Licha ya kutolewa waranti wa kumkamata, Gallant apanga safari ya kutembelea Marekani

Waziri wa zamani wa vita wa utawala wa Kizayuni wa Israel Yoav Gallant anapanga kusafiri kuelekea Marekani licha ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kutoa hati ya kumkamata kwa kuhusika na jinai za kivita katika Ukanda wa Ghaza.

Redio ya Jeshi la Israel imesema wakati wa safari yake hiyo Gallant atafanya mazungumzo na maafisa wa usalama wa Marekani.

Hata hivyo tarehe hasa ya kufanyika safari hiyo bado haijatangazwa.

Siku ya Alkhamisi iliyopita, ICC ilitoa hati za kukamatwa Gallant na waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni Benjamin Netanyahu kwa kuhusika na jinai za kivita na jinai dhidi ya ubinadamu huko Ghaza.

Kwa mujibu wa kanuni zake, ICC haiendeshi kesi bila mshtakiwa mwenyewe kuwepo mahakamani; aidha, mahakama hiyo yenye makao yake mjini The Hague haina polisi wa kutekeleza waranti inazotoa, bali inategemea nchi wanachama wake kutekeleza maagizo yake ya kuwatia nguvuni washtakiwa.

Ikulu ya White House ilitangaza siku hiyohiyo ya Alkhamisi kwamba haikubaliani na hati zilizotolewa na Mahakama ya ICC za kuwakamata Netanyahu na Gallant na kuwakabidhi kwa mahakama hiyo.

Hati hizo zimetolewa wakati mashambulizi ya kinyama na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni huko Ghaza yameingia mwaka wake wa pili hivi karibuni, yakiwa tayari yameshaua shahidi zaidi ya Wapalestina 44,200, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

Mashambulizi hayo ya kinyama ya Israel yamewafanya karibu wakazi wote wa Ghaza walazimike kuhama makazi yao huku kukiwapo na mzingiro wa makusudi linaoendelea kuwekewa eneo hilo, ambao umesababisha uhaba mkubwa wa chakula, maji safi na dawa, na kuwafanya Wapalestina wa Ghaza wakabiliwe na baa kubwa la njaa…/