Liverpool, Man United safi, Arsenal mambo magumu

Liverpool, England. Liverpool chini ya kocha Arne Slots imeonyesha kuwa imepania kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu baada ya jana kuichapa timu ngumu ya Newcastle mabao 2-0 na kukaa juu ya Arsenal kwa pointi 13.

Hii ina maana kuwa sasa Liverpool inakaribia kutwaa ubingwa huo, ikiwa ni mara ya pili kwa miaka ya hivi karibuni baada ya Jurgen Klopp kufanya hivyo.

Arsenal iliendelea kuwa na matokeo mabaya kwenye ligi hiyo baada ya kuambulia suluhu dhidi ya Nottigham Forest na kuipa Liverpool wingo mpana wa kutawala kwenye kilele cha ligi hiyo maarufu duniani.

Liverpool ikiwa kwenye Uwanja wa Anfield ilifanikiwa kujipatia mabao yake kupitia kwa Dominik Szoboszlai katika dakika ya 11 ya mchezo, huku bao la pili likiwekwa kimiani na Alexies Mac Aliister katika dakika ya 63 na kuihakikisha ushindi huo muhimu.

Ikiwa imebakiza mechi kumi kabla msimu haujamalizika, Liverpool imefikisha pointi 67 ikishinda michezo 20 na sare saba na kupoteza mmoja tu msimu huu ikiwa inapewa nafasi kubwa zaidi ya kutwaa ubingwa huo msimu huu.

Ikifuatiwa na Arsenal ambayo imeshacheza michezo 27 ina pointi 54, imetoka sare mechi tisa, imepoteza tatu na kushinda 15 ikiwa inaendelea kuwa na wakati mgumu kwenye ligi hiyo.

Manchester United ikiwa kwenye Uwanja wa Old Trafford iliibuka na ushindi mgumu wa mabao 3-2 dhidi ya Ipswch Town.

Huu ulikuwa mchezo muhimu kwa United ambayo haina matokeo mazuri msimu huu, bao la kwanza la timu hiyo liliwekwa kimiani na Sam Morsy aliyejifunga, Matthijs alifunga la pili dakika ya 26, huku Harry Maguire akiwa pia shujaa kwenye timu hiyo akifunga bao la tatu dakika ya 47.

Wageni hao ambao wanapambana kuhakikisha wanatoka mkiani walifanikiwa kujipatia mabao yao kupitia kwa Jaden Philogene aliyefunga yote mawili katika dakika ya nne na 45 za mchezo huo ambao United walimaliza wakiwa pungufu baada ya Patrick Dorgu kupewa kadi nyekundu.

Ushindi huo umeifanya United isogee nafasi moja, baada ya kutoka ile ya 15 iliyokaa kwa muda na kwenda hadi nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa imebakiza mechi 11 msimu huu.