Lissu azungumzia ‘No reform, no election’ mbele ya wahariri

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu amesema lugha inayotumia chama hicho ya ‘No reform no election’ (hukuna mabadiliko, hakuna uchaguzi) imekuwa kali kwa sababu wanataka mfumo wa sasa wa uchaguzi ufanyiwe mabadiliko kwa madai sio rafiki kwa upinzani.

Lissu ameeleza hayo leo Jumapili Machi 2, 2025, wakati akizungumza kwenye kikao baina ya viongozi wakuu wa Chadema na wajumbe wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), kimechofanyika makao makuu ya chama hicho, Mikocheni jijini Dar es Salaam.

Kikao hicho kimelenga kupata tafsiri sahihi ya kampeni ya Chadema ya ‘No reforms no election,’ ikishinikiza Serikali ifanye maboresho ya mfumo wa uchaguzi kabla ya kuingia uchaguzi mkuu Oktoba 2025.

Amesema kampeni hiyo ilipitishwa na Kikao cha Kamati Kuu cha Desemba 2-3, 2024 chini ya uenyekiti wa Freeman Mbowe na kuungwa mkono na mkutano mkuu wa Januari 21, 2025 ambao nao uliongozwa na Mbowe.

Mkutano mkuu huo ndio ulimchagua Lissu kuwa mwenyekiti kwa kura 513 dhidi ya kura 482 alizopata Mbowe ambaye alikiongoza chama hicho kwa miaka 21.

Katika mkutano huo na wahariri, Lissu amesema kwa nyakati tofauti tume zilizoundwa na marais wastaafu, ikiwamo ya Jaji Francis Nyalali na Jaji Joseph Warioba ilipendekeza kuwepo kwa mabadiliko katika mfumo wa uchaguzi.

Amesisitiza Chadema haijasema itasusuia uchaguzi, bali itazuia uchaguzi, “hatujarembaremba hapo, tutawaalika Watanzania kuunganasi kupinga mabadiliko hayo.”

Hivi karibuni, viongozi waandamizi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) akiwamo Makamu Mwenyeiti Bara, Stephen Wasira alisema uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 utafanyika kama ulivyopangwa na wala hakuna chombo chochote cha Serikali kinachoweza kuukwamisha.

Mwanasiasa huyo alisema wanaosema pasipo mabadiliko haufanyika wanaota ndoto ya mchana huku akiwaomba Watanzania kuendelea kujiandaa na uchaguzi huo.

Wasira alieleza hayo Februari 11, 2025 katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza akisema licha ya msimamo wao huo wa Chadema, uchaguzi utafanyika  baada ya Tume Huru ya Uchaguzi kutangaza tarehe kama ilivyopewa mamlaka na Katiba ya nchi.

“Sis ni wadau wa uchaguzi, kazi yetu ni kuitumia dola kuleta mabadiliko ya watu, kwa hiyo hatuwezi kuambiwa hakuna uchaguzi. Wao kama wanataka kuingia kwenye uchaguzi bahati mbaya sisi tunawakaribisha maana uwezo wa kuwashinda tunao wanatusingizia CCM wanaiba tunaiba nini?

 “Sasa mimi nataka kuwaambia hakuna mtu mwenye mamlaka ya kuhairisha uchaguzi hakuna! Hakuna chombo chochote kiwe cha kiserikali au cha nani kinachoruhusiwa kuhairisha uchaguzi, ibara ya 41 sehemu ya nne ya Katiba inaipa tume mamlaka ya kutangaza tarehe ya uchaguzi na wakati utakapofika tume itatangaza tarehe ya uchaguzi,” amesema.

Mbali na Wasira, Rais Samia Suluhu Hassan akiwa ziarani Mkoa wa Tanga, aliwahamasisha wananchi kuendelea kujitokeza kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapigakura na wakati ukifika wa kupiga kura wajitokeze kwa wingi.