Lina Tour sasa kuanzia Moro

RAUNDI ya kwanza ya michuano ya Lina Tour kwa mwaka huu inatarajiwa  kufanyika katika viwanja vya Gymkhana, mjini Morogoro na si Arusha kama ilivyotangazwa awali.

Kabla ya mabadiliko haya, raundi ya kwanza ya Lina Tour ilipangwa kuanza Februari 20 hadi 23, katika viwanja vya Arusha Gymkhana na sasa raundi ya kwanza itaanza Februari 27 hadi Machi 2, katika viwanja vya Gymkhana mjini Morogoro na yamepewa jina la Lina Professional and Amateur Golf (Pro-AM) Tour.

Mashindano haya ni maalumu kwa ajili ya kumuenzi mlezi wa gofu ya wanawake nchini Lina Nkya aliyekuwa mchezaji na kiongozi wa Chama cha Gofu ya wanawake nchini na alifariki dunia Januari 19, mwaka 2021 mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Lina Tour, Yasmin Challi alisema waandaji wa michuano hiyo ya pekee inayotoa zawadi ya fedha taslimu kwa wacheza gofu ya kulipwa na ridhaa, wamethibitisha Morogoro Gymkhana, ambao walikuwa wenyeji wa raundi ya pili mwaka jana na ndiyo watakaofungua msimu mwaka huu kwa mchezo wa siku nne ukihusisha mashimo 72.

“Tunapenda kuwaarifu wachezaji na wadau wa gofu kuhusu mabadiliko ya tarehe na viwanja vitakavyofungua michuano ya Lina Tour kwa mwaka huu. Mbadiliko haya yanalenga kuyapa mashindano ubora zaidi,” alisema Challi na kuwataka wachezaji kuendelea kujisajili kwani zoezi hilo linaendelea vizuri hadi Februari 20 kwa wachezaji wote wa kulipwa na ridhaa.

“Tuomba radhi kwa mabadiliko haya na tungependa kuwaona tena wote mkishiriki katika mashindano ya ufunguzi mjini morogoro,” alisema Challi.

Michuano hii ambayo ilianza rasmi mwaka jana, inaandaliwa na familia ya Said Nkya ikishirikiana na Chama cha Gofu ya Wanawake nchini (TLGU), Chama Gofu ya Kulipwa nchini (TPGA) pamoja na Penda Golf Tanzania.