Ligi Kuu Bara inavyotazamwa kwa jicho la kibiashara

Shirikisho la Kimataifa la Historia na Takwimu za Mpira wa Miguu (IFFHS) limeitangaza Ligi Kuu ya Tanzania Bara kuwa ligi ya nne (4) kwa ubora barani Afrika na ya 57 duniani kwa mwaka 2024.

Ligi hiyo imepanda kwa nafasi mbili kutoka nafasi ya sita mwaka 2023 ikizipiku Ligi za Afrika Kusini na Tunisia ikiwa nyuma ya vinara Ligi Kuu ya Misri inayoongoza, Morocco iliyopo nafasi ya pili na Algeria inayoshika nafasi ya tatu huku Tunisia ikikamilisha tano bora kwa Afrika.

Kabla ya hapo, ligi hiyo mwaka 2021 ilishika nafasi ya 10 Afrika kisha 2022 ikawa ya tano.

Kupanda huko kwa Ligi Kuu Bara kumezifanya klabu kubwa barani Afrika kutupia macho kusaka wachezaji jambo ambalo linazidi kuifanya ligi yetu kutazamwa kwa jicho la kibiashara.

Kwa misimu miwili mfululizo, tumeshuhudia timu za Ukanda wa Kaskazini na Kusini mwa Afrika zikitajwa zaidi kutaka wachezaji kutoka Ligi Kuu Bara huku zikiwepo dili zilizokamilika.

Biashara zilizofanyika nyingi zimehusisha uwezo binafsi wa mchezaji, achana na ile ya kocha aliyekuwa anafundisha nchini kisha alipoondoka anaondoka na wachezaji aliokuwa akiwafundisha kitu alichokifanya Abdelhak Benchikha aliyetoka Simba na kutua JS Kabylie ya Algeria akiondoka na Sadio Kanouté na Babacar Sarr.

Ishu mpya ni uhamisho wa mshambuliaji Mtanzania Seleman Mwalimu ‘Gomez’ kutoka Singida Black Stars kwenda Wydad Casablanca ya Morocco.

Gomez ambaye alikuwa akicheza Fountain Gate kwa mkopo akiwa mali ya Singida Black Stars, ameondoka akiwa amecheza Ligi Kuu Bara kwa takribani miezi sita akifunga mabao sita.

Mshambuliaji huyo uhamisho wake unatajwa kufikia Sh891 milioni akisaini mkataba wa miaka minne na nusu kuanzia Januari 31, 2025 hadi Juni 30, 2029.

Gomez anakuwa mchezaji wa tano raia wa Tanzania kucheza kwenye Ligi ya Morocco baada ya Simon Msuva, Maka Edward, Nickson Kibabage na Shaban Idd Chilunda ambao walitua kwa vipindi tofauti katika miaka 10 iliyopita.

Msuva alianza kutua Difaâ El Jadida Julai 29, 2017 akitokea Yanga kisha Novemba 10, 2020 akasajiliwa na Wydad.

Julai 2019, Nickson Kibabage alitua Difaa El Jadida ya vijana akitokea Mtibwa Sugar. Alikuwa huko hadi Septemba 5, 2021 aliporejea nchini kujiunga na KMC kisha Mtibwa Sugar, baadaye Fountain Gate na sasa yupo Yanga.

Agosti 2019 ilikuwa zamu ya Maka Edward kutua Morocco katika timu ya Moghreb Atlético Tétouan kabla ya kurejea nchini 2021 akisajiliwa na Geita Gold na sasa yupo JKT Tanzania.

Novemba 6, 2020, Moghreb Atlético Tétouan

ya Morocco ilimsajili Shaban Chilunda kutoka Azam, akaachana na timu hiyo Agosti 2021 ambapo alicheza kwa takribani msimu mmoja pekee.

Ukiweka kando dili la Mwalimu, Kaizer Chiefs imekuwa ikitajwa kuifukuzia saini ya Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam FC.

Dili hilo linapigiwa hesabu kubwa sana na kocha wa Kaizer Chiefs, Nasreddine Nabi ambaye alimfundisha Fei Toto ndani ya kikosi cha Yanga.

Inaelezwa kwamba, majadiliano ya dili hilo yanaendelea kufanyika baina ya viongozi wa Azam na Kaizer Chiefs kuona uwezekano wa kufanya biashara na kiungo huyo ambaye ana mkataba hadi Juni 2026.

