Dar es Salaam. Siyo rahisi kuzungumzia safari ya msanii Marioo kwenye muziki bila kulitaja jina la mwigizaji Eva Nchedange ‘Lissah Actress’ ambaye alikuwa ‘video queen’ kwenye video ya wimbo wa kwanza wa msanii huyo ‘Dar Kugumu’ uliotoka mwaka 2018.

Kama alivyovutia wengi kwenye video ya wimbo huo wa Marioo ndivyo alivyoendelea kuibua hisia za mashabiki katika wimbo wa Rapcha, ‘Lissa’ uliotoka miaka mitatu iliyopita.
Pengine kwa kipindi hicho watu hawakufahamu kama Lissa angekuja kuwa miongoni mwa waigizaji wataoipeperusha bendera ya Tanzania lakini kwa sasa safari yake ya mafanikio imebadilika na kuwashangaza wengi.

Mwigizaji huyo ambaye tayari ameonekana kwenye tamthilia kubwa mbili nchini Jua Kali na Jacob’s Daughters, wakati akizungumza na Mwananchi amesema alipenda sanaa tangu akiwa mwanafunzi.
“Wakati nasoma nilipenda sana kuigiza na kucheza ngoma ilianza taratibu baadaye nilikuwa natafuta njia yangu mwenyewe ya kufanya kwenye maisha nikaingia mazima kwenye kuigiza.

“Kabla ya kufanya tamthilia hizo kubwa nilifanya movie nyingi za kawaida zilikuwa zinaonekana lakini siyo sana. Baadaye nilifanikiwa kuonekana kwenye series ya Jua Kali ambayo ndiyo ilinitambulisha kwa watu wengi sana,”alisema.
Alisema mafanikio yake katika sanaa tangu ‘Dar Kugumu’ hadi sasa yanatokana na uvumilivu na kutambua anachokitaka
“Lazima ukipende kitu unachotaka kwa sababu kama unakipenda lazima utakipambania. Familia zetu nyingi zinakuwa hazisapoti mpaka waone, mwanzo walikuwa wanaona lakini hawakuwa wanaamini.
“Nilivyoamua kufanya sasa hivi wao ndio mashabiki wangu namba moja. Unajua sisi Wachaga kwetu ukienda lazima uulizwe unafanya shughuli gani mjini kwa hiyo mwanzoni nikisema msanii ilikuwa inawapa wasiwasi,”anasema.

Licha ya baadhi ya waigizaji kudai kuna aina ya uhusika hawawezi kuucheza hata wakitangaziwa dau nono. Kwa upande wa mwigizaji huyu anasema kwake ni tofauti.
“Naona nilipo nastahili kuwepo. Uhusika wowote nafanya, nafurahia sana uhusika tofauti ambao sijawahi kuucheza nyuma. Mimi nacheza uhusika wowote,”anasema Lissa.
Aidha kama wasemavyo wadau wa filamu nchini kuwa kiwanda hicho kimepitia mabadiliko makubwa ikiwemo kudondoka na sasa kuinukia kwenye uzalishaji wa tamthilia. Lissa anasema walipo sasa ni sehemu sahihi zaidi.
“Naona tunakwenda na dunia inavyoenda. Kwa hiyo kuna tofauti kubwa sana ya tulipotoka, hapa tulipo ni sehemu sahihi zaidi. Kutokana na dunia yenyewe inavyoenda.
“Miaka kumi au mitano iliyopita hatukuwa tunafanya vitu ambavyo tunafanya sasa hivi hata aina ya wasanii, waongozaji na stori hatukuwa nao kama tunavyofanya sasa,” anasema mwigizaji huyo.

Ili soko la filamu nchini liweze kukua zaidi na kuvuka mipaka Lissa anasema ni lazima sehemu za kuuzia kazi hizo ziongezeke kwani wasanii ni wengi na wanafanya kazi nzuri lakini vituo vya kununua kazi ndiyo vichache.
Hata hivyo, kwenye maisha ni lazima kuwa na plan b, umewahi kujiuliza usingekuwa huyo uliye leo pengine ungekuwa nani?. Kwa upande wa mwigizaji huyu anasema kiu yake kubwa ni kihudumia jamii.
“Nisingekuwa mwigizaji ningekuwa nesi napenda kuhudumia watu na kuwafanya wajisikie vizuri.
“Lakini katika kitu ambacho sikipendi ni kwenye watu wengi mtu ambaye simfahamu aniguse. Kuna bahati mbaya lakini kuna ile ya mtu anafanya makusudi sipendi.”
Utakumbuka Lissa anaitwa Eva kwenye kwenye tamthilia ya Jua Kali akiwa amebeba uhusika wa dada wa kazi ambaye anaishi na maambukizi ya virusi vya Ukimwi.