
Dar es Salaam. Ligi Kuu ya NBC msimu huu wa 2024/2025 imesimama kupisha mapumziko ya kupisha kalenda ya mechi za timu za taifa ambapo kwa hapa Afrika kutakuwa na mechi za kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025.
Hadi inasimama, kuna timu ambazo zilikuwa zimeshaanza kucheza mechi za raundi ya 11 huku nyingi zikiwa zimecheza raundi 10.
Yapo mambo kadhaa ya kuvutia ambayo yamejitokeza katika theluthi ya kwanza ya Ligi Kuu msimu huu ambayo pengine yatafanya ushindani uongezeke pindi itakapoendelea tena.
KMC Complex, Tanzanite nyumba za mabao
Viwanja 15 tofauti vimetumika kwa mechi 82 zilizochezwa kwenye Ligi Kuu hadi hivi sasa ambapo vipo vinavyotumika na timu mbili, kuna vilivyotumiwa na timu tatu na vingi vinatumiwa na timu moja moja kwa mechi zao za nyumbani.
Viwanja hivyo 15 ambavyo vimetumika katika theluthi ya kwanza ya Ligi Kuu ya NBC ni Benjamin Mkapa, KMC Complex, Azam Complex na Meja Jenerali Isamuhyo vilivyopo Dar es Salaam, Sheikh Amri Abeid (Arusha), Tanzanite Kwaraa (Manyara), Jamhuri (Dodoma), Kaitaba (Kagera), Liti (Singida) na Majaliwa (Lindi).
Vingine ni Sokoine (Mbeya), CCM Kirumba (Mwanza), New Amaan Complex (Zanzibar), Lake Tanganyika (Kigoma) na Ali Hassan Mwinyi (Tabora).
Uwanja ambao idadi kubwa ya mabao imefungwa ni KMC Complex uliopo Mwenge, Dar es Salaam ambapo katika mechi 11 zilizochezwa hapo, mabao 28 yamefungwa ukifuatiwa na uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati ambao nyavu zake zimetikiswa mara 24 katika mechi saba huku nafasi ya tatu ikishikwa na Uwanja wa Sokoine Mbeya ambao mabao 24 yamefungwa hapo katika mechi 11.
Uwanja wenye wastani mzuri wa mabao kwa mechi ni Tanzanite Kwaraa ambao kwa wastani, kila mechi kunafungwa mabao 3.4 ukifuatiwa na Uwanja wa KMC Complex ambao una wastani wa kushuhudiwa mabao 2.5 kwa mechi.
Benjamin Mkapa ndio Uwanja ambao una mabao machache zaidi hadi sasa ambapo umeruhusu bao moja tu msimu huu.
Simba nyumbani, Yanga ugenini
Vinara wa ligi hiyo kwa sasa, Simba ndio timu ambayo imeonekana kuutumia vyema uwanja wa nyumbani kulinganisha na nyinginezo ambapo katika mechi sita ilizocheza nyumbani, imekusanya pointi 13 ikipata ushindi mara nne, kutoka sare moja na kupoteza moja.
Singida Black inafuatia kwa kuvuna idadi kubwa ya pointi nyumbani ambapo katika mechi sita, imepata pointi 11, ikipata ushindi mara tatu, kutoka sare mbili na kupoteza mchezo mmoja.
Kengold ndio timu iliyokusanya pointi chache zaidi nyumbani ambapo katika mechi tano ilizocheza kwenye Uwanja wa Sokoine, imepata pointi nne tu.
Mbabe wa ugenini ni Yanga ambayo imepata ushindi katika mechi zote tano iliyocheza hadi sasa, ikikusanya pointi 15, ikifuatiwa na Azam FC ambayo imevuna pointi 14 katika mechi sita za ugenini.
Kengold ndio kibonde zaidi kwa mechi za ugenini kwani haijapata ushindi wowowte katika mechi sita na juu yao ipo Kagera Sugar, iliyopata pointi moja tu katika mechi zake tanio za ugenini.
