
Ukweli upi unapaswa kuzungumzwa? Unaompa faraja mgonjwa lakini haumsaidii kubadili hali yake? Unaomuumiza mgonjwa, ila ndiyo ukweli wenyewe? Mimi nachagua ukweli unaoweza kuonekana ukatili.
Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, yupo mahabusu. Kesi inayomkabili ni uhaini. Wakati huohuo, giza limetanda kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025. Ushiriki wa Chadema kwenye uchaguzi ni majaliwa. Inategemea busara zaidi. Swali, tumefikaje huku?
Nakumbuka nyakati Dk Samia Suluhu Hassan, alipoapishwa kuwa Rais wa Tanzania. Ghafla kila kona zilisikika kelele za kudai Katiba Mpya. Kelele hizo zilinifanya niandike makala yenye kichwa “Miluzi mingi ya Katiba itachokonoa ubinadamu wa Rais Samia.” Ulikuwa mwaka 2021.
Niliuliza; ni kwa nini wakati huo ndiyo madai ya Katiba yalikuwa mengi? Kiulizo hicho kilifuatiwa na viulizo vingine kadhaa; je, Rais Samia anaonekana ana ukatiba mwingi? Ama ameonekana ni msikivu zaidi? Au kwa vile alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Katiba mwaka 2014?
Viulizo viliendelea zaidi kwa kuzingatia kwamba baadhi ya hoja za kudai Katiba zinajengewa ushawishi kutokana na kile kilichotokea Uchaguzi Mkuu 2020. Kwamba makosa yaliyofanyika hayapaswi kurejea. Isiachwe mbali hii; Rais aliyekuwa madarakani ni Dk John Magufuli.
Kuna hoja zilitolewa, kwamba watu hawataki kurejea makosa waliyoyaishi wakati wa Dk Magufuli. Ni hapo sasa viulizo viliendelea; mbona hakukuwa na mwamko wa kumdai Magufuli Katiba kama ilivyo kwa Samia? Maana yeye ndiye mtajwa. Je, Rais Samia anaonekana mwepesi kudaiwa?
Swali hilo la mwisho ndilo lilikaribisha hisia za ubinadamu. Endapo Rais Samia angejiuliza swali hilo, kwamba anaonekana mwepesi ndiyo maana alidaiwa Katiba kuliko mtangulizi wake, angeweza kuingiwa na ubinadamu.
Niliandika kuwa huo ubinadamu ndio ungeweza kusababisha Rais Samia aamue kuziba masikio ili watu wasimwone mwepesi. Haikuchukua muda mrefu baada ya andiko langu hilo, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alikamatwa na kushitakiwa kwa makosa ya ugaidi.
Mbowe alikaa mahabusu kwa miezi nane. Aliachiwa nyakati ambazo Rais Samia alikuwa ametambulisha falsafa ya R4; Reconciliation (Maridhiano), Resilience (Ustahimilivu), Reform (Mabadiliko) na Rebuilding (Ujenzi mpya).
Lissu amekuwaje mahabusu baada ya utambulisho wa R4? Hotuba ya Rais Samia, kwenye mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa na Wadau wa Demokrasia, inaweza kunipa mwanzo mzuri wa kwa nini nchi imefika huku.
Hotuba yake hiyo ya Septemba 11, 2023, Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC), ilimtofautisha na Samia mwenye sauti ya upole, aliyezoeleka na kumleta mpya.
Rais Samia aliwahi kusema mwenyewe kuwa hahitaji kuongea kwa vishindo ili ujumbe ufike. Hata hivyo, nyakati zilibadilika. Dhahiri mambo mengi yaliyotokea yalitikisa ustahimilivu wake.
Hotuba ya Rais Samia iligusa vipengele nane; la kwanza ni Mapendekezo ya Kikosi Kazi. Pili, demokrasia. Tatu, mikutano ya hadhara. Nne, uhuru wa maoni. Tano, Katiba. Sita, mmomonyoko wa maadili.
Saba, Uchaguzi Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025. Nane, dira ya maendeleo 2025-2050. Japokuwa alitaja vichwa husika, lakini alikuwa akihama mara kwa mara na kujielekeza kuwashughulikia aliowaita watukanaji.
