Ligi yetu inadhalilishwa, mashabiki hawaheshimiwi

Mei 8, 2021 na Machi 8, 2025 ni tarehe ambazo zimeacha doa kubwa katika historia ya soka la Tanzania na bila shaka zimewaghadhabisha wapenzi wa soka nchini.

 Hizi ni siku mbili tofauti lakini zinafanana kwa jambo moja ambalo ni mechi kubwa ya ligi, maarufu kama “Dabi,” kuahirishwa kwa sababu zinazozuilika na wakati mwingine zisizo na mantiki yoyote.

 Ni aibu kwa soka letu kuona tukio hili likijirudia bila hatua madhubuti kuchukuliwa na tusipokuwa makini utakuwa ni utamaduni.

 Katika matukio yote mawili, mechi hizi ziliahirishwa baada ya moja ya timu kususia mchezo. Ni jambo la kushangaza kwamba, licha ya sheria na kanuni za ligi, Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), Afrika (CAF), na Dunia (FIFA) kuwepo, bado hakuna hatua kali zinazochukuliwa ili kukomesha tabia hii.

 Ni jambo lisiloeleweka kwamba Simba na Yanga, vilabu viwili vikubwa nchini, vinaweza kufanya maamuzi ya kiholela bila kuzingatia athari zake kwa mashabiki, wadhamini na uchumi wa soka kwa ujumla.

Mashabiki ni sehemu muhimu ya mchezo wa soko kama ilivyo kwa michezo mingi. Wengine wanasafiri kutoka mikoa mbalimbali, wengine kutoka nje ya nchi, huku wakitumia fedha na muda wao kuhudhuria mechi hizi.

 Fikiri mtu ametoka Kigoma, Tarime au nchi za nje huko kuja kushuhudia watani wa jadi, ameshaingia mpaka uwanjani halafu saa chache unamwambia mechi imeahirishwa itapangiwa tarehe nyingine.

Je, ni nani anawafikiria wanapofika uwanjani na kisha kukosa burudani waliyoitarajia? Hasara wanayoipata mashabiki hawa ni kubwa mno, na hakuna yeyote anayewajibika kwa hilo sanasana utasikia njoo na tiketi yako ileile utaingia wanasahau kuwa gharama ni zaidi ya tiketi.

 Si hilo tu, mechi hizi zinapo ahirishwa, gharama za maandalizi zinazopotea ni nyingi kutoka kwa waandaaji wa mechi, hoteli, wauzaji wa bidhaa viwanjani, na hata matangazo ya televisheni ambayo huandaliwa kwa ajili ya mashindano haya.

 Kiuchumi, ni sawa na kuchana pesa. Fikiri kuhusu aliyelipia kifurushi mapema ili kuiona mechi au watu kama Azam Tv na TBC Taifa ambao pengine wamefanya maandalizi ya kurusha mechi hiyo kwa muda, bila shaka wanapoteza pesha inapotokea jambo kama hilo.

Ligi Kuu ya Tanzania imepiga hatua kubwa, hadi kufikia kuwa ligi ya nne kwa ubora barani Afrika. Hili ni jambo la kujivunia, lakini linaweza kupoteza maana kama utovu huu wa nidhamu utaendelea.

 Vilabu hivi viwili, vinavyobeba historia na hadhi kubwa, vina wajibu wa kuonesha ukomavu na kuheshimu mchezo huu, siyo tu kwa faida yao binafsi, bali kwa maendeleo ya ligi nzima.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) lina wajibu wa kuhakikisha sheria zinatekelezwa kwa haki na kwa usawa. Uoga wa kuchukua hatua kali dhidi ya Simba na Yanga unaweza kuja kuigharimu ligi siku moja.

 Je, klabu ndogo zikifanya vitendo hivi zitachekewa? kwa nini vigogo wa soka waendelee kufumbiwa macho? Kukiwa na hatua madhubuti dhidi ya timu hizi, tabia ya kususia mechi itaisha mara moja.

 Hakuna klabu kubwa kuliko mchezo wenyewe. Pamoja na hilo, mashabiki wanapaswa pia kuwa na sauti katika suala hili.

Ni wakati wa wao kudai haki yao ya kupata burudani wanayoistahili kwa gharama wanazotumia. Vyombo vya habari, wanaharakati wa soka, na wadau wote wa michezo wanapaswa kushinikiza mabadiliko ili kuhakikisha matukio haya hayatokei tena.

 Hali hii ikiendelea, inaweza kupunguza mvuto wa ligi na kupunguza uwekezaji wa wadhamini ambao wanategemea hadhi ya ligi kuwa ya kuaminika.

Huu ni wakati wa TFF kufungua macho na kuweka mikakati ya kuhakikisha matukio kama haya hayatokei tena. Kama itahitaji kupunguza alama, faini kubwa, au hata kuzifungia timu zinazokiuka sheria, basi hatua hizo zichukuliwe. 

Mashabiki wanahitaji kuona uongozi wenye uthabiti na si wa kufuata mkumbo. Kama hatua kali zitachukuliwa kwa kigogo mmoja wapo, basi wengine watajifunza.

Ni wakati wa kuonyesha kuwa soka letu si la kiholela. Vilabu lazima viwajibike, mashabiki waheshimiwe, na ligi yetu iwe mfano wa kuigwa barani Afrika.

 Hii ni fursa ya kubadilisha mfumo wa usimamizi wa soka ili kuleta uwajibikaji wa kweli. Hatua zisipochukuliwa sasa, soka letu litaendelea kuwa la mazoea na si la ushindani wa kweli.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *