Mwanza. Katika safari ya maisha, kila mtu hukutana na changamoto zinazohitaji ujasiri wa hali ya juu kuzimudu.
Kwa wengi, kushika nyoka si jambo la kawaida, lakini kwa baadhi ni sehemu ya kazi na maisha yao ya kila siku.
“Mara ya kwanza niliposhika nyoka, kwa kweli nilikuwa naogopa sana,” anasema Loyce Ngoleigembe, akieleza jinsi alivyojifunza kukabiliana na hofu.
Kama ilivyo kwa mwanamke anayebeba ujauzito na hatimaye kujifungua, anasema alitambua ujasiri na uvumilivu ni silaha muhimu za kufanikisha jambo lolote maishani.
Loyce (49) ni mtaalamu wa kucheza na nyoka aina ya chatu ambaye kwa jamii ya Wasukuma anafahamika kwa jina la Nderema.

Mtaalam wa kuchezea nyoka aina ya chatu kwenye kundi la ngoma za asili la Buyegu Theatre Group, Loyce Ngoleigembe akizungumza na mwandishi wa makala haya. Picha na Mgongo Kaitira
Akiwa mama wa watoto wanne, katika mahojiano maalumu na Mwananchi anasema safari yake ya kucheza ngoma za asili ilianza mwaka 2003 alipojiunga na kikundi cha sanaa cha Buyegu, na mwaka 2007 nilianza kucheza na chatu.
“Nilijiuliza mbona mwanamume anashika nyoka, kwa nini nisiweze? Nikaanza mazoezi kidogo-kidogo akanifundisha kijana wangu, baadaye nikawa mkakamavu nikashika nyoka,” anasema.
Anasema mara ya kwanza aliogopa, swali lililogonga akili yake ni vipi iwapo nyoka huyo atamuuma? Hata hivyo, anaeleza alijikaza, akazoea na sasa ni mtaalamu wa kucheza na nyoka huyo katika hafla mbalimbali.
“Nikajikaza kama mwanamke kubeba mimba kwenda hospitali kujifungua. Siku moja nikamtoa kwenye sanduku nikambeba, kuanzia hapo nikaona kawaida kucheza na nyoka,” anasimulia.
Katika miaka 18 ya kucheza na nyoka anasema ameshawahi kuumwa na kiumbe huyo mara tatu akitumbuiza kwenye matamasha.
Anaeleza baada ya tiba, huendelea na kazi yake inayomuingizia kipato kinachomwezesha kuhudumia familia.
“Ninapomshika najihisi raha sababu nimeshamzoea, namchezea, akiruka nami naruka akinigonga nakunywa dawa… nilishagongwa na nyoka mara tatu, nilihisi maumivu kidogo nikanywa dawa, nikachanjwa nikaendelea kumchezea,” anasema.
“Kuna siku kwenye Sikukuu ya Nane Nane pale Nyamhongolo (Wilaya ya Ilemela) wakati nataka kumkamata (chatu) nikateleza kwenye nyasi akaniwahi kugeuka akanigonga kwenye mkono. Tukamaliza kucheza wakaniweka dawa nikaendelea na maisha mengine,” anasema.
Loyce anasema sanaa imemnufaisha si tu kuhudumia watoto wake na kuwasomesha, bali pia imemwezesha kufika mikoa mbalimbali nchini, ukiwamo wa Dar es Salaam aliokuwa akiusikia tu ukitajwa midomoni mwa watu.
“Kupitia sanaa hii nimezunguka mikoa mbalimbali. Zamani nilikuwa nasikia tu kuna Dar lakini nimefika, wakati wa mashindano tukawa wa kwanza. Mbeya tukawa wa kwanza na Njombe tukawa wa kwanza kwenye mashindano ya kucheza na nyoka,” anasema.
“Sijawahi kuona mwanamke anayecheza na nyoka tofauti na kikundi chetu. Napenda na wengine wajifunze kama mimi. Ni ukakamavu tu, hakuna dawa ninayotumia ili nishike nyoka.”
Anasema dawa yake ni rozari na anamtegemea Mungu pekee, siyo waganga wa kienyeji ili wampe dawa ya kushika nyoka.
Loyce anasema jamii inayomzunguka inamuona jasiri, wengine wakitamani kuwa sawa naye hasa Kisesa, wilayani Magu anapotokea.
Anavyozungumzwa
Mkurugenzi wa kikundi cha ngoma za asili cha Buyegu, Martina Lubango anasema kina wanachama 27, wanawake 11, huku watatu pekee ndio wameteuliwa kucheza na nyoka akiwamo Loyce.
Anasema licha ya kuwa wanacheza ngoma za makabila yote hususani la Kisukuma, watazamaji wanavutiwa zaidi na ngoma ya Buyeye inayochezwa na nyoka. Mvuto huwa zaidi Loyce anapocheza na chatu (Nderema).
Anasema kikundi chao kina nyoka watatu ambao hawajatolewa meno kama wengi wanavyodhani.
Anaeleza ujasiri wa Loyce na wanaume wawili wanaocheza nao ndio unaowawezesha kucheza na viumbe hao.
“Ni ujasiri tu. Ukionesha ujasiri unakamata nyoka, hatuwatoi meno kwa sababu ukiyatoa wanawahi kufa. Nyoka huyu hana sumu ya kutisha kusema kwamba labda atakung’ata utapata madhara makubwa. Anaweza akakung’ata ukaonyesha kuvimba kidogo lakini tuna dawa ya kupaka na kunywa mambo yanaendelea,” anasema.
“Dada huyu alianza kucheza ngoma, baadaye alihoji ni kwa nini huyu anakamata nyoka peke yake? Tuna nyoka watatu kwa nini nisijifunze? Basi wakawa wanaambizana wao kwa wao akafundishwa ikafika wakati akawa jasiri wa kushika na kucheza na nyoka,” anasema.
Viumbe hao anasema huwanunua wakiwa wakubwa kutoka porini baada ya kupata vibali kutoka mamlaka husika.
Anaeleza wanapozeeka huwarudisha porini na kuanza mchakato wa kupata kibali kingine cha kumiliki nyoka hao ambao ni nyara za Serikali.
“Tumesharudisha nyoka wawili waliozeeka, si kwamba wakiishazeeka uwaache tu wafe au uwafungulie watembee tu huko hapana! Sharti wakishazeeka warudishe porini wakaendelee na maisha,” anasema.
Anasema nyoka hao huwalisha kuku wawili ndani ya wiki moja na ni lazima kuku awe hai ili amuwinde mwenyewe na kwamba, wakati anakula hataki kelele.
“Huwa tunawarushia kuku ndani ya banda kwa sababu huwa tunawajengea mabanda na dimbwi la maji, hivyo unaporusha kuku mzima huwinda akiwa ndani. Anapowinda hapendi kelele, hivyo huwa tunamuacha peke yake wote tunaondoka nyumbani kwa wakati huo,” anasema.
Anaeleza eneo liliko banda la nyoka hao hakuna watu wanaoruhusiwa kupita.
Sanaa hiyo anasema imewawezesha wanakikundi akiwamo Loyce kupata mapato kwa ajili ya familia zao na kujuana na watu.
Kwa upande wake, imemwezesha kusafiri nje ya nchi katika mataifa ya Uganda, Sweden, Denmark na Ujerumani.
Mwanachama wa kikundi hicho, Silvester Kambula anasema licha ya kuwa na uzoefu wa kucheza na kupiga ngoma za asili tangu mwaka 1993 hadi mwaka huu hajawahi kupata uthubutu wa kucheza na nyoka.
“Nina uwoga wa kukamata nyoka, siyo rahisi. Ni mchezaji na mpigaji wa ngoma mpaka leo nitakachowasaidia labda ni kubeba sanduku likiwa limefungwa na kupandisha kwenye gari kama tunakwenda sehemu fulani kuonyesha shoo,” anasema.

