Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu amesema siku ya uchaguzi mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu, chama hicho kitaitisha maandamano ya kuuzuia uchaguzi usifanyike.
Kauli hiyo ya Lissu, inajibu swali kuhusu mbinu ambayo chama hicho itaitumia kuzuia uchaguzi kuendana na ajenda yake ya ‘No Reforms, No Election’ (bila mabadiliko, hakuna uchaguzi).
Lissu amesema hayo leo, Jumatatu Aprili 7, 2025 wakati akihutubia mkutano wa hadhara Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara katika ziara ya kutoa elimu kuhusu ‘No Reforms, No Election.’

Amesema iwapo Serikali haitafanya mabadiliko ya sheria na kanuni za uchaguzi, chama hicho kitawahamasisha wananchi kuandamana kuuzuia uchaguzi usifanyike.
“Hatutaenda kupiga kura, hatutaenda kujiandikisha, siku ya kupiga kura tutaandamana, watatufunga wote? Kuna sheria ya Tanzania inayosema lazima tushiriki kwenye chaguzi za kijinga?” amehoji.
Sababu ya hatua hiyo, amesema hawataki kwenda kwenye uchaguzi unaosimamiwa na wale walioharibu chaguzi za miaka iliyopita.
“Tutafanya kila linalowezekana kuhamasisha umma wa Watanzania kuzuia uchaguzi,” amesema.

Msimamo huo wa Lissu umesisitizwa na mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho, Godbless Lema akisema iwapo hakutakuwa na mabadiliko ya sheria na kanuni za uchaguzi, chama hicho hakitaingia kwenye mchakato huo wa kikatiba.
“Sio tutasusa, siku ya uchaguzi tutaitisha maandamano ya amani nchi nzima, tutazuia uchaguzi kufanyika. Hakuna kupiga kura na maana yake uchaguzi hautafanyika,” amesema.
Sababu ya yote hayo, amesema wanataka Tume Huru ya Uchaguzi ili kuwepo mazingira sawa kwa vyama vyote kushindana.
Katika ufafanuzi wake, ameeleza haitawezekana kupatikana kwa Tume Huru ya Uchaguzi iwapo Rais ambaye pia ni mgombea ataendelea kuwateua wasimamizi wa uchaguzi.
Lema amesema mazingira hayo yanasababisha kukosekana nafasi ya ushindi kwa vyama vya upinzani, ndio sababu Chadema imeamua kuzuia uchaguzi.
Amesema wapo wanaodai kuwa Chadema hawana nguvu ya kuzuia uchaguzi kwa sababu wanachama wao ni waoga.
Katika hotuba yake, Lissu ameyataja mambo anayotamani yafanyiwe mabadiliko, ikiwamo kuondolewa kwa utaratibu wa viongozi wa Tume kupatikana kwa kuteuliwa na kiongozi anayetokana na CCM.
Pia, amesema mabadiliko yafanyike kwa kuandikishwa upya kwa daftari la kudumu la wapigakura ili kuondoa wapigakura feki na hilo lifanywe na Tume Huru ya Uchaguzi.
Jambo lingine, amesema ni kukomesha mtindo wa kuwaengua wagombea kwa kubadilishwa sheria ya uchaguzi ili ikataze kuwepo kwa uchaguzi wa mgombea pekee.
“Sheria iseme kama mgombea hajui kujaza fomu, hakuna kuengua wagombea tena na Katiba iseme hakuna uchaguzi wa mgombea mmoja tena,” amesema.

Lissu amesema wanataka mabadiliko ya kuondolewa kwa fujo zinazofanywa na vyombo vya usalama dhidi ya vyama vya upinzani wakati wa kampeni.
Amesisitiza iwapo hayo hayatatekelezwa mwaka huu, watawahamasisha Watanzania kuzuia uchaguzi usifanyike na ujumbe huo wataufikisha duniani kote.