Lissu kuhutubia wananchi Morogoro akielekea Ikungi

Morogoro. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu anatarajiwa kuzungumza na wananchi wa Manispaa ya Morogoro, leo Ijumaa Februari 14, 2025, akiwa njiani kuelekea Ikungi mkoani Singida.

Lissu yuko njiani kuelekea Ikungi, Singida, atasimama katika eneo la Msamvu kuwasalimia wananchi kabla ya kuendelea na safari yake.

Hii ni mara ya kwanza kwa Lissu kwenda kwao Wilaya ya Ikungi mkoani Singida tangu amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chadema, Januari 21, 2025.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kati, Devota Minja, Lissu, pia, atapita na kusalimia wananchi katika maeneo ya Magubike (Kilosa) na Gairo Stendi.

Lissu na msafara wake watapumzika Dodoma, baada ya mapumziko hayo, ataendelea na safari yake kesho Februari 15, 2025 ambapo atafanya mkutano wake wa kwanza wa hadhara katika Jimbo la Ikungi tangu achaguliwe kuwa Mwenyekiti wa Chadema.

Minja amesema Lissu ameanza ziara yake Ikungi kama ishara ya heshima, kwani ndipo aliposhinda ubunge kwa mara ya kwanza, pia, ni nyumbani kwake.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa taarifa zaidi.