Liverpool, Barcelona zatakata Ulaya

Paris, Ufaransa. Liverpool ikiwa ugenini ilifanikiwa kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya PSG kwenye mchezo ambao ulikuwa wa kasi na kuvutia, huku Barcelona, Bayern nazo zikichomoka kwa ushindi.

Hizi zilikuwa mechi za kwanza za hatua ya 16 Bora za Ligi ya Mabingwa Ulaya ambapo timu kadhaa zimeshajiweka kwenye nafasi nzuri ya kutinga hatua ya robo fainali.

PSG ilitawala mchezo kwa sehemu kubwa ambapo pamoja na Liverpool kupata ushindi huo ilifanikiwa kupiga shuti moja tu lilolenga lango.

Bao la Majogoo hao wa Anfield liliwekwa kimiani na Harvey Ellotti katika dakika ya 87 ya mchezo na kuifanya timu hiyo inayowania ubingwa wa England kwa nguvu kubwa kuwa na nafasi kubwa ya kutinga hatua ya robo fainali itakaporudi kwenye mchezo wake wa nyumbani wiki ijayo.

Barcelona nayo ikiwa ugenini ilionyesha kiwango bora na kuibuka na ushindi wa bao 1-0 pamoja na kwamba ilikuwa pungufu uwanjani kwa muda mrefu.

Bao la Barcelona ambayo staa wake Pau Cubarsi alipewa kadi nyekundu katika dakika ya 22 ya mchezo, lilifungwa na Raphina katika dakika ya 61 ya mchezo huo uliokuwa na kosa kosa nyingi.

Hata hivyo, mechi iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wakiamini kuwa kutakuwa na matokeo ya kushangaza kati ya Bayern Munich dhidi ya Bayern Leverkusen ndiyo iliyokuwa na mabao mengi kwa jana.

Bayern Munich ikiwa kwenye kiwango bora zaidi msimu huu ilifanikiwa kuibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0, huku staa Harry Kane akifanikiwa kufunga mawili.

Kane alifunga bao lake la kwanza katika dakika ya tisa, huku akiweka la pili kwa penalti katika dakika ya 75, bao lingine la Bayern lilifungwa na Jamal Masiala dakika ya 57.

Hata hivyo, Leverkusen ambao ndiyo mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Ujerumani Bundesliga walimaliza pungufu baada ya Nordi Mukiele kupewa kadi nyekundu katika dakika ya 62 ya mchezo huo.

Sasa mashabiki wanasubiri kuona nini kitatokea kwenye michezo ya pili ya ligi hiyo wiki ijayo.