Lissu: Nimejiandaa kufungwa katika kudai haki mfumo wa uchaguzi

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasi na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu amesema amejiandaa kufungwa katika mapambano ya kudai haki katika mfumo wa uchaguzi ili mchakato uwe wa usawa kwa vyama vyote.

Februari 12, 2025 akiwahutubia Watanzania katika ofisi za makao makuu ya Chadema, Mikocheni Lissu alitangaza chama hicho kuanzisha vuguvugu la mabadiliko ya kimfumo ya uchaguzi kuekelea Uchaguzi Mkuu 2025 likiwa na kaulimbiu ya ‘No reforms, No elections’ (Hakuna mabadiliko, Hakuna uchaguzi).

Lengo la vuguvugu hilo ambalo kampeni yake itaanza mwezi ujao katika mikoa ya kusini, ni kuunganisha nguvu za Watanzania katika kudai kwenye mfumo wa uchaguzi.

Lissu ambaye ni mbunge wa zamani wa Singida Mashariki ameeleza hayo leo Jumamosi Februari 15, 2025 akizungumza na wananchi wa Manyoni mkoani Singida aliposimama kuwasalimia akielekea wilayani Ikungi ambapo atakuwa na mkutano wa hadhara.

“Kama hawataki kufanya mabadiliko kwa hiari, basi tunakwenda kwenye kushurutishana, kama ni kufungwa mimi nimejiandaa,”amesema Lissu kisha akanyamaza kidogo kwa sekunde kadhaa na kuwasikiliza wananchi aliokuwa akiwahutubia ambao walisikika wakisema tupo pamoja.

“Kauli mbiu yetu bila mabadiliko, hakuna uchaguzi, tujiandae kuzuia uchaguzi kama hawataki kuleta mageuzi. Nitaongoza mfumo wa kudai mapambano haya ya kushurutisha ili tupate mfumo mzuri wa uchaguzi,”amedai Lissu.

Kwa mujibu wa Lissu, endapo chama hicho, kitakwenda kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2025, basi hakitaambulia chochote kwa madai ya kuwa mifumo ya chaguzi siyo rafiki.

Amesema Chadema kitakwenda kupata maumivu pasipo kuambulia kitu, huku akirejea matokeo ya uchaguzi wa Serikali za mitaa wa 2024, ambayo kwa mujibu wa Tamisemi Chadema kilipata viti 87 wa vijiji nchini nzima, jambo ambalo Lissu amedai halikuwa na uhalisia.

Mwenyekiti huyo, amedai kuwa hana imani na uchaguzi mkuu utakaofanyika mwishoni mwaka huu kama utakuwa huru na haki, endapo mifumo ya mchakato huo haitarekebishwa.

Lissu amesema anakwenda Ikungi na Mahambe mkoani Singida kwa ajili ya kupata baraka za wazee katika jukumu lake jipya la uenyekiti wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

“Nakwenda nyumbani kwetu kuwaomba wazee waweke mikono yao ya baraka kwenye hii kazi nitakayoenda kuianza. Nataka wazee waweke mikono na kusema sasa mtoto wetu nenda kafanye kazi, tukishamaliza tutaingia kazini, tutaitembea nchi yote kuzungumzia habari za chaguzi za Tanzania,” amesema.

 “Jiandaeni kila mmoja wetu aweke mkono wa Baraka na afanye kwa sehemu yake, tujitolee hii kazi ni yetu sote,”amesema Lissu.