo huo wa uhamishaji wa shauri hilo kutoka Mahakama ya Wilaya ya Misenyi kwenda Mahakama Kuu.

Uamuzi huo ulitolewa Machi 7, 2025 na Jaji Gabriel Malata na hukumu yake kupatikana jana Jumanne, Machi 11, 2025 katika mtandao wa mahakama wa Tanzlii ambayo ni tovuti ya Serikali inayochapisha uamuzi, sheria na kanuni bure mtandaoni.

Kesi hiyo ilikuwa imefikishwa kortini kwa ajili ya usikilizwaji wa awali (PH), mbele ya Jaji Malata, ambapo upande wa Jamhuri uliwakilishwa na wakili wa Serikali, Elizabeth Twakazi huku mshtakiwa John akitetewa na wakili Ibrahim Mswadick.

Baada ya kusomewa shitaka la mauaji na kuelezewa kosa hilo kwa lugha ya Kiswahili na kutakiwa kukiri ama kukana kutenda kosa hilo, mshtakiwa alishindwa kuelewa kiini cha kosa hilo kwa sababu alikuwa haelewi lugha ya Kiswahili.

Kulingana na matakwa ya kisheria, Mahakama iliamua kutafuta mkalimani anayefahamu lugha ya Kiswahili na Kihaya,  mwenye uwezo wa kutafsiri kutoka Kiswahili kwenda Kihaya na Kihaya kwenda Kiswahili ambapo alipatikana Joyce Kajuna.

Hoja za Mahakama, mawakili

Kabla Mahakama haijaendelea na PH, mawakili wa pande zote mbili waliibua hoja kuwa baada ya kubaini mshtakiwa anazungumza Kihaya pekee, mwenendo wa Mahakama ya wilaya ya Misenyi uliendeshwa bila msaada wa mkalimani.

Kwa maneno mengine, mawakili hao walisema mshtakiwa hakuelewa vizuri mashitaka dhidi yake hususan hatua ya ‘committal proceedings’, ambayo ni hatua muhimu sana kwa Mahakama iliyofanya hatua hiyo na mshtakiwa mwenyewe.

Hivyo waliiomba mahakama kuwa kwa suala la kushindwa kuelewa lugha ya Kiswahili ni mwendelezo ulioanzia Mahakama ya Wilaya ya Misenyi, tatizo hilo liligusa mzizi wa shauri hilo kwa kuwa mwenendo uliendeshwa bila mshtakiwa kuelewa.

Ni kutokana na mazingira hayo, Jaji alipata fursa ya kupitia kumbukumbu za shauri hilo katika Mahakama ya Wilaya ya Misenyi na kubaini kuwa mahakama hiyo haikuwa na mkalimani wa kutafsiri kutoka Kiswahili kwenda lugha ya Kihaya.

Jaji alisema mahakama imebaini mshtakiwa haelewi lugha nyingine isipokuwa Kihaya, tatizo la kutoelewa Kiswahili sio mara ya kwanza linatokea bali ni katika maisha yake yote na aliithibitishia mahakama anaelewa lugha ya Kihaya pekee.

Halikadhalika Jaji alisema mahakama imeridhika kuwa mshtakiwa anaelewa Kihaya peke yake kwa vile alishindwa kujibu maswali ya mahakama, mwenendo wa mahakama ya Misenyi ilifanyika bila mkalimani na mshtakiwa hakuelewa.

“Kwa mazingira haya, mwenendo wa kesi hiyo ya mauaji katika Mahakama ya Wilaya ya Misenyi ilihusisha tu Jamhuri na mahakama na kumnyima mshtakiwa haki ya kuelewa nini kilichokuwa kinaendelea mahakamani,” amesema Jaji.

“Kiukweli, kesi hii inawahusu parties (wadaawa) na sio mahakama. Hivyo ni wajibu wa mahakama kuhakikisha kuwa wadaawa hasa katika kesi za jinai wanaelewa kiini cha mashitaka na mwenendo ambao ndio huzaa maamuzi,” amesema.

“Kushindwa kumpa haki hizo mshtakiwa kunasababisha anyimwe haki ya kusikilizwa ambayo ni haki ya msingi chini ya Katiba ya Tanzania,”amesisitiza.

Uamuzi wa Mahakama

Kutokana na uchambuzi huo, Jaji Malata amesema mwenendo wa shauri hilo katika Mahakama ya Wilaya ya Misenyi ni msingi wa maamuzi mengine yote mbele ya Mahakama Kuu inayosikiliza shauri hilo na Mahakama ya Rufani ya Tanzania.

Jaji alisema kutokana na mapungufu hayo, mahakama inaamuru mwenendo huo katika mahakama ya wilaya ya Misenyi unafutwa kwa kuwa ulifanyika pasipo kuwepo kwa mkalimani kutafsiri lugha ya Kiswahili au Kiingereza kwenda lugha ya Kihaya.

Mbali na kueleza hivyo, Jaji alisema mshtakiwa hafahamu Kiswahili wala Kiingereza isipokuwa Kihaya pekee, hivyo anaiagiza mahakama ya Misenyi kuendesha upya ‘committal’ kwa msaada wa mkalimani kutafsiri lugha hizo.

Lakini pia mahakama hiyo imeagiza kuwa usikilizwaji huo ufanyike ndani ya siku 30 kuanzia tarehe ya uamuzi wake huo ambayo ni Machi 7,2025 na usikilizwaji wa awali (PH) wa shauri hilo sasa utaendelea Aprili 18,2025 saa 3:00 asubuhi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *