KENGOLD bado inajitafuta baada ya kurejea katika duru la pili ikiwa imefanya usajili wa kibabe dirisha dogo la usajili lililofungwa katikati ya mwezi uliopita.
KMC nayo imekuwa na mwenendo wa kusuasua kwani katika mechi tano zilizopita za Ligi Kuu Bara imeshinda moja tu.
Sasa timu hizo jioni ya leo zitashuka uwanjani kuumana katika muendelezo wa ligi, huku kila mmoja ikizipigia hesabu pointi tatu, ili kujiweka pazuri katika msimamo.
Utamu wa mchezo huo utakaopigwa kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya ni kuzikutanisha timu zilizotoka kufuingwa mabao 6-1 hivi karibuni na watetezi wanaoongoza pia msimamo wa ligi hiyo, Yanga zote ndani ya mwezi huu wa Februari.
KenGold ndio iliyokuwa ya kwanza kufumuliwa 6-1 na Yanga katia mechi iliyopigwa Februari 5 kabla ya KMC nao kupokea kipigio kama hicho Siku ya Valentine yaani Februari 14.
Mechi hiyo ya jijini Mbeya ni moja kati ya michezo miwili inayopigwa leo, ikiwamo ile ya Dodoma Jiji itakayokuwa wenyeji wa Fountain Gate, timu ambayo haijaonja ushindi tangu mwaka huu uingie, lakini ikiwa imekuwa wepesi wa kuruhusu mabao katika mechi ilizocheza.

KenGold itakuwa wenyeji wa KMC kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya huku wenyeji hao wakiwa na matokeo ya kuvuna pointi saba katika mechi tatu zilizopita, ikiwamo kushinda mchezo uliopita dhidi ya Kagera Sugar. KenGold iliifunga pia Fountain na kutoka sare na Tabora United ikiwa ugenini.
Ikiwa na mastaa kama Obrey Chirwa aliyeifungia bao moja hadi sasa tangu ajiunge nayo, Seleman Rashid ‘Bwenzi’ aliyeanza na moto kwa kufunga mabao matatu katika mechi nne zilizopita sambamba na wengine wenyeji wanapewa nafasi kubwa ya kuchomoza na ushindi mbele ya KMC.
Hii ni namna timu hiyo ilivyorudi katika ligi hiyo ikiwa kivingine kwani hadi duru la kwanza linaisha ilikuwa imevuna pointi sita tu katika mechi 15, lakini hivi sasa imeshafikisha alama 13 na kama itatoka na ushindi katika mechi hiyo ya 21 kwa msimu huu itajiongezea pointi zitakazoendelea kuiweka pazuri.
KenGold inayonolewa na kocha Mserbia Vladislav Heric ilikuwa inasikilizia Kagera Sugar iliyokuwa uwanjani jana, kwani kama imepasuka basi wenyewe wakishinda mbele ya KMC itawatoa mkiani baada ya kukaa hapo kwa muda mrefu tangu ipande daraja msimu huu sambamba na Pamba Jiji.
Hata hivyo, licha ya kuwa na mwenendo nzuri tangu duru la pili lianze kulinganisha na wapinzani wao, lakini KenGold haipaswi kuwachukulia poa KMC, kwani katika mchezo wa duru la kwanza uliopigwa KMC Complex, ilipasuka bao 1-0, lakini Vijana wa Kinondoni hawatabiriki.
Ikiwa imetoka kupoteza nyumbani kwa mabao 2-0 mbele y JKT Tanzania ni wazi KMC itapenda kupata ushindi ugenini ili kuendeleza ubabe kwa wenyeji wao, lakini kujiweka pazuri katika mechi hizi za lala salama.
Katika mechi tano zilizopita, KMC imeonja ushindi mara moja tu dhidi ya Singida Black Stars, huku ikipoteza michezo mitatu na moja tu iliambulia sare, huku ikiruhusu jumla ya mabao 11 na kufunga manne tu, wakati KenGold katika mechi tano kama hizo, imeshinda mbili vipigo viwili na sare moja.
KenGold katika mechi hizo tano imefunga jumla ya mabao matano tu, lakini ikifungwa tisa, ikiwa na maana kama itajilegeza kwa KMC huenda ikaongeza idadi ya mabao iliyoruhusu kutokana na aina ya wachezaji wa wapinzani wao walivyo na kasi hasa Redatius Mussa, Daruwesh Saliboko, Oscar Paul, Idd Shaaban Chilunda na mabeki wa pembeni akiwamo Raheem Shomary na Hance Masoud.

