Lissu, Chalamila walivyomzungumzia Profesa Sarungi

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Tundu Lissu, amesema kuwa Profesa Philemon Sarungi amefanya kazi nzuri nchini na kwamba maisha yake yanapaswa kusherehekewa. Lissu amesisitiza kuwa uwepo wa watu wa aina hiyo duniani unafanya maisha kuwa bora na ya maana zaidi.

“Kuna nini la kusema zaidi? Nafikiri uwepo wa watu wa aina hii katika dunia hii unafanya maisha ya dunia hii kuwa mazuri zaidi. Uwepo wa watu wa aina ya Sarungi unatuwezesha kuwa na imani kwamba bado inawezekana kuwa na nchi na jamii iliyo bora zaidi.

“Nafikiri ni vema na haki tumshukuru Mungu kwa maisha ya Philimon Sarungi,” amesema Lissu.

Lissu amesema hayo leo, Jumatatu, Machi 10, 2025, katika viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam, wakati wa kuaga mwili wa Profesa Sarungi, aliyefariki dunia Machi 5, 2025, jijini Dar es Salaam.

Tuwaenzi watu wakiwa hai

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ametoa wito kwa jamii kuzingatia kutoa heshima kwa watu wakiwa hai, badala ya kusubiri kifo cha mtu ndipo kuanza kutoa sifa na mapendekezo.

“Mzee huyu amefanya mambo mengi na amepata bahati ya kuishi miaka karibu 90. Kuna huu ushauri mwingi sana umetolewa hapa kumfafanua sana Mzee Sarungi, lakini inawezekana tumefanya makosa makubwa sana ya kuyaeleza haya yote baada ya kifo chake. Pengine enzi za uhai wake, angefurahi sana kuona hizi proposal zikibadili jina la MOI na kuwa kwenye jina lake,” amesema Chalamila.

Ameongeza: “Mimi kama Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, hata mimi sijawahi kufikiri, lakini hata ninyi mliopata bahati ya kumfahamu kazi zake nzuri sana, bado hamkuleta proposal hizi enzi za uhai wake, angefurahi sana. Sasa kuna tatizo kidogo la watu hawa wakishafariki, wakati fulani tunaweza kuongea mambo ya kweli, au wakati mwingine tunatafuta maneno ya kuweza kusema kwenye msiba. Ni muhimu, mkipata bahati ya kumfahamu mtu, yafanyeni yaliyo mema enzi za uhai wake, atakwenda akiwa amefarijika kwa kuwa ameenziwa,” amesema.

Mwili wa Profesa Sarungi utazikwa leo katika makaburi ya Kondo Kunduchi, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *