
KUNA uhondo wa mechi nne za Ligi Kuu Bara Jumapili hii ambapo zimekaa kimtego kweli, huku kila timu ikipiga hesabu kali kinoma.
Kwa namna ambavyo muda wa mechi hizo ulivyowekwa, huna haja ya kugusa rimoti kubadilisha chaneli kwani ukianza kuangalia ile ya saa 8:00 mchana ambayo Tanzania Prisons itaikaribisha Kagera Sugar, hautabanduka hadi saa 3:00 usiku Namungo itakapokuwa mwenyeji wa KMC.
Mechi hizo nne zimepangiliwa vizuri muda wake ambapo haziingiliani, ikiisha moja inafuatia nyingine hadi zote zinakamilika kwa kukata kiu yako.
TZ PRISONS V KAGERA SUGAR
Wenyeji Tanzania Prisons watakuwa na kibarua kigumu kuvunja rekodi ya Kagera Sugar ambayo haijawahi kupoteza mchezo wowote kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya kuanzia saa 8:00 mchana.
Tanzania Prisons itaikaribisha Kagera Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu Bara raundi ya 25 ikiwa kila timu inahitaji ushindi ili kujinasua nafasi za chini kwenye msimamo wa ligi hiyo.
Katika michezo 24 zilizochezwa kwa timu hizo kila moja, Kagera Sugar imekusanya pointi 22 ikiwa nafasi ya 12, huku Tanzania Prisons nafasi ya 14 kwa pointi 18 na kufanya mechi hiyo kuwa na vita ya namba kukwepa kushuka daraja.
Kagera Sugar chini ya kocha mpya, Juma Kaseja imeonekana kuwa na mwenendo mzuri kwani katika mechi nne alizoongoza zikiwamo mbili za Kombe la Shirikisho (FA) na zingine Ligi Kuu Bara wameshinda zote.
Kaseja aliyewahi kutamba na timu kadhaa akicheza langoni ikiwamo Simba, Yanga na Kagera Sugar, alianza kwa kishindo dhidi ya Namungo kwa kuichapa mabao 3-0 katika Kombe la FA, kisha akaibonda Pamba Jiji mabao 2-1 (ligi Kuu), akaiondoa Tabora United kwa penalti 5-4 baada ya sare ya 1-1 (Kombe la FA) na kuilaza Coastal Union 2-1 kwenye ligi.
Tangu Kagera Sugar ianze kucheza mechi Ligi Kuu katika Uwanja wa Sokoine, matokeo magumu kwao ni sare huku zaidi ikiwa ni ushindi kwa timu za mkoani Mbeya.
Tanzania Prisons chini ya Kocha Aman Josiah katika michezo minane ya ligi aliyoiongoza hadi sasa imeshinda mmoja, sare mmoja na kupoteza sita timu hiyo ikiwa katika nafasi ya 14 kwa alama 19. Mechi alizoongoza ni dhidi ya Mashujaa aliyoshinda 2-1, na sare ikiwa 1-1 dhidi ya Tabora United huku akipoteza mbele ya Simba (3-0), Namungo (1-0), Dodoma Jiji (3-2), Fountain Gate (1-0), Azam (4-0) na KMC (3-2).
Pia alipoteza mbele ya Bigman kwa penalti 3-1 baada ya sare ya 1-1 kwenye Kombe la FA ikifanya jumla ya michezo tisa ya michuano tofauti.
Kocha Msaidizi wa Kagera Sugar, Themi Felix amesema mechi hii si ya ufundi sana bali ni nguvu zitakazotumika zaidi kutafuta pointi tatu kutokana na mahitaji ya kila upande.
Amesema wamejipanga kuendeleza ushindi ili kujinasua nafasi za mwisho akieleza kuwa wanafahamu ugumu wa mechi hiyo kutokana na wapinzani namna walivyo.
“Vijana wote wako fiti kwa mchezo huo, tunajua ugumu na umuhimu wake kwakuwa hatutofautiani sana na wapinzani hivyo kikubwa itatumika nguvu sana badala ya ufundi,” amesema Felix.
Nyota wa timu hiyo, Godfrey Manyasi amesema kwa sasa mechi zilizobaki ni vita kali katika kutafuta ushindi na kujiweka nafasi nzuri hadi mwisho wa msimu.