Wakali wa nyavuKuna kundi la wachezaji 13 ambao kila mmoja amefunga mabao matatu au zaidi na idadi kubwa ya wachezaji wamefunga mabao mawili au moja hadi sasa.
Wachezaji hao 13 wanaongozwa na kinara wa kufumania nyavu, Seleman Mwalimu wa Fountain Gate ambaye ameshapachika mabao sita akifuatiwa na Charles Ahoua wa Simba mwenye mabao matano sawa na William Edgar wa Fountain Gate.
Ambao wamefunga mabao manne ni Paul Peter (Dodoma Jiji), Peter Lwasa (Kagera Sugar) huku waliofumanua nyavu mara tatu kila mmoja wakiwa ni Offen Chikola (Tabora United), Saadun Nassor (Azam), Joshua Ibrahim (KenGold), Salum Kihimbwa (Fountain Gate), Mabad Maabad (Coastal Union), Maxi Nzengeli (Yanga), Elvis Rupia na Marouf Tchakei (Singida Black Stars).
Nuksi ya makocha
Idadi ya makocha saba wameshindwa hata kufika angalau theluthi moja ya msimu huu baada ya kuachana na timu zao kwa sababu mbali.
David Ouma alikuwa kocha wa kwanza kupewa mkono wa kwaheri baada ya waajiri wake Coastal Union kuamua kuachana naye kabla ya mechi za Ligi Kuu msimu huu kuanza ambaye amefuatiwa na makocha wengine sita.
Makocha wengine ambao baadhi wameonyeshwa mlango wa kutokea na timu zao kwenye mabao ni Youssouf Dabo (Azam FC), Fikiri Elias ((Simba), Paul Nkata (Kagera Sugar), Goran Kopunovic (Pamba), Mwinyi Zahera (Namungo) na Francis Kimanzi (Tabora United).
Kadi nyekundu zatishia
Idadi ya kadi nyekundu sita zimetolewa hadi sasa ambapo nyingi kati ya hizo ni za moja kwa moja kutokana na makosa ya faulo au utovu wa nidhamu.
Idadi kubwa ya kadi nyekundu hadi sasa zimeonyeshwa katika Uwanja wa huo unaomilikiwa na Azam FC huku viwanja vingi vikiwa havijashuhudia kadi nyekundu hadi sasa.
Kadi nyekundu nne zimetolewa katika Uwanja wa Azam Complex na kadi nyekundu mboja imetolewa katika Uwanja wa Kwaraa uliopo Babati.
Kadi nyekundu ya kwanza kutoka kwenye Uwanja wa Azam Complex ilikuwa ni Septemba 14 ambayo ilionyeshwa kwa Cheick Sidibe wa Azam FC aliyemfanyia faulo Salehe Masoud na mwamuzi aliyetoa kadi hiyo alikuwa ni Tatu Malogo.
Kadi ya pili kutolewa katika Uwanja huo ilikuwa ni ya Salehe Masoud huyohuyo wa Pamba aliyoipata Oktoba 3 dhidi ya Yanga kutoka kwa refa Sady Mrope baada ya kumfanyia faulo Chadrack Boka.
Oktoba 22, kipa Denis Richard wa JKT Tanzania alionyeshwa kadi nyekundu kwenye Uwanja wa huo wa Azam Complex na refa Ahmed Arajiga baada ya kufanya kosa la kugusa mpira kwa mikono nje ya eneo la hatari na kuzuia nafasi ya wazi ya bao ya Yanga.
Juzi, Refa Arajiga alimuonyesha kadi nyekundu Ibrahim Hamad ‘Bacca’ wa Yanga katika mchezo dhidi ya Azam FC, baada ya beki huyo kumchezea rafu, Nasso Saadun aliyekuwa akielekea kufunga.
Ukiondoa kadi hizo nne ambazo zimetolewa katika Uwanja wa Azam Complex, kadi nyekundu zilizotolewa katika Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati ni ya kiungo mshambuliaji wa KMC, Ibrahim Elias na ya kiungo wa Fountain Gate, Abalkasim Seleman.