Hata hivyo, washambuliaji wa KMC watakuwa na kazi mbele ya ukuta mgumu wa KenGold utakaokuwa chini ya mkongwe, Kelvin Yondani akishirikiana na Zawadi Mauya, japo timu hiyo itaendelea kumkosa Bernard Morrison ambaye tangu asajiliwe na kutambulishwa hajawahi kuitumikia katika Ligi Kuu ikielezwa bado hayupo fiti tangu alipoumia wakati akiwa FAR Rabat Morocco.
Makocha wa timu hizo, Kally Ongala wa KMC na kocha msaidizi wa KenGold, Omary Kapilima kila mmoja amejinasibu wanauchukulia mchezo huo kwa uzito mkubwa na wamejiandaa kutoka na ushindi wa pointi tatu ili kujiwekea hazina katika ngwe hii ya lala salama.
DODOMA JIJI v FOUNTAIN GATE
Katika mechi nyingine itakayopigwa saa 1:00 usiku, wenyeji Dodoma Jiji wakatakuwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, kuikaribisha Fountain Gate ya kocha Robert Matano anayesaka ushindi wa kwanza katika Ligi Kuu Bara tangu alipoajiriwa na kikosi hicho kiliambulia pointi mbili tu katika mechi tano zilizopita.
Dodoma ikaikaribisha Fountain ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 3-2 katika mechi iliyopita uwanjani hapo dhidi ya Tanzania Prisons na itaendelea kuwategemea Paul Peter ambaye ndiye kinara wa mabao wa timu hiyo akiwa na sita hadi sasa.
Timu hizo zimetofautiana pointi moja tu kwa sasa, Dodoma ikiwa nafasi ya tisa na pointi 23 kupituia mechi 19, wakati Fountain imecheza mechi 20 ikivuna pointi 22 na ipo nafasi ya 10 na matokeo yoyote ya ushindi kwa timu moja yao iitakuwa na maana na kujiongezea hazina na kuondoka eneo iliyopo sasa.

Katika mchezo wa kwanza msimu huu uliopigwa Septemba 9 mwaka jana zilitoka sare ya mabao 2-2, lakini rekodi zinaonyesha Fountain tangu ikiwa Singida Fountain Gate haijawahi kupoteza mchezo wowote tangu ilipopanda mwaka 2022, kwani imeshinda mechi tatu na zilizosalia mbili ziliisha kwa sare.
Hii ikiwa na maana mchezo wa leo Dodoma itakuwa na kazi ya kutaka kujivua unyonge mbele ya wageni wao, lakini ikitaka pia kuendeleza wimbi la ushindi baada ya kushinda mechi iliyopita.
Katika mechi tano zilizopita za Dodoma, timu hiyo imeshinda mbili na kupoteza mbili na kutoka sare moja, wakati wapinzani wao wamepata sare mbili tu katika mechi tano zilizopita na kupoteza tatu, lakini ikiwa ndiyo timu inayoongoza kwa kuruhusu mabao mengi kifungwa 38 katika mechi 20.
Ni mechi mbili tu pekee ambazo Fountain kwa msimu huu ilicheza bila kuruhusu bao kutinga nyavuni mwa lango lao, ni siku ilipoilaza Namungo 2-0 na mchezop wa mwisho ilipotoka suluhu na Tabiora United, lakini zilizosalia zote 18 zilizosalia imekuwa ikiruhusu walau bao moja na kuendelea.

Hivyo kwa leo ni wazi kocha Matano ataingia na mbinu ya kudhibiti rekodi hiyo mbaya kama ilivyofanya katika mchezo uliopita dhidi ya Tabora, lakini akiwategemea washambuliaji wake Edger Williams, Salum Kihimbwa, Mukono Edinho na Dickson Ambundo kutupia nyavuni kupata ushindi.
Kocha wa Dodoma Jiji, Mecky Maxime alikaririwa mapema kwake kila mechi kwa zilizosalia ni fainali kutokana na tofauti ndogo ya pointi zilizopo baina ya timu moja hadi nyingine kuanzia zilizopo chini ya Tano Bora.
Maxime alisema anajua kufanya kosa lolote na kuruhusu kufungwa ni kujiweka pabaya na kutoa mwanya kwa wapinzani kuwaacha kipointi na ubaya ni hizi ni mechi za lala salama zinazoamua hatma ya ubingwa na kusalia na za kushuka daraja au kucheza play-off ya kuepuka kushuka daraja.
Matano kwa upande wake alisema anaamini wachezaji wameanza kumzingatia baada ya awali kupata ugumu kwa vile ni kocha mpya kikosini, lakini akikiri Ligi Kuu Bara ni ngumu na isiyotabirika hivyo kila mchezo anauchukulia kwa uzito mkubwa kwa ajili ya kuiweka timu sehemu salama.