Lipumba alia na sera ya kukuza uchumi

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema kutokuwa na sera ya kukuza uchumi, ufisadi wa kutisha hasa kwenye miradi pamoja na ubinafsi ni sababu ya ajira kuendelea kuwa kizungumkuti kwa vijana wanaohitimu vyuo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili Machi 2, 2025 wakati akitoa mwelekeo wa CUF katika uchaguzi ujao, Profesa Lipumba amesema Serikali isichukulie utani na kuendelea kuwakatisha tamaa vijana kwa kuwa, kama hakutakuwa na mabadiliko kipindi cha sasa mbeleni wanakoelekea hali itakuwa mbaya zaidi. 

Hata hivyo, jana  Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alisema Serikali itaendelea kutoa ajira kwa wahitimu kila zinapopatikana katika sekta mbalimbali ikiwamo tasnia ya ualimu.

Msigwa alitoa kauli hiyo, kujibu kile kilichokuwa kimetokea Februari 21, 2025 walipoibuka viongozi wa Umoja wa Walimu wasiokuwa na ajira kuanzia mwaka 2015 hadi 2023 (Neto) na kutoa tamko mbele ya vyombo vya habari kuishinikiza Serikali kuwaajiri.

Hata hivyo, siku tatu baadaye viongozi wa umoja huo walitiwa mbaroni kwa nyakati tofauti na Jeshi la Polisi akiwamo mwenyekiti wao, Joseph Kaheza na katibu mkuu wao, Daniel Edgar kwa kile kilichodaiwa umoja wao hakuwa umesajiliwa kisheria.

Profesa Lipumba, amesema umaskini unaowakabili Watanzania hasa vijana ni wa kutengenezwa na suluhisho linaweza kupatikana iwapo Serikali itakuja na mipango yenye malengo ya kukuza uchumi unaozalisha ajira kwa wingi.

 “Hali ya maisha ya Watanzania inaendelea kuwa ngumu, vijana wengi hawana ajira wanabangaiza maisha kwa kufanya shughuli zisizokuwa na tija na kesho yao; hata wale wanaomaliza vyuo hawana hali nzuri,”amesema.

Profesa Lipumba amesema gharama za maisha zinaendelea kupanda licha ya Serikali kudai mfumuko wa bei ni asilimia nne pekee.

“Tanzania ipo kwenye orodha ya nchi zenye wastani wa nchi zenye uchumi wa kati wa chini, lakini kila Watanzania 100 kati yao 45 ni maskini  kwa kuzingatia kigezo cha kimataifa,” amesema Lipumba ambaye pia ni mtaalamu wa uchumi kitaaluma.

Amedai kuwa, Serikali imeshindwa kuja na sera ya kutumia utajiri wa rasilimali zilizopo nchini yakiwamo madini, gesi asilia, bahari na vivutio vya utalii kuendeleza Taifa.

Amesema idadi ya watu inaongezeka kwa asilimia 3.2 kila mwaka kama Watanzania wapo milioni 62, ikifika mwaka 2045 watakuwa watu 124 milioni ikiwa hakutakuwa na sera za kuongeza ajira na kuwapa mafunzo ya ujasiriamali, tatizo litakuwa kubwa zaidi.

Lipumba amesema takwimu za Taifa zinaonesha uwekezaji ni mkubwa kwa wastani wa asilimia 40 hadi 45 kwa miaka saba iliyopita huku akisema tafsiri ya kiuchumi ikifanyika, uwekezaji wa namna hiyo, uchumi unatakiwa kukua kwa asilimia 10 hadi 12.

“Tanzania kwa miaka yote hiyo uchumi umekua kwa asilimia tano, mfano wa wazi angalia foleni ya magari iliyopo Dar es Salaam wanachangamkia kujenga barabara ili wapate asilimia 10, lakini hakuna kuchangamkia barabara iishe mabasi yakubeba abiria yaanze kufanya kazi,” amesema Profesa Lipumba.

Amesema kila sehemu wanawaza kuchimba na hakuna barabara inayokamilika ili mabasi yaanze kutoa huduma, matokeo yake takwimu zinaonyesha uwekezaji ni mkubwa lakini ukuaji wa uchumi hauonekani.

Profesa Lipumba amedai kuwa, ni muhimu kwa Serikali kutumia fursa ya  Jiografia ya Tanzania ya kuzungukwa na nchi ambazo hazina bandari ili zichochee ukuajia wa ajira viwandani lakini pia kuongeza thamani katika madini.

“Uwepo wa madini ya Graphite, Nickel, Cobalt, Lithium, Copper na kupakana na nchi ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo (DRC) yenye madini mengi, uvutie uwekezaji katika viwanda vya betri na magari ya umeme,” amesema Profesa Lipumba.

Amesema asilimia 10 ya madini ya Graphite ulimwenguni yanapatikana Tanzania kule Ruangwa mkoani Lindi lakini pia kuna gesi iliyoanza kugunduliwa tangu mwaka 2000 ambao hadi sasa haujaanza.

“Gesi iliyogunduliwa ni zaidi ya futi za ujazo 45 trilioni hadi sasa bado haijaanza kutumiwa tatizo ni kutokuwa na sera ya kukuza uchumi na kuongeza ajira,” amesema Profesa Lipumba.

Akitayafafanua masuala yote kupitia ilani yao ya uchaguzi, amesema: “Maandalizi ya ilani inayoendelea kufanyika ya uchaguzi mkuu mwaka huu, yanatumia akili mnemba kutathimini matatizo yanayoikabili jamii kiuchumi na kuangalia uzoefu wa nchi zingine duniani zilizofanikiwa.”