“Nilipoingia katika kikundi cha Buyegu dada huyu alinishangaza kwa ujasiri. Ni wachache, hata jamii tu inayokuzunguka wakiona wapo watakaokusifia, wapo watakaokuogopa, hawaamini kwamba anakamata kwa hiari yake,” anasema.
Kila kazi haikosi changamoto, kwa wanakikundi hao ya kwao ni malipo madogo kutoka kwa watu wanaowaalika, ambayo hayaendani na gharama za kuhudumia nyoka na uhifadhi wa vifaa vya asili wanavyotumia.
Mkurugenzi Lubango anasema wakati mwingine wanalipwa Sh300,000 ambayo hugawana wanakikundi wote 27, usafiri na gharama za kuhudumia nyoka watatu ambao kwa wiki kila nyoka anakula kuku wawili wanaouzwa kati ya Sh20,000 na Sh25,000 kulingana na upatikanaji wake.
Sifa za nyoka jamii ya chatu
Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali duniani, asilimia 98 ya nyoka hao hawana sumu, japo kuna aina zaidi ya 3,000 za nyoka duniani lakini aina 200 sawa na asilimia mbili pekee ndiyo wenye sumu.

Nyoka wenye sumu huitumia kuwinda, kusaidia mmeng’enyo wa chakula na kujilinda dhidi ya adui. Wasio na sumu hutumia njia mbadala kuhakikisha wanapata chakula na kujilinda.
Miongoni mwa wasio na sumu ni jamii zote za chatu ambao hujipatia chakula kwa kunyonga windo lake na kulivunjavunja kabla ya kulimeza, kadiri windo linavyovuta pumzi ndivyo chatu huongeza bidii ya kunyonga.
Jamii hii ya nyoka hujikinga na maadui kwa kuwang’ata ili kusababisha maumivu, kujifananisha na mazingira, kujiviringisha ili kuficha kichwa, kutetemesha mkia na wengine hujisugua magamba ili kutoa sauti ya kumtisha adui. Hata hivyo, hatari inavyozidi kuwa kubwa kwao, hukimbia kwa usalama.