Dar es Salaam. Baada ya mchekeshaji Leornado kushinda tuzo ya ‘Overall Best Comedian Of The Year’ katika usiku wa Tanzania Comedy Award, zilizotolewa jana Februari 22, 2025 kwenye ukumbi wa The Super Dome Masaki, ameeleza furaha yake na kuahidi kuendelea kufanya makubwa zaidi kwenye tasnia ya uchekeshaji.

“Kiukweli tuzo yangu nimeipokea kwa ukubwa kwa sababu ndio tuzo ambayo Overall kati ya wengi. Mimi ndio mkubwa wao kwa hiyo namshukuru Mungu sana, nashukuru mashabiki kwa sababu walikuwa wananipambania sana,” amesema Leonardo.
Leonardo ambaye alikuwa akiwania vipengele vitatu kwenye tuzo hizo, ameongezea kuwa amefarijika sana kushinda kipengele hicho kimoja ambacho ni kikubwa.
“Kichwani nilikuwa nawaza kama nisipopata zile mbili basi nipate hii moja kubwa kwa hiyo nilivyoona nimekosa mbili zile nikasema Eeh! sasa imebaki ile moja kubwa. Lakini nashukuru Mungu nimepata na moyo umesuuzika kwa kweli,” amesema Leonardo.

Hata hivyo, licha ya tuzo hizo kuwa na maneno mengi baada ya kutambulishwa kwake mapema mwaka 2025, kwa upande wake Leornado amesema haki imetendeka na kila aliyechukua tuzo alistahili.
“Nadhani kila sehemu ambayo imeenda tuzo ni sahihi kwa sababu ukiangalia wachekeshaji wengi wamekuwa na muendelezo mzuri wa kufanya kazi za ucheshi kwa mwaka mzima, hivyo ukiangalia unaona kabisa kila aliyechukua amestahili,” amesema Leonardo.
Leornado amezungumzia kumbukumbu yake nzuri aliyoipata usiku huo wa tuzo za wachekeshaji nchini ambazo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na kuhudhuriwa na viongozi wa Basata na Bodi ya Filamu.
“Nadhani ule muda wa maokoto lakini kwanza kufanya tu ucheshi mbele ya Rais ni kitu kikubwa sana. Kwa sababu ametupa muda wake kutusikiliza mawazo yetu lakini matukio yote ni mengi,” amesema.

Ushindi wa tuzo hiyo ya Best Comedian Of The Year Overall umemfanya Leornado kukabidhiwa Sh30 milioni kutoka kwa waandaji wa tuzo hizo chini ya mmiliki wa mchongo huo, Omary Nyembo ‘Ommy Dimpoz’ lakini pia kwa kila mchekeshaji aliyepafomu mbele ya Rais alipata bahasha ya fedha.