Lori la mafuta laripuka na kuua watu 90 kaskazini magharibi mwa Nigeria

Takriban watu 90 wamepoteza maisha na wengine 50 kujeruhiwa baada ya lori la mafuta kuripuka na kusababisha moto mkubwa kaskazini magharibi mwa Nigeria.

Msemaji wa jeshi la polisi, Lawan Adamu amethibitisha habari hiyo na kusema kuwa lori hilo limeripuka kando ya barabara kuu ya Kano-Hadejia kwenye eneo la Taura la jimbo la Jigawa la kaskazini magharibi mwa Nigeria.

Ameongeza kuwa, tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo Jumatano na kusababisha hasara kubwa ya mali na roho za watu.

Matukio kama hayo ni jambo la kawaida nchini Nigeria. Mwanzoni mwa mwezi uliopita wa Septemba, makumi ya watu walipoteza maisha baada ya lori la mafuta kuripuka kaskazini mwa Nigeria.

Ajali kama hizi mbaya zinazopelekea magari kuwaka moto ni jambo la kawaida nchini Nigeria

Mkuu wa Idara ya Dharura ya Jimbo la Niger huko Nigeria (NSEMA), Abdullahi Baba Arah alisema wakati huo kuwa, watu 48 walipoteza maisha baada ya lori hilo kugongana na gari nyingine. 

Mbali na kupoteza maisha makumi ya watu, ajali hiyo ilisababisha hasara pia kwa mifugo ambapo kwa mujibu wa mkuu huyo wa NSEMA, mifugo 50 iliteketea kwa moto kwenye ajali hiyo. 

Aidha ajali mbaya za barabarani huripotiwa mara kwa mara nchini Nigeria, na mara nyingi husababishwa na upakiaji kupita kiasi, hali mbaya ya barabara na kuendesha gari kwa kasi ya juu. 

Ubadhirifu na rushwa iliyokithiri ni sababu nyingine inayopelekea kutoheshimiwa viwango na sheria za usafiri nchini Nigeria.