“Tutawaheshimu wapinzani kwakuwa tunajua uhitaji wao, hawako sehemu nzuri sawa na sisi, hivyo tutaenda kwa mipango ileile kama michezo mingine iliyopita,” amesema Manyasi.
Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Aman Josiah amesema pamoja na matokeo mabovu waliyopata mechi zilizopita, lakini si kwa ubovu wa kiwango cha wachezaji bali ‘timu ya tatu’ ilivyoamua iwe.
“Wachezaji wako tayari kwa mechi hiyo, tumepoteza mechi za nyuma ikiwamo KMC na Fountain Gate lakini si kwa kiwango duni cha vijana bali timu ya tatu ilivyoamua, hilo halituumizi sana bali tunajipanga kwa kesho tushinde,” amesema Josiah.
Tanzania Prisons inashuka uwanjani huku ikitarajiwa vigogo wa juu wa timu hiyo kushuhudia mechi hiyo huku ikiwa ni mkakati wa kushinda mechi zilizobaki kukwepa kushuka daraja baada ya kikao kizito cha usiku wa kuamkia Aprili 5 mwaka huu kilichoshirikisha wadau mbalimbali.
SINGIDA BS V AZAM
Saa 10:15 jioni ikiwa ni muda mchache baada ya kumalizika kwa mechi ya Tanzania Prisons dhidi ya Kagera Sugar, wenyeji Singida Black Stars wataikaribisha Azam kwenye Dimba la Liti mkoani Singida.
Mchezo huu unazikutanisha timu ambazo zinashika nafasi ya tatu na nne kwenye msimamo wa ligi huku zikipishana pointi nne, Azam inazo 51 na Singida Black Stars imefikisha 47.
Kupishana pointi hizo zinaufanya mchezo kuwa mgumu kwani Singida ikishinda, itapunguza gepu na kubaki moja kitu ambacho Azam hataki kuona kikitokea kwani inataka kumaliza ligi si chini ya nafasi iliyopo sasa.
Timu hizo zimetoka kufanya kweli mechi zao za mwisho ugenini, Azam ikiichapa KenGold mabao 2-0 na Singida Black Stars ikiifunga Fountain Gate 3-0. Mchezo wa duru ya kwanza, Azam ikiwa nyumbani ilishinda 2-1.
DODOMA JIJI V KENGOLD
Ni mchezo mwingine kwa KenGold kupigania uhai wao kwenye ligi kufuatia kuburuza mkia na pointi 16 baada ya kucheza mechi 24, ina mechi sita tu za kupambania kubaki. Dodoma Jiji itaikaribisha KenGold kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma, mchezo utakaofanyika saa 12:30 jioni.
KenGold kupoteza mchezo huu kwao itakuwa hatari zaidi kwani itawasogeza karibu zaidi na shimo la kushuka daraja huku Dodoma Jiji nayo ikipambana kushinda kutafuta nafasi ya kujihakikishia kubaki kwani hivi sasa ipo nafasi ya nane kabla ya mechi za jana ikikusanya pointi 28.
NAMUNGO V KMC
Funga dimba kwa Jumapili hii ni mchezo huu utakaofanyika kwenye Uwanja wa Majaliwa uliopo Ruangwa mkoani Lindi kuanzia saa 3:00 usiku. Timu zote hizi bado hazina uhakika wa kubaki kwenye ligi kufuatia pointi walizopishana KMC ikiwa nazo 27 huku Namungo ikikusanya 24.
Namungo ikishinda, inamaanisha itazifikia pointi za KMC na kuongeza presha zaidi kwa WanaKinondoni hao kupambania mechi zilizobaki kuepuka kushuka daraja. Hata hivyo, matokeo ya mchezo wa duru la kwanza yanaifanya KMC kuingia kwa kujiamini kutokana na kushinda nyumbani 1-0, huku pia mchezo uliopita ikiichapa Tanzania Prisons 3-2. Mara ya mwisho zilipokutana uwanjani hapo msimu uliopita Agosti 19, 2023, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1, huku rekodi za jumla zikionesha tangu msimu wa 2019-2020, KMC imeshinda mechi tatu pekee dhidi ya mbili za Namungo kati ya mechi 11, huku sare zikitawala ambazo ni sita.