Yupo mtu muda huu angeweza kusema Rais Samia alitoa hotuba mbaya. Mwingine angewaza, mbona siku zote alizungumza kwa upole na ustaarabu mwingi. Yupo ambaye atakumbusha uhusika wa Samia Bunge la Katiba 2014; mwanamke mtulivu, mvumilivu, mkomavu na mstahimilivu.
Hakosekani wa kusema kuwa Rais Samia alishavumilia mengi. Sakata la mkataba wa Bandari, baina ya Tanzania na kampuni ya Dubai, DP World, lilipoibuka, alisakamwa kuwa yeye ni Mzanzibari, lakini anauza bandari za Watanganyika. Je, hakuumia kwa mashambulizi hayo?
Kabla ya kuunda Tume ya Mipango, Rais Samia aliomba watu wapendekeze majina ya wale ambao inaonekana wangefaa. Taifa linajengwa moja, badala ya wengine kukosoa tu, kama wana uwezo na mawazo mazuri, basi watumike kwa masilahi ya nchi.
Lissu, alipotakiwa kutoa maoni kuhusu ombi hilo la Rais Samia, alijibu “hiyo akili ni matope.” Ni kosa kubwa kuamini kwamba hilo jibu halikumuumiza Rais Samia.
Hakuna binadamu mwenye uvumilivu wa kudumu. Hata ajaliwe moyo wa subira kiasi gani, zipo nyakati atatetereka. Je, Rais Samia ameamua kuacha nchi iende yenyewe bila R4? Au amejihakikishia kwamba wapinzani hawabebeki?
Rafiki yangu mmoja aliwahi kuniambia kuwa pamoja na matatizo ya kidemokrasia, sheria na mifumo ya uchaguzi kuwa na upungufu, tatizo kubwa Tanzania ni wanasiasa wa upinzani kupenda kudeka.
Kwamba Rais Magufuli alipoyafanya mazingira ya kisiasa kuwa magumu, wanasiasa walinyamaza, waliojitoa mhanga walikosoa kwa tahadhari kubwa. Lissu na wengine, waliishi uhamishoni Ulaya na Amerika (Canada).
Msomi mmoja wa sayansi ya siasa aliwahi kuniuliza; kati ya Rais Samia na wapinzani, nani aliyezihitaji zaidi R4? Mimi nilimjibu kuwa nchi ilizihitaji. Akaniuliza tena; ukiondoa nchi, kati ya Rais Samia na wapinzani, nani alihitaji R4 zaidi.
Nilimjibu msomi huyo kwamba wote walizihitaji. Jibu langu halikumtosheleza msomi, akasema, wapinzani walizihitaji zaidi R4 kuliko Rais Samia, lakini matendo yao yalikuwa sawa na mtoto mwenye madeko, ana njaa lakini anajifanya hataki kula mpaka abembelezwe.
Ufafanuzi wa msomi huyo ulitetewa na hoja kwamba Rais Samia aliposhika madaraka ya nchi, alikuta hali ya kisiasa siyo nzuri, lakini ilikuwa imeshajitengeneza. Wapinzani walinyamazishwa na dola ilikuwa na nguvu ya kufanya chochote. Bunge tayari lilishakuwa na nguvu ya upande mmoja. Hivyo, Rais Samia kama angetaka kutawala peke yake, hakuhitaji R4.
Wapinzani ndio walizihitaji R4 zaidi, maana walitaka kufanya siasa na kushindana kisiasa, mlango ambao ulifanywa kuwa mgumu na Magufuli. Rais Samia aliamua kufungua milango ya kisiasa. Shughuli za kisiasa zikawa halali. Waliokuwa uhamishoni wakarejea.
Msomi alisema, wapinzani kwa tabia ya madeko, badala ya kuzitumia R4 kama fursa ya mwanzo mzuri wa kujenga siasa safi kwa nchi, wao waliamua kuzitweza, mithili ya mtoto mwenye madeko anavyochezea sahani ya chakula. Ndiyo sababu ya kufika hapa.
Ombi kwa Rais Samia, akiwa pia Mama wa nchi, anapaswa kukumbuka methali ya “mtoto na mkono”. Taifa linahitaji siasa safi. Historia itamkumbuka daima atakapofanikisha mageuzi chanya kisiasa bila visasi, vinyongo wala chuki.