Pia Clement Mzize wa Yanga amekuwa akitajwa zaidi kutakiwa na timu za Kaskazini mwa Afrika ikiwemo Wydad na RS Berkane zote za Morocco. Pia Al Ittihad ya Algeria nayo inamuhitaji.

Stephane Aziz Ki wa Yanga, naye anahusishwa na Wydad. Kumbuka Wydad ilikuwa inawahitaji zaidi Aziz Ki na Mzize kipindi hiki, lakini kuna uwezekano wakajiunga na timu hiyo mwisho wa msimu huu.

Ukiangalia mlolongo wa madili hayo, utagundua kwamba ndani ya misimu hii miwili, nyota wanaocheza Ligi Kuu Bara wamekuwa wakitolewa sana macho na klabu kubwa za Afrika, lakini pia hata kutoka nje ya Afrika zinawaangalia kama inavyobainishwa hapa chini.

Fiston Mayele

Msimu wa 2023-2024, Yanga ilifanya biashara ya kumuuza mshambuliaji wake kinara, Fiston Mayele ambaye alifanya vizuri kipindi cha misimu miwili aliyoitumikia timu hiyo aliyojiunga nayo akitokea AS Vita Club ya kwao DR Congo.

Mayele ambaye msimu wa kwanza 2021-2022 alifunga mabao 16 Ligi Kuu Bara na kuwa namba mbili kwa ufungaji wa mabao nyuma ya kinara George Mpole, aliendeleza kuuwasha moto msimu uliofuatia ambao ulikuwa wa mwisho kwake.

Msimu wake wa mwisho 2022-2023, Mayele alikuwa mfungaji bora Ligi Kuu Bara akifunga mabao 17 sawa na Saido Ntibazonkiza aliyekuwa Simba, akiwa pia kinara wa Kombe la Shirikisho Afrika akifikisha mabao saba.

Pia alibeba tuzo ya mchezaji bora wa ligi na bao bora la ligi.

Mayele ambaye kiasili ni mshambuliaji wa kati, pia ana uwezo wa kucheza kama mshambuliaji wa pili na kutokea upande wa kulia. Ubora wake huo ndio uliwafanya mabosi wa Pyramids kutoka Misri kumsajili.

Mkataba wake na Pyramids aliosaini Julai 30, 2023, unatarajiwa kufikia tamati Juni 30, 2026 huku akiwa bado na makali yake ya kucheka na nyavu kwani msimu huu katika michuano yote amefunga mabao tisa na asisti moja akicheza mechi 19.

Kwa mujibu wa mtandao wa Transfermarket unaojihusisha na masuala ya takwimu za soka na thamani za wachezaji, wakati Mayele anatoka Yanga kwenda Pyramids, dau lake lilikuwa Sh1.9 bilioni.

Kipre Junior

Kutoka viunga vya Azam FC, winga huyu raia wa Ivory Coast, Julai 9, 2024 alijiunga na MC Algiers ya Algeria.

Kipre mwenye uwezo wa kucheza winga ya kushoto na kulia, ndani ya MC Algiers mkataba wake unatarajiwa kufikia tamati Juni 30, 2025.

Wakati anatua MC Algiers, Transfermarket ilibainisha kuwa dau lake likuwa Sh729.8 milioni.

Benjamin Tanimu

Ni beki raia wa Nigeria ambaye mara kadhaa amekuwa akicheza timu ya taifa hilo. Agosti 30, 2024 alijiunga na Crawley Town inayoshiriki Ligi Daraja la Pili England akitokea Singida Black Stars huku dau lake likitajwa kufikia Sh2.3 bilioni.

Tanimu mwenye uwezo wa kucheza beki wa kati na kulia, alitua nchini kipindi cha usajili wa dirisha dogo msimu wa 2023-2024 akisajiliwa na Singida Fountain Gate akitokea Bendel Insurance ya kwao Nigeria.

Beki huyo licha ya kusajiliwa na Singida, lakini aliicheza Ihefu kwa muda kabla ya timu hiyo kuitwa Singida Black Stars.

Pale Crawley Town aliyojiunga nayo Agosti 30, 2024, mkataba wake unatarajiwa kumalizika Juni 30, 2026. Msimu huu amecheza mechi tisa, zikiwemo sita za ligi na mbili Kombe la FA.