
WAKATI timu zikisubiri kutangaziwa tarehe ya kuanza mashindano ya Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), klabu 11 kati ya timu 16 zinazoshiriki ndizo zilizoanza mazoezi kujiandaa na kipute hicho kinachotarajiwa kuwa na mvuto wa aina yake.
Mwanaspoti limetembelea katika viwanja vya timu hizo na kuzishuhudia 11 zikiwa na vikosi vyenye nyota kadhaa zikijifua kwa ajili ya maandalizi ya ligi hiyo ambayo katika miaka ya karibuni imeanza kurejea katika ubora iliokuwa nao miaka ya 1990 hadi 2000.
Timu zilizoanza maandalizi ni JKT inayofanyia katika Uwanja wa Mgulani, ABC (Twalipo), Mchenga Stars (Spide), Kampala International University (KIUT), Pazi (Tanesco) na UDM Outsiders (Chuo Kikuu cha Dar es Saalam).
Zingine ni Dar City (Oysterbay), Polisi (Bandari), Stein Warriors (TPDC), Kurasini Heat (Bandari) na Mgulani (JKT).
Timu ambazo hadi jana zilikuwa hazijaanza ni Srelio, Vijana ‘City Bulls’ inayotumia Uwanja wa Zanaki, Savio (Upanga), DB Oratory (Oysterbay) na Chui (Makongo).
Mkurugenzi wa Ufundi wa Mchenga Stars, Mohamed Yusuph alisema timu hiyo itakuwa inafanya mazoezi usiku katika Uwanja wa Spide kuhakikisha kwamba inafanya vizuri katika mashindano hayo.
“Tumeamua tufanye mazoezi usiku kwa ajili ya kuwapumzisha wachezaji waliofunga kwenda kufuturu,” alisema Yusuph na kwamba idadi ya walioripoti ni wachache.
“Naamini mazoezi yatakavyokuwa yakiendelea idadi ya wachezaji wa timu itaongezeka.”
Aliwataja baadhi ya wachezaji walioanza mazoezi kuwa pamoja na mchezaji bora wa BDL msimu uliopita, Amin Mkosa na Alex Bwana.
MNYAMOKO ATAMBA
Kocha msaidizi wa Srelio, Miyasi Mnyamoko amesema bado hawajaanza maandalizi ya BDL, lakini watashangaza wengi mwaka huu.
Alisema kushangaza kwao kutatokana na wachezaji walio nje ya nchi watapokuwa wamejiunga na timu hiyo mapema na kutaifanya iimarike zaidi, akiwataja miongoni mwao kuwa ni Sponcian Ngoma, Joseph Kamamba (Zambia) na Charles Kaseeng (Cameroun).
“Ubora wa wachezaji hao ulichangia timu kucheza robo fainali mwaka jana,” alisema Mnyamoko.
Katika Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam mwaka jana timu hiyo ilitolewa na Dar City katika robo fainali kwa michezo 3-1. Srelio ilimaliza mzunguko wa pili ikishika nafasi ya nane kwa pointi 44.