
ZIKIWA zimesalia mechi nne kumalizaka kwa msimu wa 2024/25 kwa Ligi Kuu ya Wanawake kuna vita mbili kwenye ligi hiyo za kuwania nafasi.
Katika msimamo wa ligi hiyo, JKT Queens iko kileleni na pointi 38, tofauti ya pointi moja na Simba Queens ya pili na pointi 37, Yanga Princess ya tatu na pointi 30.
Vita iliyopo ni kuwania nafasi ya tano kati ya Ceasiaa yenye pointi 16 na Alliance Girls ya sita yenye 15, huku Ceasiaa imecheza mechi 13 ikiwa na mchezo mmoja mkononi wakati Alliance imecheza zote 14.
Ceasiaa imeshinda mechi tano, sare moja na kupoteza saba, ikiruhusu mabao 31 na kufunga mabao 20, huku Alliance ikishinda nne, sare tatu na kupoteza pia saba na imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara 27 na kufunga mabao 17.
Wakati timu hizo zikiwa kwenye vita ya tano bora, kuna ile ya kushuka zinazozihusu Bunda Queens iliyopo nafasi ya nane na pointi tisa ikibakiza viporo vitatu baada ya kucheza michezo 11 ili kufikia michezo 14 na Gets Program ya tisa na pointi tisa pia na kiporo kimoja baada ya kucheza michezo 13.
Timu hizi mojawapo inaweza kuungana na Mlandizi mwisho wa msimu kushuka daraja ili kuzipa nafasi timu mbili kupanda Ligi Kuu.
Mlandizi Queens tayari imeshuka hadi Ligi Daraja la Kwanza ilipotoka msimu uliopita baada ya kuambulia alama moja kwenye mechi 13, ikiwa timu pekee iliyoruhusu mabao mengi 68.