Lissu: Tutaiondoa CCM madarakani kwa uchaguzi huru siyo silaha

Mbeya. Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema namna bora ya kukiondoa Chama Cha Mapinduzi (CCM) madarakani ni kutumia utaratibu wa uchaguzi huru, haki na siyo kutumia silaha.

Pia, kimesema bila kudai mabadiliko katika uchaguzi haitawezekana kuking’oa CCM madarakani kutokana na mazingira yalivyo kwa sasa kikiwaomba wananchi kuamua.

Akizungumza leo Machi 23, 2025 kwenye mkutano wa hadhara ulioambatana na kuzindua operesheni ya ‘No Reforms No Election’, Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Tundu Lissu amesema kwa takwimu za uchaguzi kwa miaka 10 iliyopita na mwaka jana vinashangaza.

Amefafanua kuwa katika miaka 10 iliyopita ya uchaguzi 2014, Chadema ilipata vijiji 1,754 na mitaa 980, lakini kwa uchaguzi uliopita 2024, chama hicho kimepata vijiji 97 sawa na asilimia 0.8 huku mitaa wakibeba 36 kwa nchi nzima.

“Siku ya uchaguzi wagombea wetu wanaenguliwa, Polisi na watumishi wanakuja na mabegi yenye kura haramu, wanatembea na vifaru, watu wanauawa, hivyo kwa utaratibu huu hatuendi popote.”

“Kwa maana hiyo wakiendelea kutawala watatumaliza, hivyo ili kuondokana na hali hii, tubadili hali ya uchaguzi, tubadili tume, hakuna mtumishi kusimamia uchaguzi, wagombea waapishwe na kutoenguliwa ili kura zihesabike kama ilivyokuwa 1995” amesema Lissu.

Ameongeza kuwa jukumu lao kwa sasa ni kubadili utaratibu wa uchaguzi na iwapo watashindwa basi wataisha, akisisitiza kuwa Chadema haitashindwa.

Amesema ili kubadili utaratibu huo ni kukwamisha uchaguzi mkuu wa mwaka huu akieleza kuwa hakuna mtu atawekewa bunduki kwenda kupiga kura, wala kujiandikisha na kwamba nguvu ipo kwa wananchi kuleta mabadiliko.

“Tukikwamisha kelele itakuwa kubwa kwa nchi na dunia kwa ujumla, watakuja mezani kuzungumza na uwezo tunao wa kukwamisha, hebu angalieni mlivyokuja kwa wingi, hatuwezi kuamua? Hatuwezi? Amehoji huku wananchi wakiitikia kuwa wanaweza.

“Tuwaambie na viongozi wa vyama vingine, wa kidini kwani hili linatuhusu wote wakiwamo Polisi, mtumbwi wetu ndio huu, tuunganishe nguvu ya pamoja ili kubadili mfumo wa uchaguzi kama alivyofanya Jaji Nyalali na Warioba tunachodai ni haki tu” amesema Lissu.

Awali Mwenyekiti wa Chama hicho Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ amesema kwa sasa anapokea simu nyingi wananchi wakiuliza hatima yake ya uchaguzi akieleza kuwa hawawezi kushiriki uchaguzi iwapo hakutakuwapo mabadiliko.

Amesema kwa sasa hali ya maisha kwa wananchi yamekuwa magumu ikiwamo makandarasi kudai fedha zao na migogoro ya ardhi, akiahidi Chadema kuyafanyia kazi kuhakikisha kila mtu anapata haki yake.

“Uchaguzi ambao kila mara lazima uumize watu, kipindi nachaguliwa kuwa mbunge yalichomwa matairi, tunaumiza Watanzania bila kujali, ndio maana tumekuja na No Reforms No Election’ ” amesema Sugu.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Bara, John Heche amesema Tanzania inazo rasilimali nyingi lakini kutokana na uongozi usio na uwezo changamoto ya ajira na uchumi vimekuwa kero.

Amesema miundombinu ya barabara, huduma za afya na elimu ni tatizo akieleza kuwa wananchi wanapaswa kuunga mkono juhudi za Chadema katika kudai mabadiliko na kuheshimu thamani ya kura za wapigakura.

“Serikali inaandaa bajeti lakini haina uhakika wa fedha hizo, kwa kuwa inategemea hisani, tunakosa uongozi thabiti na ili kupata maisha bora lazima tuombe kwa mabadiliko, hatutaki huruma ya CCM”

“Gesi wanazotoa haziwezi kutufikisha popote, hiyo gesi ikiisha hakuna wa kukujazia na baada ya uchaguzi shida zitarejea upya, tunachohitaji ni mtu awe na uchumi wake binafsi kuondokana na utegemezi” amesema Heche.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *